Uturuki: Meya wa Istanbul anayezuiliwa ateuliwa kuwa mgombea Urais na chama chake

Meya wa upinzani wa Istanbul Ekrem Imamoglu, aliyesimamishwa kazi na kufungwa Jumapili, Machi 23, ameteuliwa rasmi na chama chake kuwa mgombea wa uchaguzi ujao wa urais uliopangwa kufanyika mwaka 2028, msemaji wa chama hicho ameliambia shirika la habari la AFP.

Imechapishwa:

Dakika 1

Matangazo ya kibiashara

Chama cha Republican People’s Party (CHP, social democrat), kikosi kikuu cha upinzani, kilifanya uchaguzi wa mchujo siku ya Jumapili ambapo Ekrem Imamoglu, mpinzani mkuu wa Rais Recep Tayyip Erdogan, ameteuliwa kuwa mgombea pekee.

Siku ya Jumapili Machi 23, 2025 jaji aliamuru kufungwa kwa Ekrem Imamoğlu, mpinzani mkuu wa Rais Recep Tayyip Erdogan kwa makosa ya “ufisadi”. Pia alifukuzwa kazi. Ekrem Imamoğlu anashutumu “kunyongwa bila kesi.” Uamuzi wa kumfungwa jela unaweza kuzidisha hasira inayotanda nchini, kwani ulikuja siku chache kabla ya kuteuliwa kuwa mgombea mkuu wa upinzani katika uchaguzi wa urais wa mwaka 2028.

Ekrem Imamoğlu, ambaye kifungo chake kiliombwa na upande wa mashtaka, anatuhumiwa kuongoza “kundi la wahalifu.” Anashitakiwa katika mifumo miwili ya uchunguzi, mmoja kwa “ufisadi” na mwingine “kusaidia kundi la kigaidi,” Chama cha Wafanyakazi wa Kurdistan (PKK).

Kwa kuwa kifungo hicho kimewekwa kama sehemu ya uchunguzi  wa kwanza, na sio kwa tuhuma za ugaidi, viongozi wa Uturuki hawawezi kuweka jiji kubwa zaidi la nchi chini ya usimamizi. Hii labda ni kwa matumaini ya kutuliza au kudhibiti mivutano mitaani.

Baraza la halmashauri ya Istanbul linaloshikiliwa na upinzani linatarajiwa kumchagua meya mpya katika siku zijazo. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *