Utupaji taka ovyo aibu, sote tuukatae

Gazeti hili wiki hii limechapisha mfululizo wa makala zinazohusu tatizo la kuzagaa kwa taka katika miji mbalimbali nchini.

Hali hii inatokana na sababu mbalimbali zinazomhusu kila mwananchi na ulegevu kwenye usimamiaji wa sheria.

Suala la usimamizi wa taka si la Serikali pekee, bali linahitaji mchango wa jamii nzima. Kila mmoja anapaswa kujiuliza kwa nini anatupa taka ovyo; kwenye makazi yake, mitaroni, barabarani, au hata katika vyanzo vya maji. Ni wazi kuwa suluhisho la kudumu linahitaji mabadiliko ya tabia kupitia elimu na utekelezaji thabiti wa sheria za mazingira.

Tatizo la utupaji ovyo wa taka limekuwa janga kubwa katika miji mingi, hasa Dar es Salaam ambako kila siku, tani 4,500 za taka huzalishwa jijini, lakini ni nusu tu ndiyo hukusanywa ipasavyo.

Matokeo yake ni mirundikano ya taka mitaani, mitaroni na hata kwenye vyanzo vya maji, hali inayosababisha magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu na kuhatarisha afya ya wananchi.

Pamoja na jitihada za Serikali na wadau mbalimbali, bado tatizo hili linasalia kuwa changamoto. Suluhisho la kudumu linahitaji mabadiliko ya kimtazamo kupitia elimu ya utunzaji wa mazingira kwa kila mtu, kuanzia ngazi ya familia hadi taifa kwa jumla.

Elimu ya mazingira ni silaha muhimu katika kumaliza tatizo hili. Wananchi wengi wanapuuza athari za utupaji hovyo wa taka kwa sababu ya uelewa mdogo wa madhara yake. Watu wanahitaji kufahamu kuwa taka zinapotupwa ovyo huchafua mazingira, huharibu mifumo ya maji na hata kuathiri hali ya hewa kwa kuleta gesi hatari.

Ikiwa elimu ya utunzaji wa mazingira itaingizwa katika mitalaa ya shule na kufundishwa kwa vitendo, watoto watakua wakijua wajibu wao wa kutunza mazingira, hivyo kupunguza tabia ya kutupa taka ovyo.

Aidha, jamii inapaswa kuelewa kuwa utunzaji wa mazingira ni jukumu la kila mtu, si la Serikali pekee. Ikiwa kila mmoja atawajibika ipasavyo, hali ya usafi itaboreshwa kwa kiwango kikubwa.

Elimu ya kutenganisha taka, kutafuta mbinu mbadala za kuzitumia tena, na kushiriki katika shughuli za urejelezaji ni njia mojawapo ya kupunguza uchafuzi wa mazingira.

Nchi nyingi zilizoendelea zimefanikiwa katika kudhibiti taka kwa kuwaelimisha wananchi wake juu ya njia bora za kushughulikia taka. Tanzania inapaswa kufuata mfano huo kwa kuhamasisha jamii kushiriki kikamilifu katika utunzaji wa mazingira.

Zaidi ya elimu kwa wananchi, mamlaka husika zinapaswa kusimamia sheria za usafi kwa ukamilifu. Kukiwa na adhabu kali kwa wanaotupa taka ovyo, watu watachukua hatua madhubuti za kuhakikisha wanatunza mazingira yao.

Katika baadhi ya miji, raia wanajua kuwa ukitupa taka ovyo utakumbana na mkono wa sheria, hivyo wanajiepusha na tabia hiyo. Hii ni mifano inayopaswa kuigwa katika miji yote nchini.

Utupaji ovyo wa taka ni aibu kwa jamii inayotaka maendeleo. Hakuna mji unaoweza kustawi ikiwa umejaa taka mitaani.

Hii ni changamoto inayotugusa wote, na suluhisho lake liko mikononi mwetu. Ni wakati wa kuhamasisha elimu ya mazingira kwa kila mtu, kuanzia majumbani, shuleni na katika jamii kwa jumla.

Tukumbuke kuwa mazingira safi ni afya bora, na afya bora ni msingi wa maendeleo endelevu. Tuukatae utupaji ovyo wa taka, tujenge Tanzania safi na salama kwa vizazi vijavyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *