
Walebanoni saba na Wasyria wengi wameuawa siku ya Jumatatu, Machi 17, katika mapigano yaliyozuka siku moja kabla kwenye mpaka wa Lebanon na Syria. Rais wa Lebanoni Joseph Aoun aliamuru jeshi la Lebanon kulipiza kisasi, kabla ya kukubaliana kusitisha mapigano jioni, kufuatia mazungumzo ya simu kati ya mawaziri wa ulinzi wa nchi hizo mbili.
Imechapishwa:
Dakika 1
Matangazo ya kibiashara
Na mwanahabari wetu mjini Beirut, Paul Khalifeh
Mapigano hayo yalitokea kati ya wanajeshi wa Syria na jeshi la Lebanoni na jamii ya Mashia kutoka uwanda wa Bekaa mashariki. Nguvu ya mapigano ilipungua polepole wakati wa usiku na utulivu wa kiwango cha juu unatawala kwa sasa katika eneo la mpaka, lililoko mashariki na kaskazini mashariki mwa Lebanoni.
Hata hivyo, mvutano unaendelea huku jeshi la Lebanoni likiendelea kutuma vikosi vyake baada ya Rais Joseph Aoun kuagiza majibu. Upande wa Syria pia jeshi linazidi kujiimarisha.
Milio ya risasi na milipuko ya roketi na makombora viliendelea kusikika siku ya Jumatatu nzima, huku wanajeshi wa Syria wakijaribu kusonga mbele. Mashambulizi hayo yalisababisha uharibifu mkubwa katika takriban miji mitatu ya mpakani mwa Lebanoni.
Hezbollah inakanusha kuhusika kwa namna yoyote
Mapigano hayo yalizuka usiku wa Jumamosi kuamkia Jumapili baada ya koo za Washia wa Lebanon kuwakamata na kuwaua Wasyria watatu waliokuwa wameingia Lebanoni. Hali iliongezeka haraka na makombora yakaanza kurushwa upande wa Lebanoni, na kusababisha jeshi la Lebanoni kuingilia kati.
Mapigano hayo yanatokea katika eneo linalochukuliwa kuwa ngome ya Hezbollah, ambalo limekanusha kuhusika kwa vyovyote katika mapigano hayo. Sambamba na majibu ya kijeshi, Lebanoni imezidisha juhudi za kidiplomasia kujaribu kurejesha utulivu kwenye mpaka. Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi hizo mbili walikutana mjini Brussels kujadili usitishaji vita.