
Dodoma. Wizara ya Madini imewasilisha bajeti yake kwa mwaka 2025/26, huku ikieleza kusudio la kuja na utaratibu wa kudhibiti madini ya Tanzanite kwa kuwataka wakaguzi na wathamini wa madini hayo kuvaa kofia ngumu zenye kamera.
Waziri wa Madini Antony Mavunde leo Mei 2, 2025 ameliomba Bunge limuidhinishie Sh224.98 bilioni katika mwaka 2025/2026, huku miradi ya maendeleo yakitengewa Sh124.60 bilioni sawa na asilimia 55.38 ya bajeti yote ya mwaka huo.
Pamoja na bajeti hiyo, wizara hiyo imepanga kukusanya maduhuli ya Sh1.4 trilioni kwa mwaka 2025/26 ikilinganishwa na Sh1.16 zilizopangwa kukusanywa mwaka 2024/25.
Akiwasilisha bajeti ya wizara hiyo, Mavunde amesema ili kuimarisha udhibiti na kuzuia utoroshaji wa madini ya Tanzanite, katika mwaka 2025/26, wizara yake kupitia Tume ya Madini inakusudia kuja na mfumo na utaratibu thabiti utakaowataka wakaguzi na wathamini wa madini hayo kuvaa kofia ngumu zenye kamera wakati wakitekeleza majukumu yao.
Amesema lengo ni kurahisisha usimamizi na ufuatiliaji wa mwenendo kwenye eneo Tengefu la Mirerani na masoko kunakofanyika biashara ya madini hayo.
“Kutokana na mafanikio yatakayopatikana, utaratibu huu utatumika kwenye madini mengine ya vito,” amesema Mavunde na kuongeza kuwa katika kuimarisha ukusanyaji wa maduhuli na usimamizi wa sekta ya madini, wizara inatarajia kununua magari 26 kwa ajili ya kuimarisha shughuli zitakazotekelezwa na Tume ya Madini.
“Hatua hii itachangia katika kusimamia ukusanyaji wa maduhuli, udhibiti wa utoroshwaji na biashara haramu ya madini pamoja na kufuatilia shughuli mbalimbali za madini,” amesema.
Pia, Mavunde amesema kuanzia Julai 2024 hadi Machi 2025, wizara kwa kushirikiana na mamlaka nyingine za Serikali imefanikiwa kukamata madini ya aina mbalimbali yenye thamani ya Sh17.75 bilioni katika mikoa ya kimadini 12.
Mikoa hiyo ni pamoja na Geita, Ruvuma, Kahama, Mwanza, Shinyanga, Kagera, Dar es Salaam, Mirerani, Simiyu, Singida, Chunya, Arusha, na Lindi.
Amesema madini hayo yaliyokamatwa yalitaifishwa na watuhumiwa 75 walifikishwa kwenye vyombo vya sheria.
“Ni rai yangu kwa wachimbaji na wafanyabiashara wa madini kujiepusha na utoroshaji wa madini ili kuepuka hasara kwenye biashara zao na Taifa kwa ujumla,” amesema.
Vipaumbele vya bajeti
Katika mwaka 2025/2026, Wizara ya Madini imeainisha kutekeleza vipaumbele vinane, ikiwemo kuimarisha ukusanyaji wa maduhuli.
Vingine ni kuongeza mchango wa sekta ya madini kwenye Pato la Taifa, kuendeleza mnyororo wa thamani katika madini muhimu na madini mkakati na kuhamasisha uwekezaji na uongezaji thamani madini.
Mavunde ametaja vipaumbele vingine ni kuimarisha uendeshaji wa minada na maonesho ya madini ya vito, kuongeza uwekezaji kwenye tafiti za madini za kina na kurasimisha, kuendeleza wachimbaji wadogo wakiwemo vijana, wanawake na watu wenye ulemavu pamoja na kuzijengea uwezo taasisi zilizo chini ya Wizara ya Madini.
Aidha, amesema msimamo wa Serikali kwamba hatutatoa Leseni za uchimbaji wa kati (ML) na mkubwa (SML) wa madini muhimu na ya mkakati kwa mwekezaji yeyote kama hatokuwa na mpango mzuri wa kuongeza thamani ya madini hayo hapa nchini.
“Lengo ni kuifanya nchi yetu ya Tanzania kunufaika na rasilimali madini ambayo Mwenyezi Mungu ametujalia,” amesema Mavunde.
Amesema pia wizara itakamilisha na kuanza kutekeleza mikakati iliyoanishwa kwenye mkakati wa madini muhimu na madini mkakati.
Amesema lengo la mkakati huo ni kuwezesha Serikali kusimamia madini hayo na kupata manufaa zaidi kwa kuboresha maisha ya Watanzania na kuleta maendeleo endelevu kwa nchi.
Uzalishaji wa Kiwira kuanza
Mavunde amesema Shirika la Madini Taifa (Stamico), litaendelea na uzalishaji mkubwa wa makaa ya mawe katika eneo la Kabulo-Kiwira na katika mwaka 2025/2026 jumla ya tani 732,770 zimepangwa kuchimbwa.
“Ili kuimarisha na kuongeza uzalishaji huo, shirika limepanga kununua mitambo na vifaa mbalimbali, vikiwemo dump trucks (3), bulldozer D8 (1), longwall coal shearer (2), Hydraulic Prop (1), kifaa maalum cha mawasiliano mgodini (1) na excavator (1) yenye uwezo wa tani 50,” amesema.
Aidha, Mavunde amesema katika kuboresha huduma za maabara, Taasisi ya Jiolojia na Utafiti Tanzania (GST) itaendelea kufanya uchunguzi kwa kuzingatia vigezo vya ithibati.
“GST itajenga maabara mpya ya kisasa (State of the Art Geoscientific Laboratory) katika eneo la Kizota Dodoma,” amesema.
Amesema maabara hiyo itafanya uchunguzi wa madini, ikiwemo yale yanayohitajika kwenye nishati safi kama vile nickel, cobalt na lithium.
Aidha, Mavunde amesema GST itaendelea na ujenzi wa maabara nyingine katika maeneo ya Chunya-Mbeya na Geita kwa lengo la kusogeza huduma karibu na wananchi wanaojihusisha na shughuli za madini.
Kuhusu wachimbaji wakubwa, Mavunde amesema wizara imefanya majadiliano na wachimbaji wakubwa wa madini ya dhahabu nchini kwa ajili ya kutenga asilimia 20 ya sehemu ya uzalishaji wao ili isafishwe katika viwanda vilivyopo na kuuzwa nchini.
Kupitia utaratibu huo, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeendelea kununua na kuhifadhi dhahabu na hadi kufikia Machi 2025, kiasi cha tani 3.16 zimenunuliwa kutoka kwa wachimbaji wadogo na wa kati.
Kuhusu utafiti, wizara hiyo ipo katika hatua za utekelezaji wa kurusha ndege za utafiti wa madini kwa njia ya high-resolution airborne geophysical survey kwenye maeneo ya wachimbaji wadogo.
Katika kutekeleza hilio, Wizara ya Madini imefanya majaribio kwa kurusha ndege nyuki katika maeneo ya Mkoa wa Dodoma, Shinyanga, Geita, Lindi na Mkoa wa kimadini Mirerani.
Wachimbaji wadogo
Mavunde amesema ili kuwawezesha wachimbaji wadogo wanufaike na rasilimali madini, Serikali imeunda timu ya wataalamu sita wenye uzoefu na masuala ya fedha, madini na sheria kwa ajili ya kutoa mapendekezo ya namna ya kuwawezesha wachimbaji wadogo kupata mitaji.
“Hatua hii itawawezesha wachimbaji hao kufanya uchimbaji wenye tija na kunufaika zaidi kiuchumi,” amesema.
Aidha, Mavunde amesema wizara kupitia Stamico itaendelea kuwalea na kuwaendeleza wachimbaji wadogo kwa kuwajengea vituo vya mfano vya kuchenjua dhahabu kwa kusimika mitambo mingine ya CIP katika maeneo yenye uchimbaji mdogo.