Utofauti wa JKT Queens, Simba Queens kubeba ubingwa leo uko hapa

Utofauti wa JKT Queens, Simba Queens kubeba ubingwa leo uko hapa

Dar es Salaam. Mzunguko wa mwisho wa Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) msimu wa 2024-2025, unahitimishwa leo Mei 20, 2025 kwa mechi tano kuchezwa kwenye viwanja tofauti.

Timu mbili za Mlandizi Queens na Gets Program tayari zimeshuka daraja wakati leo mashabiki wakiwa macho kufahamu nani atatwaa ubingwa wa michuano hiyo kati ya Simba na JKT Tanzania ambazo zitakuwa kwenye viwanja viwili tofauti.

Katika kuhitimisha msimu, michezo miwili ambayo Gets Program dhidi JKT Queens na Alliance Girls dhidi Simba Queens, itaenda kuamua bingwa wa ligi hiyo kutokana na msimamo ulivyo.

JKT Queens na Simba Queens zimelingana pointi kwenye msimamo zote zikiwa na 44, baada ya kucheza mechi 17 zikitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa tu, huku kila moja ikiwa imepoteza mchezo mmoja.

Ili Simba Queens itetee ubingwa wa ligi hiyo, inatakiwa kushinda dhidi ya Alliance Girls huku ikiombea JKT Queens ipoteze au kutoka sare dhidi ya Gets Program.

Msimamo wa ligi hiyo unaonyesha kuwa JKT ndiyo kinara wa kufunga mabao ikiwa na tofauti ya mabao kumi zaidi ya Simba, lakini pia ikiwa imeruhusu mabao saba tu na Simba imeruhusu 15, hivyo kinga kubwa kwa Simba kutwaa ubingwa hapa ni kuhakikisha JKT inapoteza au inatoa sare nayo inashinda mchezo wa leo.

JKT Queens inausaka ubingwa wa ligi hiyo ilioupoteza msimu uliopita huku ikifukuzia rekodi ya Simba Queens inayoongoza kubeba mara nne. Kwa sasa JKT Queens imeshinda ubingwa huo mara tatu na kama itautwaa leo basi itakuwa mara ya nne.

Mabingwa waliopita

Rekodi za mabingwa wa Ligi Kuu Wanawake zinaonyesha hivi; Mlandizi Queens (2017), JKT Queens (2017/2018), JKT Queens (2018/2019), Simba Queens (2019/2020), Simba Queens (2020/2021), Simba Queens (2021/2022), JKT Queens (2022/2023) na Simba Queens (2023/2024).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *