Utekelezaji wa hukumu ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC), mtihani kwa Wamagharibi

Ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya haki za binadamu huko Palestina amesema kuwa utekelezaji na kushikamana nchi za Magharibi na uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) wa kuwakamata viongozi wa utawala wa Kizayuni ni mtihani wa kupima azma na uwajibikaji wa Wamagharibi kuhusu hukumu hiyo.

Francesca Albanese ameongeza kuwa: “Amri ya kukamatwa Benjamin Netanyahu na Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni na Yoav Gallant, Waziri wa Vita wa zamani wa utawala huo, kwa hakika ni utekelezaji wa madai yetu ya kupatikana haki na kuadhibiwa wahusika wa vita na mauaji  ya kimbari. Aidha ameonya kuhusu mgawanyiko baina ya nchi za Magharibi kuhusiana na hukumu ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC).

Hukumu ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai dhidi ya wahalifu wa utawala wa  Israel

Matamshi ya Francesca Albanese, yamekuja baada ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) ya The Hague, baada ya miezi kadhaa ya jinai za kivita zinazofanywa na utawala katili wa  Israel dhidi ya Wapalestina, kutoa waranti  ya kukamatwa  Benjamin Netanyahu na Yoav Gallant kwa tuhuma za uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya ubinadamu na matumizi ya njaa kali dhidi ya  watu  wa Ukanda wa  Gaza kama silaha ya vita. Hii ni mara ya kwanza kwa Mahakama ya The Hague kuamuru kukamatwa viongozi wakuu wa utawala haramu wa  Israel.

Hata hivyo na baada ya miezi kadhaa ya vita vya Gaza, hukumu ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC)  imetolewa, huku Wizara ya Afya ya Gaza ikitangaza katika habari zake za hivi karibuni kwamba idadi ya mashahidi wa Gaza tangu kuanza kwa vita vya Gaza ni zaidi ya 44,000  na idadi ya waliojeruhiwa ni zaidi ya 104,000. Mauaji na jinai za Israel pia zingali zinaendelea hadi sasa, na  njia za kutoa misaada kwa Gaza bado zimefungwa na misaada ya UNRWA pia imekatwa.

Katika hali hii, uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya jinai umekabiliwa na hisia tofauti kutoka nchi za Magharibi. Rais Joe Biden wa Marekani ameitaja hatua ya mahakama ya ICC mjini The Hague kuwa ya kidhalimu na kwa mara nyingine tena kusisitiza uungaji mkono wake wa hali na mali kwa utawala huo pandikizi wa  Israel. Victor Orban,  Waziri Mkuu wa Hungary, ambaye nchi yake inashikilia urais wa zamu wa Umoja wa Ulaya, amesema kuwa  anamwalika Netanyahu, waziri mkuu mwenzake wa Israel kutembelea Budapest na kwamba haheshimu agizo hilo la mahakama ya (ICC).

Kuchukuliwa msimamo kama huo kumezitia wasiwasi taasisi za haki za binadamu kiasi cha kumfanya ripota maalum wa Umoja wa Mataifa kutoa onyo kali kuhusu suala  hilo.

Francesca Albanese amesema: “Nchi kama Marekani, Hungary na nyinginezo zinazoendelea kuiunga mkono Israel bila kujali hali ya sasa huko Gaza na kuihadhalilisha Mahakama ya Kimataifa ya Jinai katika hali ambayo kutolewa waranti ya kukamatwa Netanyahu na Gallant ni nukta muhimu katika historia ya dunia.

Kwa hakika, mashirika ya kutetea haki za binadamu yana wasiwasi mkubwa kuhusu uungaji mkono huo wa nchi za Magharibi ambao unaufanya utawala katili wa Israel uendeleze jinai zake huko Gaza. Utawala haramu wa Israel, ambao  umethibitisha kwa miaka mingi kwamba  hauzingatii sheria wala kanuni zozote za kimataifa umechukua msimamo dhidi ya uamuzi huo, na washirika wake pia kuunga mkono katika hilo. Hii ni katika hali ambayo  muendelezo wa hali hii bila shaka utazidisha maafa ya kibinadamu huko Gaza. Kwa msingi huo maafisa wa Umoja wa Mataifa wanasema utekelezwaji wa hukumu hiyo ni mtihani mkubwa kwa nchi za Magharibi wakupima iwapo zinaheshimu kisheria za kimataifa kama zinavyodai au la.

Natalie ‎Buckley,  naibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA), pia ameashiria hati ya kukamatwa wanasiasa waandamizi wa Israel na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai kama “kushughulikiwa mateso wanayopata mamilioni ya watu.”  Huku akiashiria ukweli kwamba “kimsingi watu wa Gaza wanakodolewa macho na baa la njaa kali” na hivyo wanahitajia sana msaada wa dharura, amesema kuwa viongozi  wanapaswa kuwajibika kwa ukiukwaji wote wa sheria za kimataifa unaofanyika, na uamuzi wa sasa wa Mahakama ya Jinai dhidi ya maafisa wawili wa Israeli ni mwanzo wa uwajibikaji huo.

Hata hivyo, baadhi ya nchi za Magharibi hazionekani kuwa na wajibu wa kutekeleza hukumu hii au kujaribu kusimamisha jinai zinazotendwa na utawala  wa Israel, kwani ndani ya siku mbili tu baada ya uamuzi wa mahakama ya ICC, azimio lililopendekezwa kusitisha vita huko Gaza katika Usalama lilipingwa na Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya, ikiwemo Ujerumani, na kukisisitiza kuendelea kuutumia silaha utawala huo wa Kizayuni.