
WAKATI uongozi wa Fountain Gate ukipanga kukutana na kipa wa timu hiyo, John Noble ili ajibu tuhuma za kucheza chini ya kiwango, mwenyewe anadaiwa kutopatikana huku ikidaiwa kwamba kaondoka nchini kimyakimya kurudi kwao Nigeria.
Mwanaspoti limefanya juhudi za kumtafuta Noble, lakini hajapatikana na wala simu yake ya mkononi haikupatikana na hata alipotumiwa ujumbe wa maandishi wa kawaida na ule wa WhatsApp hauonekani kusomwa na hata simu yake haionyeshi kuwa hewani.
Sakata la kipa huyo lilianza baada ya mchezo dhidi ya Yanga uliochezwa Aprili 21, 2025 kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa uliopo Babati mkoani Manyara, ambapo aliruhusu mabao mawili kipindi cha kwanza katika kipigo cha mabao 4-0 ilichopata timu hiyo.