Utaratibu wa Kanisa Katoliki wa kufuata pale tu kifo cha Baba Mtakatifu kinapokuwa kimetokea

UTANGULIZI: Waheshimiwa na wapendwa, poleni sana na kifo cha Baba Mtakatifu Francesco: Papa, wakili wa Kristo, alifa wa Mtume Petro, Daraja la Juu la Kanisa Katoliki (Supreme Pontiff of the Catholic Church), Daraja la Juu la Kiroma (Roman Pontiff), Patriacha wa Magharibi (cheo hiki kilikuwa kimeondolewa wakati wa upapa wa Baba Mtakatifu Benedict XVI, kikarejeshwa wakati wa upapa wa Baba Mtakatifu Francesco), Mtumishi wa watumishi wa Mungu, wa kwanza kwa Ukuu (Primate) katika Italia na Metropolitano wa Provinsia ya Roma, na Mtawala wa Dola ya Vatikano (Sovereign of the Vatican City State).

 Tunaendelea kumlilia Baba Mtakatifu Francesco na kumuombea pumziko la milele mbinguni. Naomba tuzungumzie linalofuata baada ya kifo chake. Apumzike kwa amani mbinguni.

MADA YENYEWE: Ili kuelewa vizuri utaratibu wa kufuata pale Baba Mtakatifu anapokuwa ameaga dunia waweza kuelewa vizuri zaidi ikiwa mwenye kutaka kuufuata atasoma kwa umakini nyaraka zifuatazo mintarafu utaratibu wa kufuata baada ya kifo cha Baba Mtakatifu:

(i) Maelekezo mintarafu taratibu za kufuata baada kifo cha Papa. Waraka huu ulitolewa na Baba Mtakatifu Paulo VI mnamo mwaka 1975. 

(ii) Universi Dominici Gregis (yaani, Mchungaji wa kundi lote la Bwana). Waraka huu ulitolewa na Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili.

(iii) Normas Nonnulas (yaani, Baadhi ya Kanuni). Waraka huu ulitolewa na Baba Mtakatifu Benedikto XVI mnamo mwaka 2013. 

Kwa ufupi waraka tajwa wa Baba Mtakatifu Paulo VI ulitamka yafuatyo:

Camerlengo, yaani, msimamizi mkuu wa nyumba ya kitume [apostolic palace] na mali za kitume [apostolic heritage], wa Kanisa Takatifu la Roma [hapa inamaanisha DAYOSISI YA ROMA] ATATHIBITISHA KIFO CHA PAPA.

(a) Itampasa Camerlengo kumjulisha Kardinali Wakili kwa ajili ya Jiji la Roma (Cardinal Vicar for the City of Roma). Itambidi Kardinali Wakili kuwajulisha waamini wa Dayosisi ya Roma. NB: Ikumbukwe, kwa kawaida Baba Mtakatifu, kama Askofu wa Dayosisi ya Roma, anakuwa na mawakili (Vicars general) wawili: Kardinali Wakili kwa ajili ya Jiji la Roma (Cardinal Vicar for the City of Rome) na Kardinali Wakili kwa ajili ya Jiji-Dola ya Vatikano (Cardinal Vicar for the Vatican City State).

(b) Itambidi Camerlengo kufunga kwa ‘seal’ maalumu vyumba vyote vya kipapa.

(c) Hatua za mazishi zitafanyika na kutangazwa.

(d) Makardinali watakusanyika kwa mkutano maalumu wa faragha (conclave) kwa lengo la kumchagua Papa.

(e) Hakuna Kardinali mwenye umri zaidi ya miaka 80 atashiriki mkutano (conclave) wa kumchagua Papa.

Kwa ufupi, waraka tajwa hapo juu, yaani, Universi Dominici Gregis wa Baba Mtakatifu Yohane Paulo II ulisema yafuatayo mintarafu kiti cha Kitume kinapokuwa wazi:

(a) Kiti cha Kitume kinapokuwa wazi, makardinali hawatakuwa na uwezo (jurisdiction) juu ya shughuli zote zilizomhusu Baba Mtakatifu wakati wa uhai wake au yaliyohusu ofisi yake kama Papa. Mambo hayo yote yatamsubiri Papa atakayemrithi.

(b) Wakati kiti cha kitume kinapokuwa wazi, utawala wa Kanisa unakuwa mikononi mwa Baraza la Makardinali kwa mambo yale tu ambayo hayawezi kuahirishwa; na kwa mambo yanayohusu maandalizi ya kumchagua Papa.

(c) Baraza la Makardinali haliwezi kufanya mabadiliko yoyote kuhusu haki za Kiti cha Kitume na za Kanisa la Roma (Dayosisi ya Roma), bali kwa pamoja watalinda haki hizo.

(d) Wakati Kiti cha Kitume kinapokuwa wazi, sheria zilizotungwa na Papa haziwezi kusahihishwa au kurekebishwa; na hakuna chochote kiwezacho kuongezwa au kuondolewa, na hakuna yeyote anayeweza kupata kibali cha kutozifuata.

(e) Kama kuna jambo halieleweki kuhusu sheria na kanuni yoyote wakati kiti cha kitume kinapokuwa wazi, ni baraza la makardinali lenye uwezo wa kushughulikia mashaka hayo na kutoa tafsiri sahii ya jambo/mambo hayo. Ili hili lifanyike inalazimu sehemu kubwa ya makardinali wawepo (simple majority).

(f) Kama kuna jambo litajitokeza ambalo haliwezi kuahirishwa, Baraza la Makardinali litashughulikia jambo hilo na kutoa jibu kwa mujibu wa kauli ya makardinali walio wengi (voice of the simple majority). 

Kwa ufupi, waraka tajwa (Normas Nonnulas) wa Baba Mtakatifu Benedict XVI ulisema yafuatayo kama nyongeza kwa nyaraka tajwa hapo juu, hasa waraka Universi Dominici Gregis:

(a) Makardinali wanatengewa eneo ndani ya jiji la Vatikano pasipo kuwasiliana na watu wa nje wakati wote wa mkutano wa faragha (conclave).

(b) Theluthi mbili kuongeza kura moja zitahitajika kumtangaza Papa.

(c) Baba Mtakatifu aliyechaguliwa atavaa kanzu nyeupe akiwa ndani ya Chumba cha Machozi kabla hajarudi kwenye chumba cha faragha (conclave). Chumba cha machozi ni tafsiri ya “Stanza delle Lacrime” ikimaanisha “Room of Tears” kwa Kiingereza. Chumba hiki kidogo wakati mwingine kinaitwa “Stanza del Pianto” yaani, chumba cha mwenye kulia.

Ni imani yangu dondoo hizi zimetoa mwanga na kuondoa dukuduku juu ya taratibu za kufuata kama Baba Mtakatifu amekufa au kama kiti cha papa ki wazi kwa sababu nyingine.

Ikumbukwe pia kuwa Camerlengo huthibitisha kifo cha Papa mbele ya Mliturjia Mkuu wa Kipapa (Papa Master of Ceremonies) na mbele ya wajumbe wengine wakaao katika nyumba ya kipapa.

Vilevile picha au filamu za Papa iwe katika kitanda cha kifo au baada ya kifo haziruhusiwi.

Lakini pia, ikiwa Baba Mtakatifu alikuwa ameandika wosia na kumteua mwosia (executor of the will), mwosia huyo atatoa taarifa juu ya wosia huo kwa Papa mpya tu.

Kuhusu mazishi ya Papa:

 Baada ya kifo cha Papa kunakuwapo siku kenda (9) za maombolezo, mazishi hufanyika kati ya siku ya 4 na ya 6 baada ya kifo isipokuwa kama kuna sababu maalumu.

Kama Papa hakusema vinginevyo wakati wa uhai wake, kwa kawaida mazishi ya Papa hufanyika ndani ya Basilika la Mt. Petro, ambako mwili wa Papa utawekwa kwa lengo la kutolewa heshima.  

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *