Utani wa Simba na Yanga ulivyompa daktari kiwanja

Dodoma. Si kila utani unasababisha ugomvi bali utani mwingine una manufaa katika jamii katika kuimarisha udugu, ushirikiano na umoja.

Hali hii imejithiirisha katika kijiji cha Ngomai, kata ya Ngomai wilayani Kongwa, ambapo mashabiki wa Simba na Yanga, wameamua kutumia utani kukusanya fedha kwa ajili ya kumzawadia kiwanja daktari Peter Mwakalosi  anayewahudumia.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu, Septemba 23, 2024, Mwenyekiti wa Kijiji wa Ngumai, Sospeter Chamasi amesema waliamua kufanya hivyo kutokana na daktari huyo  kujituma kwa bidii.

“Ana mapokeo mazuri mgonjwa anapofika pale usiku akimwambia samahani kwa kuamsha, yeye majibu yake huwa ni kuwa ugonjwa wala ajali haina saa wala tarehe au muda, hivyo niamsheni muda wowote. Anasema mimi nimeacha wazazi wangu kuja kuwahudumia kuwatumikia nyinyi,”anasema mwenyekiti huyo.

Anasema ujumbe huo umewafurahisha wanakijiji wengi hasa kutokana na daktari aliyekuwepo kabla yake kuwa mlevi sana wa pombe na kila walipokuwa wanakwenda kutibiwa iliwalazimu kumtafuta katika vilabu vya pombe.

Anasema tangu mwaka 2005, alipofika daktari huyo (Peter), hadi leo hajawahi kutoka tena katika zahanati hiyo na mambo yalibadilika katika utoaji wa huduma za afya kwa wananchi kupata huduma nzuri.

“Ngumai kuna utani wa Simba na Yanga, sasa Simba wakasema kwa nini tusimtunuku daktari wetu ni mtu anayejituma sana. Muda wote hamyanyapai mgonjwa. Ilikuwa Aprili wakati ligi inaishia baadaye wakati wakitambulisha wachezaji suala hilo likaibuliwa tena tukaamua kufanya tamasha letu,” amesema.

Chamasi amesema katika tamasha hilo watani kutoka Simba walitoa Sh600,000 na wadau wengine katika tamasha hilo walichangia zaidi ya milioni tatu na hivyo kufanya jumla ya michango hiyo kuwa Sh4 milioni.

Amesema kati ya fedha hizo walinunua kiwanja chenye thamani ya Sh3.6 milioni ambacho kina ukubwa wa robo tatu eka na nyumba mbili ambazo zina matofali siyo wa kuchoma.

Anasema katika kumwezesha kujenga nyumba Serikali ya kijiji imemchangia mifuko 60 ikiwa ni kuwaunga mkono wananchi kwa wazo walilolitoa.

Daktari azungumza

Dk Mwakalosi amesema anamshukuru Mungu kwa kitendo walichomfanyia wana kijiji hao.

“Sauti ya wengi ni sauti ya Mungu, ukiona watu wamefanya hivyo maana wamekupima kwa muda kadhaa kwa sababu nikipiga hesabu sasa huu ni mwaka wa 19 nimekaa hapa. Ukiona kipindi chote hawakufanya, ina maana wamekuchambua.”

Anasema anajua kilichomsababishia kupewa zawadi hiyo ni kutokana na kujituma kwake kwa bidii usiku na mchana bila kujali ugumu wa kazi wanayoifanya.

“Licha ya ugumu huo, ukiendelea kuamshwa na kuamka, sana ni kujituma kwa moyo katika kazi tunazozifanya bila kuchoka.

“Japokuwa tunachoka unamuomba Mungu akuongezee nguvu ufanye kazi,” anasema.

Anasema jambo lingine ni kushirikiana na jamii kunapotokea matukio ya kijamii na kwamba hata kunapotokea changamoto ya usafiri hujitolea usafiri wake katika kuisaidia jamii.

Dk Mwakalosi amesema kwa mwezi wanawahudumia wagonjwa wasiopungua 500 kutoka katika maeneo mbalimbali ya kata ya Ngomai.

Zahanati hiyo ina watumishi watano na wawili kati ya hao wanafanya kazi kwa kujitolea ambao ni daktari na muuguzi.

“Chumba cha kujifungulia ni kidogo na bahati nzuri huku watu wanajitahidi katika kujifungulia kwenye zahanati, sisi kwa mwezi tunawasaidia kujifungua wanawake kuanzia 30 hadi 40,” anasema.

Amesema wakati mwingine wanajifungua wanawake hadi watano kwa siku moja na hivyo eneo linakuwa dogo, hivyo wanaomba msaada wa kuboreshewa eneo hilo.

Anapoulizwa wito wake kwa watumishi wengine, Dk Mwakalosi amesema kazi hiyo ni wito hivyo wakisimamia katika uaminifu na uadilifu wana thawabu kubwa sana kwa Mungu.

Amesema anafahamu kuwa wanachoka kwa kiasi kukubwa kutokana na kazi ngumu wanayoifanya na tena yenye viatarishi vingi.

“Lakini niwatie moyo wenzangu kuwa kazi ni ngumu lakini cha kwanza tumuombe Mungu tuendelee kufanya kazi hii kwa bidii tutambue kazi hii ni ya wito na tuitumikie ipasavyo kama viapo vyetu vinavyosema,” amesema Dk Mwakalosi.

Zahanati hiyo inahudumia vijiji vinne vya Wilaya ya Kongwa na vijiji vingine vya Wilaya ya Kiteto Mkoani Manyara.