Jumatano, Aprili 2, 2025, Simba itakuwa ugenini katika mchezo wa kwanza wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya wenyeji wao Al Masry ya Misri kuanzia saa 1:00 usiku kwa muda wa Afrika Mashariki.
Mchezo huo baina ya Al Masry na Simba utachezwa katika Uwanja wa Suez ambao upo katika jiji la Suez lililopo katika Pwani ya Kaskazini ya Misri.

Uwanja huo wa Suez una dondoo mbalimbali ambazo baadhi wanazifahamu na wengi hapa nchini hawazifahamu lakini kupitia mchezo huo baina ya Al Masry na Simba, uwanja huo utakuwa sio mgeni kwa Watanzania.
Mwaka 1990 ndio kipindi ambacho uwanja huo ulifunguliwa rasmi na unamilikiwa na serikali ya Misri chini ya Halmashauri ya Jiji la Suez.
Ni uwanja ambao nyasi zake ni mchanganyiko (hybrid) wa bandia na asilia na unaingiza idadi ya mashabiki 27,000 wakiwa wameketi vitini.

Wakati wa Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2019 ambazo zilifanyika Misri, mechi nane za mashindano hayo zilichezwa katika uwanja huo ambapo sita zilikuwa za hatua ya makundi, moja ya hatua ya 16 bora na nyingine moja ya robo fainali.
Mwaka 2013, Uwanja huo ulifanyiwa ukarabati ambao uligharimu kiasi cha Dola 26 milioni (Sh68.8 bilioni) ukifanywa chini ya mkandarasi mzawa, kampuni ya Arab Contractors.
Uwanja huo una bwawa la kisasa la kuogelea lakini pia kuna uwanja wa kisasa wa ndani ambao unatumika kwa michezo mingine ambayo sio mpira wa miguu.
Katika mechi 10 zilizopita ambazo Al Masry imecheza katika Uwanja wa Suez, imepata ushindi mara nne, kutoka sare nne na kupoteza mechi mbili, ikifunga mabao 14 na imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara tisa.