Utamu, uchungu mgawanyo wa majimbo

Dar es Salaam. Utamu na uchungu, ndiyo maneno mafupi yanayoakisi kilichoelezwa na wadau wa siasa kuhusu matokeo ya uamuzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kugawanya majimbo.

Mgawanyo huo umesababisha kuzaliwa kwa majimbo mapya manane ya uchaguzi na hivyo, kufanya uchaguzi wa baadaye mwaka huu uhusishe jumla ya majimbo 272, Tanzania Bara na Zanzibar.

Uamuzi huo wa INEC, kwa mujibu wa wadau wa siasa, una pande tamu na chungu kwa wabunge wa sasa wenye nia ya kuendelea kugombea nafasi hizo.

Upande mtamu utatokana na kile wanachoeleza, iwapo mgawanyo huo haujagusa eneo ambalo ni mtaji wa kura za mbunge husika, lakini uchungu ni pale ambapo eneo linaloonekana turufu kwa mgombea limegawanywa.

Sambamba na mitazamo kuhusu matokeo ya uamuzi huo kwa wabunge, baadhi ya wadau wanashuku mgawanyo huo umelenga kuwabeba baadhi ya viongozi walioonekana kuwa katika hatari ya kupoteza nafasi zao.

Mgawanyo wenyewe

Kwa mujibu wa taarifa ya mgawanyo wa majimbo hayo iliyotolewa na Mwenyekiti wa INEC, Jaji Jacobs Mwambegele, imesema Jimbo la Ukonga limegawanywa kuzaa jimbo lingine la Kivule, huku Mbagala likigawanywa na kuzaa Chamazi, kama ilivyo kwa Dodoma Mjini lililozaa jimbo jipya la Mtumba.

Kwa upande wa Mkoa wa Mbeya, Jimbo la Mbeya Mjini limezaa jimbo jipya la Uyole, huku Jimbo la Bariadi mkoani Simiyu limezaa jimbo la Bariadi Mjini.

Lililokuwa Jimbo la Busanda mkoani Geita limezaa Jimbo la Katoro, Jimbo la Chato limezaa Chato Kusini, na Solwa la Mkoa wa Shinyanga limemegwa na kuanzishwa Jimbo la Itwangi.

Jaji Mwambegele ametaja vigezo vinne vilivyozingatiwa katika mgawanyo huo, ambavyo ni kwa jimbo la mjini kuwa na idadi ya watu 600,000, na watu 400,000 kwa vijijini.

Uwezo wa ukumbi wa Bunge, idadi ya wabunge wa viti maalumu na jimbo moja kutokuwa katika wilaya au halmashauri mbili, ni vigezo vingine vilivyotumika.

Mgawanyo huo, kwa mujibu wa Jaji Mwambegele, umehusisha pia mabadiliko ya majina ya majimbo. Lililokuwa linaitwa Chato sasa ni Chato Kaskazini, Nkenge litaitwa Missenyi, Mpanda Vijijini litaitwa Tanganyika, na Buyungu litaitwa Kakonko.

Kwa upande wa Jimbo la Bariadi litaitwa Bariadi Vijijini, Manyoni Mashariki litaitwa Manyoni, Singida Kaskazini litaitwa Ilongero, Manyoni Magharibi litaitwa Itigi, Singida Mashariki litaitwa Ikungi Magharibi, na Handeni Vijijini litaitwa Handeni.

Amesema uchaguzi huo utakuwa na jumla ya kata 3,960, zikiongezeka mpya tano ambazo ni Ngereyani, Sinonik katika Halmashauri ya Longido, huku Mupi, Bwawani Mjini na Shela katika Mji wa Rufiji.

Tamu, chungu

Mbunge wa zamani aliyehudumu kwa zaidi ya miaka 20 katika moja ya majimbo nchini, amesema mgawanyo unabeba matokeo hasi na wakati mwingine chanya kwa mbunge husika.

Mwanasiasa huyo aliyeomba hifadhi ya jina lake kwa sababu ya itifaki za nafasi aliyonayo sasa, ameeleza kuwa inakuwa mbaya kwa mbunge iwapo eneo lililomegwa ndilo lililokuwa mtaji wa kura zake.

“Unapokuwa mbunge katika jimbo unaloliongoza, kuna eneo unakubalika na kuna eneo unapigwa vita na hukubaliki kabisa. Sasa kama eneo lililoondolewa ni kule unakokubalika, huo ni mtihani mzito kwako,” amefafanua.

Kwa mujibu wa mwanasiasa huyo mkongwe, itakuwa bahati kwa mbunge kama mgawanyo wa jimbo uliofanywa unamwachia kata au tarafa ambazo ni mtaji kwake.

Amesema hali huwa shwari kwa mbunge husika kama ana uhakika alikuwa anakubalika katika kata zote za jimbo husika.

Kama alivyoeleza mwanasiasa huyo, Mbunge wa Mbagala, jimbo lililogawanywa na kuzaa majimbo ya Mbagala na Chamazi, Abdallah Chaurembo amesema faida na hasara za mgawanyo zinategemea mbunge aliishije na wapigakura.

“Inawezekana ikawa turufu na inawezekana ikawa maumivu. Kikubwa ni namna gani uliishi na watu. Kama umeishi na watu vizuri, jimbo likigawanywa unashindwa kujua uende wapi kwa sababu pande zote zitakuhitaji,” amesema.

Amesema hiyo ndiyo hali inayomkabili yeye kwa sasa baada ya taarifa za kugawanywa kwa jimbo hilo, akisema kila upande anakubalika, hajui aende wapi kati ya Chamazi au Mbagala.

“Kwangu imekuwa kama kuna taharuki jimboni, ukizingatia maeneo yote nina makazi. Hawa wa huku wanataka nibaki huku na wa kule wanataka niende, sasa mtihani ni kuamua,” amesema Chaurembo.

Kwa sababu aliutumia muda wake wa uongozi kutumikia wananchi wote, amesema haimpi wasiwasi wa kura, badala yake amebaki na mkwamo wa kuamua ni wapi aende kwa kuwa kote ana watu.

“Bahati nzuri hata zilipokuja tetesi za mgawanyo, sikubagua, niliendelea kufanya kazi kwa sehemu zote,” amesema Chaurembo.

Kwa mtazamo wa kiuchumi, mgawanyo wa maeneo ya utawala unaongeza gharama za uendeshaji wa Serikali katika eneo husika, hivyo bajeti italazimika kuongezwa, kama inavyoelezwa na mwanazuoni wa uchumi, Profesa Benedict Mongula.

Amesema hali itakuwa mbaya zaidi iwapo gharama za uendeshaji wa Serikali zitaongezeka, lakini ufanisi wa utendaji wa viongozi wa maeneo yaliyogawanywa ukawa kinyume na ilivyotarajiwa.

“Wanagawanya kwa lengo la kuongeza ufanisi wa utendaji na kusogeza karibu huduma kwa wananchi. Inagharimu, lakini gharama hizo zikiambatana na kukosekana kwa ufanisi wa uongozi unaopewa madaraka katika eneo husika, zinakuwa mara mbili zaidi,” amesema Profesa Mongula.

Tiba ya purukushani za kisiasa

Mbio za ubunge katika majimbo ya Mbeya Mjini, Ukonga na Dodoma Mjini zilisababisha purukushani za kisiasa kutoka miongoni mwa wanasiasa wanaonyemelea ubunge majimboni humo.

Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson alikuwa na kibarua kigumu Mbeya Mjini kukabiliana na wanasiasa wengine wa CCM wanaoutaka ubunge jimboni humo, lakini sasa uamuzi unabaki nani aende Uyole na nani abaki Mbeya Mjini.

Mgawanyo umezingatia nini?

Pamoja na ufafanuzi uliotolewa na INEC kuhusu vigezo vya mgawanyo wa majimbo hayo, Mwanazuoni wa Historia ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Bonn nchini Ujerumani, Philemon Mtoi amesema haieleweki tume imezingatia nini.

Kutokuelewa kwake kunatokana na kile alichofafanua kuwa, kuna majimbo yaliyogawanywa yana idadi ndogo ya watu ukilinganisha na baadhi ya maeneo, akitolea mfano Mbeya Mjini dhidi ya Kigamboni.

Kwa mujibu wa Mtoi, pamoja na sababu nyingine, mgawanyo uliofanywa una ishara za kimazingira kuwa umelenga kuwalinda baadhi ya viongozi wanaoonekana wako katika hatari ya kupoteza nafasi zao.

“Inanishangaza pamoja na ufafanuzi wa kikanuni uliotolewa na INEC, bado mgawanyo wa majimbo nchini haufanywi kwa utashi wa kisiasa wa kusaidia watu,” amesema.

Ameijenga hoja yake hiyo akirejea hali ilivyo katika mataifa mbalimbali yenye idadi kubwa zaidi ya wabunge kwa lengo la kusogeza karibu huduma kwa wananchi na kuweka usawa wa uwakilishi.

“Kuna nchi zina wabunge zaidi ya 600 au 700 wakiwa na dhamira ya dhati ya kusaidia watu. Hii itasaidia kila mwananchi awakilishwe katika usawa. Huu mgawanyo umezingatia usawa kwa idadi ya watu au wameangalia nini?” amehoji.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *