Utajiri wa nchi unavyohamishwa kupitia vivutio kwa wawekezaji

Utajiri wa nchi unavyohamishwa kupitia vivutio kwa wawekezaji

Dar es Salaam. Wakati Tanzania ikikadiriwa kuwa na walipakodi karibu milioni tano, kumekuwa na upotevu wa mapato kutokana na vivutio wanavyopewa wawekezaji wa nje ikiwamo misamaha ya kodi na vivutio visivyo vya kifedha.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa bungeni na Wizara ya Fedha, Septemba 2023, hadi Juni 30, 2023, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) hadi wakati huo ilikuwa imesajili jumla ya walipakodi takribani milioni 4.7 ambao ni sawa na asilimia 16 ya nguvu kazi iliyopo nchini.

Pamoja na uchache huo wa walipakodi, bado Tanzania imekuwa ikitoa vivutio au motisha za kikodi kwa wawekezaji ili kuvutia wawekezaji wa ndani na wa nje, hali hiyo wakati mwingine inayochangia utitirishaji wa fedha kwenda nje ya nchi.

Kwa mujibu wa ripoti ya Global Financial Integrity, Tanzania hupoteza zaidi ya Sh4.79 trilioni kila mwaka kutokana na utoroshwaji wa fedha kwenda nje ya nchi.

Pamoja na kuwa motisha hizo zina mchango mkubwa katika kuvuta uwekezaji wa kigeni wa moja kwa moja, pia, inaelezwa kuifukarisha nchi.

Vivutio EPZ, SEZ

Miongoni mwa maeneo yanayotajwa kuchota utajiri wa nchi ni uwekezaji ulio chini ya Mamlaka ya Maeneo Maalumu ya Uzalishaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA), ambapo wawekezaji wamekuwa wakinufaika na vivutio kodi kama vile likizo za kodi, misamaha ya ushuru wa forodha, ushuru wa bandari na VAT kwa malighafi na huduma za msingi.

Kwa mujibu wa Sheria ya EPZ kifungu cha 15(1), wawekezaji pia hupata fursa ya uendeshaji wa biashara chini ya leseni moja pekee iliyotolewa na EPZA, urahisi wa kupata visa kwa wafanyakazi wa kiufundi mara tu wanapoingia nchini, uhuru wa kuhamisha faida.

Mtaalamu wa uchumi aliyefanya utafiti wa uwekezaji wa EPZA mwaka 2015, Moses Kulaba alisema kuna hatari kubwa ya wawekezaji kuhamisha utajiri wa nchi kupitia kuhamisha faida.

“Wakati nafanya utafiti nilibaini kwamba kampuni nyingi zilikuwa na makao makuu yake nchini Mauritius, ambako viwango vyake vya kodi ni vidogo mno na baadhi ya kodi ni sifuri.

“Kwa hiyo wanapohamisha faida kutoka Tanzania, hawakatwi kodi kwa sababu ya vivutio, halafu wakifikisha Mauritius napo hawakatwi kodi, maana yake mwekezaji halipi kodi mara mbili.

“Halafu ile ile faida wanairudisha Tanzania kuongeza mtaji, ambapo haikatwi kodi na wakizalisha, wanaihamisha tena kama faida bila kukatwa kodi,” alisema.

Hata hivyo, Meneja Uhusiano wa EPZA, Panduka Yonazi anapinga vivutio hivyo kutoa njia ya utoroshwaji wa mapato, akisema vinasaidia katika ushindani wa uwekezaji duniani.

“Ukienda Dubai kuna vivutio, ukienda China au hata Kenya kuna vivutio. Hii ni dunia ya ushindani, usipoweka vivutio wenzako wanaweka na wanapata wawekezaji,” anasema.

Akichambua vivutio hivyo, Yonazi anapuuza madai kuwa mwekezaji anaporuhusiwa kuhamisha faida anachochea pia utoroshwaji wa fedha nje ya nchi.

“Ni kama wewe ukipata mshahara tukupangie jinsi ya kutumia? Hiyo iko duniani kote, hata ukienda Dubai, Rwanda, popote pale, wanakuruhusu kuondoka na faida uliyozalisha,” anaeleza.

Kuhusu likizo ya kodi (tax holiday) ya miaka 10, Yonazi anatetea akisema inawawezesha wawekezaji kujipanga tangu kujenga kiwanda hadi kuanza kutengeneza faida.

“Kwa mfano moja ya mahitaji kwa mwekezaji ni kujenga kiwanda kitakachozalisha bidhaa za Dola za Marekani 500,000 (Sh1.4 bilioni) kwa mwaka.

“Sasa aanze ujenzi wa kiwanda, aweke mashine, atoe mafunzo kwa wafanyakazi, unakuta kiwanda kina wafanyakazi 6,000, ndipo aanze uzalishaji na kufanya majaribio ya muazo, unafikiri ndani ya mwaka mmoja atafikisha mauzo ya Sh1.4 bilioni?” anahoji.

Katika hilo, Kulaba alisema wakati wa utafiti wake, alibaini baadhi ya kampuni kutojenga majengo ya kudumu hali iliyokuwa ikitishia uwekezaji huo kuwa wa muda mrefu.

“Mwekezaji anaweza kufanya kazi kwa miaka 10, kisha akaondoka akiwa amevuna faida. Kama kweli tunataka Tanzania ya viwanda, tunapaswa kuwa na mipango ya muda mrefu. Tangu EPZA zimeanzishwa wakati wa Rais Benjamin Mkapa, tungetarajia kuona viwanda vikubwa vilivyosimama,” anasema.

Wakati Kulaba akiyasema hayo, Yonaza anabainisha kuwa, kwa sasa Tanzania kuna wawekezaji zaidi ya 250 waliojenga viwanda maeneo mbalimbali nchini na wameajiri wafanyakazi zaidi ya 70,000 wa kada mbalimbali.

“Wapo wafanyakazi wa kada ya chini, wengine ni wataalamu na wengine wapo kwenye utawala,” alisema.

Hata hivyo, Kulaba alisema alibaini kuwa wafanyakazi wengi ni wa kada ya chini.

“Ajira wanazopewa ni zile ndogo kama kushona na nyingine ambazo sio za utaalamu mkubwa. Kwa hiyo hata suala la kubakisha teknolojia kutoka nje linakuwa gumu, maana wazawa hawahusihwi kwenye utaalamu mkubwa kama wa mitambo,” alisema.

Pia, alisema ajira hizo haziwezeshi Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kukusanya mapato ya kutosha (Paye) kwa kuwa ujira wa wafanyakazi uko chini.

Mwananchi limezungumza na mmoja wafanyakazi wa kiwanda cha Tooku aliyeomba kutotajwa jina lake, akijitambulisha kuwa fundi charahani.

“Mshahara hapa ni Sh150,000, ukikatwa pensheni nabaki na Sh130,000, bado sijalipa kodi na mambo mengine,” anasema.

Uingizaji malighafi zilizotengenezwa

Kuhusu wawekezaji kuingiza malighafi kutoka nje zikiwa zimeshatengenezwa nusu, Kulaba alisema alibaini kuwa baadhi ya viwanda vya nguo viliagiza kwa ajili ya kuja kushonwa kwenye viwanda vya ndani.

“Kwa nini wasitumie pamba inayozalishwa nchini, wazalishe vitambaa hapa? Kwa hiyo utaona wafanyakazi walioko kwenye viwanda hivyo kazi yao ni kukata na kushona tu. Ajira nyingi zinazalishwa kwenye nchi zinazotengeneza malighafi kabla ya kuleta nchini.

“Halafu bidhaa hizo zinakuja kuunganishwa Tanzania na kubandikwa nembo ya “Made in Tanzania”, hali inayowaruhusu kupata misamaha ya kodi,” anasema.

Hata hivyo, Yonazi anafafanua kuwa wawekezaji huwa wanapewa vigezo vya malighafi ya kutumia na masoko wanayoyahudumia.

“Wazalishaji wa nguo wana vigezo walivyopewa na kampuni kubwa, kwa hiyo ni lazima wanunue vitambaa, zipu, vifungo vinavyotakiwa na kampuni hizo.

“Pale wanaleta vitambaa, nguo vinashonwa pale kuanzia mwanzo kabisa,” anasema.

Profesa wa uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anayefanya utafiti kuhusu vivutio vya kodi, Abel Kinyondo anasema vivutio hasa katika maeneo ya uzalishaji kwa mauzo ya nje yaliwekwa kwa lengo zuri, lakini matokeo yake hayajawa mazuri.

Hata hivyo, anasema tofauti na matarajio, maeneo hayo yamekuwa njia ya kukwepa kodi badala ya kuchangia kikamilifu uchumi wa Taifa.

“Ingawa EPZs na SEZs zinavutia wawekezaji kwa motisha mbalimbali, kuna wasiwasi mkubwa kuhusu manufaa yao kwa uchumi wa Tanzania. Ikiwa hazitoi ajira bora, haziimarishi teknolojia ya ndani, na hazichangii ipasavyo kwenye mapato ya kodi, basi kuna haja ya kufanyia marekebisho mfumo wa motisha hizi ili kuhakikisha zinaunga mkono maendeleo ya kweli ya kiuchumi,” anasema.

Chimbuko la EPZA

Kwa mujibu wa taarifa ya mamlaka hiyo iliyopo kwenye tovuti yake, EPZA ilianza rasmi shughuli zake mwaka 2007 kwa kuwa na viwanda vichache vya EPZ vya mtu mmoja mmoja na kisha Serikali ikajenga eneo lake la kwanza la viwanda linalomilikiwa na Serikali katika Mabibo External, Dar es Salaam, ambapo ilivutia uwekezaji wa takriban dola 88 milioni (takribani Sh236.72 bilioni).

Akitoa wasilisho wakati wa kuikaribisha ujumbe kutoka Ubalozi wa Angola uliokuja kujifunza jinsi Tanzania imepiga hatua kupitia miradi yake chini ya EPZA Februari 18, 2025, Mkurugenzi Charles Itembe, anaeleza kuwa mamlaka hiyo imesajili miradi ya viwanda yenye thamani ya zaidi ya Sh8.07 trilioni ambayo ipo katika hatua mbalimbali za maendeleo.

Sheria za uwekezaji

Mbali na wawekezaji kwenye maeneo ya EPZ na SEZ, Tanzania pia inatoa vivutio kwa wawekezaji wengine wakubwa kupitia sheria zake.

Sheria ya Uwekezaji iliyofanyiwa mapitio Juni 2023, kifungu cha 19 (1), inawataka wawekezaji kuwasilisha maombi yao ya kupewa motisha katika Kituo cha Uwekezaji Tanzania, ambacho ndio kitatangaza vyeti, hivyo kwa mujibu wa taratibu zilizoainishwa katika kanuni.

Mbali na sheria hiyo, vivutio kwa wawekezaji pia vinatolewa kupitia Sheria ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (2019), Sheria ya Usimamizi wa Kodi (2022), Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) (2014), Sheria ya Kodi ya Mapato, 2019 na Sheria ya Usimamizi wa Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (2019).

Madhara utoroshwaji wa fedha

Akizungumza katika mkutano wa wadau wa kupambana na utiririshwaji haramu wa fedha jijini Dodoma hivi karibuni, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Saint Augustine (SAUT), Norah Kawiche, anasema kukithiri kwa tatizo hilo kunasababisha kupotea kwa mapato, kutotosheleza kwa bajeti ya Serikali na kuongezeka kwa deni la Serikali.

 “Kupungua kwa bajeti kunaathiri sekta muhimu kama elimu, afya na miundombinu. Katika Deni la Taifa, hadi kufikia Juni 30, 2024 deni la Taifa lilifikia zaidi ya Sh97.35 trilioni, likiwa ni ongezeko la zaidi ya Sh15.1 kutoka zaidi ya Sh82.25 trilioni mwaka 2022/23, sawa na ongezeko la asilimia 18.36,” anasema.

Anashauri kuwepo kwa mabadiliko ya sheria ikiwamo Sheria ya Kuzuia Utakatishaji wa fedha haramu ya 2022, kuboresha Sheria ya Kampuni ya 2022 na Sheria za Kodi na kurekebishwa kwa kanuni ya kuihamisha bei 2018.

Akijibu hoja hizo katika mkutano huo, Mwanasheria kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Charles Mpaka anasema tatizo la mtiririko wa fedha haramu limedhibitiwa Tanzania na ndio maana miradi ya uwekezaji imeongezeka.

“Kwa Tanzania tumeweka mazingira mazuri ambayo yanampa uhakika mwekezaji. Kwa mfano ukiangalia takwimu za uwekezaji kwa miaka mitano, utaona unapanda.

“Mathalani mwaka 2020, TIC ilisajili miradi 207, mwaka 2021 miradi 236, mwaka 2022 miradi 293, mwaka 2023 miradi 526 na mwaka 2024 miradi 901 yenye thamani ya dola 7.75 (zaidi ya Sh2 trilioni), kwa hiyo inaonyesha kuna imani ya wawekezaji kuja kuwekeza Tanzania kwa sababu wana uhakika na sera tulizonazo,” anasema.

Hata hivyo, anasema changamoto hizo zipo kwa sababu zinabadilika kitu.

“Ukiniambia Tanzania kuna upenyo wa mtiririko wa fedha haramu, nitakwambia ndiyo au hapana. Nitakwambia ndio kutokana na faida ambazo ambazo zipo.

“Kwa nini pamoja na sheria na njia nyingi, bado mtiririko bado upo? Jibu ni moja, mbinu na namna ya kutitirisha fedha haramu zinabadilika kila asubuhi. Wewe wakati unafanya maboresho ya sheria wenzako wameshakaa, unajikuta umebaki pale pale,” anasema.

Habari hii imepata ufadhili kutoka Taasisi ya Thomson Reuters Foundation kupitia Wakifu wa vyombo vya habari Afrika Magharibi (MFWA). Maudhui ya makala hii ni ya mwandishi pekee na hayajaidhinishwa wala kuhusishwa na Thomson Reuters Foundation, Thomson Reuters, Reuters, wala mashirika mengine yanayohusiana nayo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *