Utafiti wabaini wananchi vijijini hawali mayai

Morogoro. Ulaji wa mayai na unywaji wa maziwa kwa wananchi wa vijijini unaonekana kuwa mdogo ikilinganishwa na wa mijini.

Hayo yamebainika kutokana na utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kupitia mradi wa Food Land, ambapo imegundulika kuwa wananchi hao kwa kiasi kikubwa wanakosa protini inayotokana na wanyama.

Akitoa matokeo ya utafiti huo, Mratibu wa utafiti ambaye pia ni mtafiti kutoka SUA, Profesa Suzan Nchimbi amesema utafiti huo ulifanyika katika wilaya za Kilombero na Mvomero, hasa katika kijiji cha Kinda, ukitumia njia mbalimbali ikiwemo dodoso.

Profesa Nchimbi amesema kuwa wamebaini wananchi wa vijijini hufuga kuku wa mayai kwa dhumuni la kibiashara, badala ya kula mayai kama sehemu ya lishe, wao huuza mayai ili kupata fedha kwa matumizi mengine.

“Tulipokwenda kwenye eneo la utafiti tulizungumza na wananchi na walitueleza kuwa hawali mayai kama sehemu ya lishe bali wanafuga kuku ili kuwauza wao au mayai waliyotaga ili kupata fedha. Kuhusu unywaji wa maziwa, wananchi wengi hawanywi kwa sababu hawafugi ng’ombe wala mbuzi wa maziwa,” amesema Profesa Nchimbi.

Aidha, ameeleza kuwa utafiti huo pia ulibaini kuwa wananchi wa kijiji cha Kinda wanalima kwa wingi maharage. Kupitia utafiti huo, SUA ilikuja  na aina nne za mbegu za maharage zilizoimarishwa kwa madini ya chuma na zinki.

“Aina hizo za mbegu ni PIC 130, Nuha 629, Nuha 660 na Mashamba, ambazo zote zipo katika hatua mbalimbali za majaribio kwenye taasisi husika ikiwemo TOSCI,” amesema Profesa Nchimbi.

Utafiti huo pia ulijikita katika ufugaji wa samaki, hususan uboreshaji wa chakula chao, pamoja na mbinu bora za kuhifadhi mazao kama matunda, yakiwemo maparachichi.

Awali, mmoja wa washiriki wa utafiti huo, Profesa Dismas Mwoseba amesema utafiti huo ulianza mwaka 2020 na unafanyika katika nchi sita: Morocco, Tunisia, Ethiopia, Kenya, Uganda na Tanzania. Kwa Tanzania, utafiti ulifanyika katika mkoa wa Morogoro (Kilombero na Mvomero) na Dar es Salaam.

Profea Mwoseba amesema kuwa mradi huo unalenga sekta za kilimo, elimu, afya na lishe. Katika upande wa elimu, utafiti ulibaini kuwa vijana wengi wa kijiji cha Kinda hawajui kusoma, hali inayowafanya washindwe kuelewa vipeperushi na majarida yanayohusu lishe, hivyo kushindwa kuzingatia mlo bora.

Kwa upande wao, baadhi ya wananchi wa Wilaya ya Mvomero ambao ni wafugaji wa kuku wanakiri kuwa hawali mayai, badala yake huuza ili kupata fedha za kujikimu.

Mratibu wa mradi wa utafiti wa Food Land unaoshughulika na masuala ya lishe, kilimo, elimu na afya, Suzan Nchimbi akiwasilisha matokeo ya utafiti huo uliofanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero na Kilombero mkoani Morogoro. Picha Hamida Shariff, Mwananchi

Mmoja wa wafugaji wa kuku, Prosper Mkunule, amesema si mayai tu, bali hata mboga na matunda wanayozalisha huuza badala ya kula kwa sababu hawana elimu ya lishe.

“Tunazalisha njegere, karoti na mboga nyingi za majani, lakini kwa kuwa hatuna elimu ya lishe, vyakula hivyo tunauza. Vilivyo sinyaa au kupoteza ubora ndio tunakula. Tunaomba watafiti baada ya kugundua changamoto hii, watufundishe masuala ya lishe ili tubadilike,” anasema Mkunule.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *