
Unguja. Meli ya utafiti wa bahari na samaki, Dk Fridtjof Nansen kutoka Norway, inatarajiwa kuanza utafiti wake nchini.
Utafiti huo unalenga kubaini aina mpya za samaki, hatua ambayo itasaidia Serikali kuelekeza nguvu katika rasilimali hizo na kuongeza tija katika uchumi wa buluu.
Katika utafiti wa mwaka 2023, watafiti waligundua aina 20 za samaki ambazo hazikuwahi kuonekana katika maji ya Tanzania na jumla ya aina za samaki nchini kufikia 540.
Utafiti mpya unaotarajiwa kuanza kesho Alhamisi, Aprili 3, 2025, utashirikisha wataalamu 26 kutoka mataifa 13 kwa muda wa takribani mwezi mmoja. Lengo lake si tu kubaini wingi wa samaki kwa ajili ya mipango ya Serikali, bali pia kusaidia kupanga matumizi endelevu ya bahari na kuwasaidia wavuvi kujua maeneo yenye samaki wengi.
Akizungumza wakati wa kuipokea meli hiyo katika Bandari ya Malindi leo Jumatano Aprili 2, 2025, Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar, Shaaban Ali Othman amesema Serikali imewekeza kwa kiasi kikubwa katika sekta ya bahari, hivyo taarifa zitakazopatikana kupitia utafiti huu zitasaidia kuonyesha mwelekeo mpya wa maendeleo.
“Hii inatusaidia kujua uhalisia wa bahari yetu, nini kilichomo na kutupa mwangaza wa hatua tunazopaswa kuchukua kwa maendeleo ya sekta hii,” amesema Waziri Othman.
Hafla ya kuipokea meli hiyo pia iliambatana na maadhimisho ya miaka 50 ya mpango wa Ecosystem Approach to Fisheries (EAF-Nansen), unaolenga kuhakikisha uvuvi unafanyika kwa njia salama na endelevu.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Tanzania, Dk Edwin Mhede, amesema utafiti huo utatoa mwanga kuhusu uwepo wa viumbe mbalimbali baharini, pamoja na kiwango cha oksijeni na uhai wa viumbe wa baharini, ikiwemo biomass, kipimo muhimu cha wingi na afya ya samaki.
“Takwimu zinaonyesha kuwa mwaka 1982/83, Tanzania ilikuwa na biomass kati ya tani 100,000 hadi 175,000, lakini ilipungua hadi kufikia tani 32,123 mwaka 2018. Hata hivyo, mwaka 2023, kiwango hicho kiliongezeka kwa takribani tani 5,000 kwa mwaka. Tunahitaji kufahamu sababu zilizopelekea mabadiliko haya,” amesema Dk Mhede.
Ameongeza kuwa utafiti huu hautajikita tu katika kupima kiwango cha biomass, bali pia kuelewa sababu zilizopelekea kupungua kwake hapo awali, pamoja na kuchunguza ikiwa mabadiliko ya tabianchi yana mchango wowote katika mwenendo huu.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (Tafiri), Dk Ismael Kimirei amesema utafiti huo utathibitisha takwimu zilizopatikana katika awamu mbili zilizopita na kueleza muundo wa sakafu ya bahari, rasilimali zilizopo, wingi wa samaki na mtawanyiko wao.
“Utafiti huu utafanyika kwa siku 19, kuanzia Machi 3, na utahusisha maji yote makuu kutoka Mtwara hadi Pemba. Watafiti wataangalia wingi wa samaki, mtawanyiko wao, na aina mpya za samaki zilizopo katika bahari yetu,” amesema Dk Kimirei.
Kwa ujumla, utafiti huu unatarajiwa kutoa taarifa muhimu zitakazosaidia Serikali na wadau wa sekta ya uvuvi kufanya maamuzi sahihi kuhusu matumizi endelevu ya rasilimali za bahari, hivyo kuchochea maendeleo ya uchumi wa buluu nchini.
Katika utafiti wa mwaka 2023 kuhusu maji ya Tanzania, ilibainika kuwa kuna aina 540 za samaki.
Hata hivyo, kwa kujumlisha viumbe wengine wa majini kama kaa na majongoo bahari, idadi hiyo ilifikia 850.
“Tunaamini kuwa maji yetu bado yana rasilimali nyingi ambazo zinaweza kuwa na manufaa makubwa kwa taifa letu,” amesema mmoja wa watafiti hao.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi na Maliasili Zanzibar (Zafiri), Zakaria Ali Khamis, amesema matokeo hayo ni muhimu kwa sababu Zanzibar inaweka mkazo kwenye ajenda ya uchumi wa buluu.
Utafiti huo utasaidia kutoa takwimu zitakazosaidia kusimamia kwa ufanisi rasilimali za nchi katika sekta ya uvuvi na uchumi wa buluu.
“Wakati meli hii ilipopita maeneo ya Tumbatu, tuligundua kuwa kuna mazalia mengi ya dagaa, jambo linaloonyesha kuwa Zanzibar ina akiba kubwa ya dagaa ambayo inaweza kuchangia uchumi wa taifa,” amesema Khamis.
Mwakilishi Msaidizi wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), Charles Tulahi, amesema shirika hilo limekuwa likishiriki katika mpango huu unaotekelezwa katika maeneo mbalimbali, huku kwa Tanzania ukihusisha Bahari ya Hindi.
“Meli hii inapofanya utafiti, inachunguza mazingira ya viumbe wa majini, kutathmini uwepo wa uchafuzi wa maji, pamoja na kubaini mabadiliko ya tabianchi yanayoweza kuathiri viumbe hao,” amesema Tulahi.
Ameongeza kuwa FAO inashiriki katika miradi inayolenga kuhakikisha uvuvi unafanyika kwa njia endelevu, huku ikizingatia utunzaji wa mazingira, hususan katika ukanda wa pwani.
Kwa upande wake, Balozi wa Norway nchini Tanzania, Tone Tinnes amesisitiza kuwa nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika mipango yake ya maendeleo kupitia programu mbalimbali.