Usiyoyajua kwenye albamu ya Kendrick Lamar

Marekani. Novemba 22, 2024 msanii wa rap kutokea nchini Marekani Kendrick Lamar  aliwashtukiza mashabiki wake kwa kuachia albamu yake ya sita inayofahamika kama GNX.

Kutokana  na msanii huyo kuwa na ushawishi mkubwa kwenye muziki wa rap kwa miaka ya hivi karibuni alichukua nafasi kwenye mitandao ya kijamii huku mashabiki wakionesha kuipokea albamu hiyo kwa furaha. Lakini kuna mambo ambayo yapo kwenye albumu hiyo kama vile.

Jina la albumu “GNX” pamoja na cover art vimetokana na gari ambalo baba wa msanii huyo aliwahi kulimiliki. 

Baba yake K-dot alikuwa anamiliki gari aina ya Buick Grand Nationa Regal GNX” ya mwaka 1987. Na gari hilo ndio lilitumika kumbeba Kendrick Lamar kutoka hospitali kwenda nyumbani siku aliyozaliwa.

Mwaka 2012 rapa Kendrick Lamar aliliambia jarida la Complex,  “Nilipozaliwa, nilifikishwa nyumbani toka  nikiwa ndani ya gari hilo huku baba yangu akisikiliza nyimbo za Big Daddy Kane.”alisema Kendrick.

Albamu ya GNX imekuja na sura mpya kuibua bifu kati ya rapa Kendrick Lamar na Lil Wayne; mwaka 2024 ni miongoni mwa miaka ambayo K-dot amepata mafanikio makubwa sana kwenye muziki wake. 

Kwanza amefanikiwa kushinda bifu lake na Drake baada ya kuachia ‘Not Like Us’ ngoma ambayo inaonekana kama ngumi nzito iliyomshukia rapa Drake kwenye ulingo wa bifu lao, lakini pia amefanikiwa kuingia kuwania tuzo za Grammy 2025 kwa vipengele 7 kama haitoshi ametajwa kuwa ndio msanii ataekuwa kinara kwenye ‘Half Time Show ya Super Bowl 2025’ lakini pia mtandao wa kusikiliza muziki wa Spotify unamtaja  Kendrick kuwa Msanii Bora wa Hip Hop 2024. 

Baada ya  kuchaguliwa kuwa msanii kinara ambaye atatumbuiza kwenye Half Time Show ya Super Bowl 2025 itakayo fanyika New Orleans katika mji aliozaliwa rapa Lil Wayne, mashabiki wa Wayne hawakupendezwa  walitamani kumuona  Lil Wayne akifanya hivyo kwenye ardhi ya nyumbani ya New Orleans.

Na hapo ndipo shida ikaanzia baada ya wadau na mashabiki wa Kendrick kumkingia kifua rapa wao kuwa anastahili na anakila sifa ya kuwa kinara kwenye Super Bowl 2025 sasa kwenye album mpya ya Kendrick Lamar amempitia Lil Wayne kwa kumchana. 

Hata hivyo, Lil Wayne ameonesha kujibu mapema tu baada ya kusikia hiyo mistari aliyo disiwa huku akijaribu kumuonya Kendrick. 

“Nimefanya nini tena ? nimetulia lakini bado wanataka kunipanda kichwani msichukulie upole wa mtu kuwa ni mdhaifu. Nipumzisheni, hakuna anaehitaji kuharibikiwa hata mimi sitaki, nitawaharibia wanaonisumbua” aliandika Lil Wayne kupitia mtandao wa X zamani kama Twitter

Hata hivyo, wadau mbali mbali wameonesha kuguswa na mjadala huu wa Kendrick  na Wayne wengi wakionesha kuunga mkono kuwa  huu ni wakati wa Kendrick kutambaa zaidi lakini asitumie hiyo kumdharau Lil Wayne maana ni mkongwe na kwa wakati wake alitamba zaidi. 

GNX ni Albamu ya sita ya Kendrick lakini ni albamu ya kwanza tangu atoke kwenye record lebo ya Top Dawg Entertainment ilyoanzishwa mwaka 2004 na Antony “Top Dowg” Tiffith, lebo hii ipo mahususi kwa ajili ya muziki wa hiphop, Kendrick alisainiwa kwenye  mwaka 2005 na kuondoka mwaka 2022 lakini ameendelea kufanya kazi na wasanii wa lebo hiyo.

Mapokezi ya albamu ya GNX yamekuwa makubwa mpaka kufikia kuvunja rekodi yake mwenyewe na kuwa msanii wa kwanza kufanikisha kuingiza nyimbo tano kwenye chart za Apple Muziki huku album hiyo ikikamata nafasi ya kwanza kwenye jukwaa hilo.