Usiyoyajua kuhusu ziara ya Rais Samia Tanga

Dar es Salaam. Februari 23, 2025, Rais Samia Suluhu Hassan alianza ziara ya siku saba mkoani Tanga.

Hiyo ni ziara ya kwanza mkoani Tanga tangu aapishwe kuwa Rais, Machi 19, 2021.

Hata hivyo, mkoa huo ndio uliokuwa wa mwisho kwa Rais Samia kuutembelea akiwa na cheo cha makamu wa Rais, Machi 2021.

Samia akiwa makamu wa Rais, ndipo Rais John Magufuli alipofariki dunia Machi 17, 2021.

Samia akiwa makamu wa Rais alilitangazia Taifa na ulimwengu juu ya kifo hicho akiwa Tanga, kisha akaapishwa kuwa Rais kwa mujibu wa Katiba.

Mwananchi inakuchambulia mambo ya pekee katika ziara hiyo iliyohitimishwa jana Jumamosi, Machi 1, 2025.

Rais Samia Suluhu Hassan amependekeza Shule ya Sekondari ya Wasichana Tanga ipewe jina la Beatrice Shellukindo, aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Kilindi hadi kifo chake Julai 2, 2016.

Akizungumza leo Jumanne, Februari 25, 2025, wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo mkoani Tanga, Rais Samia amesema Shellukindo alikuwa mpambanaji wa haki za wanawake na angefurahia kuona shule hiyo ikijengwa katika eneo lake.

Shellukindo alikuwa ni mmoja wabunge hodari wa kupambania haki za wanawake, lakini pia aliwahi kuwa mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (Eala). Pia Shellukindo aliwahi kuwa Mjumbe wa Halmshauri ya Kuu ya CCM (NEC) kupitia wilaya ya Kilindi.

Umbali wa safari

Katika ziara hiyo, Rais Samia amesafiri umbali wa kilomita 901 kutoka Dar es Salaam hadi Mkoa wa Tanga na wilaya zake.

Safari yake ya Februari 23, 2025 ilikuwa kutoka Dar es Salaam kwenda Tanga kupitia njia ya Bagamoyo yenye umbali wa kilomita 344 kwa mujibu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra).

Katika safari hiyo alisimama Handeni kuzindua jengo la Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, kisha akazungumza na wananchi wa Mkata na kuelekea Ikulu ndogo ya Tanga.

Mbali na safari hiyo kubwa, pia amesafiri katika wilaya zote saba za Mkoa wa Tanga ambazo ni Pangani, Lushoto, Handeni, Korogwe, Kilindi, Makinga, Muheza na Tanga Mjini.

Safari ya pili, ilikuwa kutoka Tanga Mjini hadi Lushoto Mjini yenye umbali wa takriban kilomita 190.

Katika safari hiyo pia, alirudi Korogwe na kulala katika Ikulu ndogo ya wilaya hiyo na kesho yake uelekeo wa safari, ulikuwa Kilindi sawa na umbali wa kilomita 180.

Safari nyingine ni kutoka Tanga Mjini kwenda Muheza (kilomita 35), Mkinga (Kilomita 33) na Handeni (kilomita 119).

Rais Samia Suluhu Hassan akiwa na wanafunzi wakati baada ya kufungua Shule ya Sekondari ya wasichana Tanga iliyopo Mabalanga katika Kijiji cha Michungwani Wilaya ya Kilindi, ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya kikazi mkoani Tanga Februari 25, 2025.

Hata hivyo, kilomita za safari hizo hazijumuishi safari ndogondogo za ndani ya Jiji la Tanga, ikiwamo kwenda Uwanja wa Mkwakwani, Bandari ya Tanga na ulipo mtambo wa uhifadhi mafuta wa Kampuni ya GBP.

Mikutano aliyohutubia

Mkuu huyo wa nchi akiwa mkoani Tanga amehutubia mikutano 13 mikubwa na midogo aliyofanya katika wilaya za mkoa huo.

Mkutano wa kwanza ni wa Mkanda wilayani Handeni, kisha ukafuatiwa na mikutano miwili wilayani Bumbuli na Korogwe.

Kisha alihutubia mikutano katika wilaya za Kilindi na Handeni na kesho yake, akahutubia mikutano ya Pangani na Tanga Mjini.

Mikutano hiyo, ilifuatiwa na ile miwili aliyohutubia Muheza kisha akamalizia Mkinga kumaliza ratiba ya siku ya tano.

Siku ya sita, alihutubia mkutano mkubwa wa kujumuisha yote katika ziara yake, uliofanyika Uwanja wa Mkwakwani Tanga Mjini.

Jumamosi, Machi 1, 2025 ziara yake ilikoma kwa kuhutubia mkutano miwili Tanga Mjini, alipokuwa Bandari ya Tanga na alipoweka jiwe la msingi la ujenzi wa Kituo cha gesi asilia (LPG) cha Kampuni ya GBP, Tanga Mjini.

Rais Samia Suluhu Hassan akiwa na Waziri wa Uchukuzi, Prof Makame Mbarawa katika  Bandari ya Tanga mara baada ya kukagua maboresho ya gati mbili mpya wakati akihitimisha ziara yake ya kikazi mkoani Tanga Machi 1, 2025.

Miradi iliyozinduliwa

Ziara hiyo pia amezindua miradi 13 kwa kuweka mawe ya msingi ya kuanza ujenzi, kuzinduliwa na mingine kukagua mwenendo wa utekelezwaji wake.

Miradi hiyo ni Hospitali ya Wilaya ya Handeni, Jengo la Halmashauri ya Bumbuli na Kuweka jiwe la Msingi la Ujenzi wa Bwawa la Umwagiliaji Mkomazi.

Pia, amezindua Shule ya Sekondari ya Wasichana Tanga, jengo la Halmashauri ya Mji wa Handeni na Kuweka jiwe la msingi la mradi wa Maji wa Miji 28.

Katika ziara hiyo, ameweka jiwe la msingi wa ujenzi wa mradi wa Daraja la Mto Pangani, amezindua boti za uvuvi 20 na boti 50 za kilimo cha mwani.

Pia, ameweka jiwe la msingi la upanuzi wa msikiti mkuu wa Ijumaa jijini Tanga, kazindua mradi wa awamu ya pili ya ugawaji wa mitungi ya gesi na kiwanda cha chokaa na saruji.

Pia, aliweka jiwe la msingi katika mradi wa maji wa Tanga-Horohoro.

Ziara yake ilihitimishwa kwa kutembelea Bandari ya Tanga kisha kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa mtambo wa gesi asilia wa Kampuni ya GBP.

Katika mikutano ya maeneo mbalimbali ya mkoani Tanga, alitoa maagizo  na maelekezo kwa wateule wake.

Agizo la kwanza alilitoa alipokuwa katika Halmashauri ya Bumbuli, alipowataka watumishi wa halmashauri hiyo wasitumie uzuri wa jengo hilo kupandisha mabega.

Alitaka jengo hilo, liwe nyenzo ya huduma bora kwa wananchi.

Agizo lingine alililotoa alipokuwa Kilindi, akimtaka Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Pindi Chana aangalie upya sera na sheria inayohusu fidia kwa wananchi walioharibiwa mazao na wanyamapori.

Alisema kuwa, mapitio hayo, yalenge kuhakikisha fidia anayolipwa mwananchi inamsaidia kutokana na uharibifu aliofanyiwa.

Akiwa Mkinga alimwagiza Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Deogratius Ndejembi aangalie namna mashamba makubwa yaliyopo katika eneo hilo yanatumiwa na wananchi.

Amemtaka akapitie upya mikataba ya ubinafsishwaji wa mashamba hayo ili kuona namna ya wananchi kuyatumia.

Agizo lingine, alilitoa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Msajili wa Hazina kupitia upya mikataba ya ubinafsishwaji mashamba na viwanda ili kuona kama wawekezaji wamekiuka masharti.

Alisema ofisi hizo zishauri namna ya kufanya ili kuhakikisha viwanda na mashamba hayo, yanatumiwa na kuwanufaisha wananchi.

Dhamira ya agizo lake hilo, alisema ni kuirudisha hadhi ya viwanda katika Mkoa wa Tanga.

Maelekezo yake mengine aliyatoa alipokuwa bandarini, alitaka ijengwe barabara ya kulipia itakayopitia Singida kuingiza na kutoa mizigo kutoka Bandari ya Tanga.

Pia, aliiagiza bodi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), kuchukua hatua kwa watumishi wabadhirifu, huku akisisitiza isimamie kukomesha ufisadi.

Akiwa katika mradi wa Kampuni ya GBP, aliiagiza Wizara ya Nishati, kupitia upya sera na sheria ili wasambazaji wa mafuta wa Kanda ya Kaskazini wasilazimike kufuata nishati hiyo Dar es Salaam badala ya Tanga ambako ni jirani kwao.

‘Hadhi ya Tanga’

Kwa jumla, Rais Samia alisema anataka kurejesha heshima na hadhi ya Tanga ile ya zamani ya viwanda. Katika kulifanikisha hilo, alisema tayari Serikali imeanza kuchukua hatua za kupanua viwanda vilivyopo na kujenga vipya ili kutoa fursa za ajira kwa wananchi.

“Kwanza ninatamani kuirudisha Tanga ya viwanda kama ilivyokuwa huko nyuma, hili ndilo tamanio langu kubwa,” alisema.

Alisema tayari kuna hatua zimeshaanza kuchukuliwa kwa baadhi ya viwanda kuanza kufanyiwa upanuzi na vingine vinajengwa upya.

Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza na wafanyakazi wa Bandari ya Tanga mara baada ya kukagua maboresho ya gati mbili mpya wakati akihitimisha ziara yake ya kikazi mkoani Tanga Machi 1, 2025.

Aliahidi kulegeza masharti ya uwekezaji ili kuwavutia wawekezaji wengi zaidi na hatimaye kutengeneza fursa lukuki za ajira kwa vijana wa mkoa huo.

“Hiyo ndio Tanga ninayotamani kuirudisha ili vijana wetu wapate ajira na Tanga kusiwe na watu wanazubaa kwenye vijiwe kunywa kahawa na kupiga majungu hapana,” alisema.