
Dar es Salaam. Katika miaka yake zaidi ya 18 katika muziki, Barnaba amekuwa akisifika kwa utunzi mzuri na uimbaji wenye kushawishi kitu kilichompatia mashabiki wengi na kuwa na nguvu ya kuendelea kufanya kazi yake.
Ni miongoni mwa wasanii wa mwanzo waliotoka chini ya Tanzania House of Talent (THT), huku akishinda tuzo kadhaa za muziki Tanzania (TMA) ikiwemo ile ya Msanii Bora wa Kiume 2012. Huyu ndiye Barnaba.
1. Barnaba alikuwa akienda THT na nguo za shule ili kutafuta njia ya kuonyesha uwezo wake na kutoka kimuziki, wakati huo Mwasiti ndiye aliyekuwa Jaji wa THT na alimpa nafasi na mengine sasa ni historia tu.
Utakumbuka THT wamepita wasanii kama Mwasiti, Linah, Amin, Ruby, Ditto, Ibrah Nation, Recho Kizunguzungu, Jolie, Ally Nipishe, Nandy, Jay Melody n.k.
2. Na wimbo wa Mwasiti, Sio Kisa Pombe (2011) akimshirikisha Quick Rocka uliandikwa na Barnaba ambaye pia amewaandikia wasanii wengine kama Lulu Diva, Ruby, Shilole, Linah, Recho, Vanessa Mdee n.k.
3. Barnaba ameandika nyimbo mbili za Shilole, Malele (2014) na Say My Name (2016), mbili za Vanessa, Chausiku (2011) na Siri (2015), pia ameandika Kizunguzungu (2011) wa Recho, Na Yule (2015) wa Ruby, Milele (2016) wa Lulu Diva n.k.
4. Katika wimbo wa Marlaw, Daima na Milele kuna sauti (back vocal) za wasanii wa THT akiwemo Mwasiti, wakati Marlaw anajiunga THT wasanii aliowakuta ambao walikuja ni Mwasiti, Vumi, Barnaba, Amini na Maunda Zorro.
5. Barnaba ndiye msanii pekee aliyepita THT mwenye albamu nyingi zaidi, ametoa albamu tatu, Gold (2018), Refresh Mind (2020), Love Sounds Different (2022) pamoja na EP moja, Mapenzi Kitabu (2020).
6. Albamu yake ya tatu ilishinda tuzo za TMA 2022 kama Albamu Bora ya Mwaka baada ya kuzibwaga nyingine kali kama ‘The Kid You Know’ ya Marioo, ‘Made For Us’ ya Harmonize, ‘Street Ties’ ya Conboi na ‘Romantic’ ya Kusah.
Hakuwahi kutoa albamu kali kama hii, imeshirikisha majina makubwa kama Diamond Platnumz, Jux, Alikiba, Nandy, Rayvanny, Phina, Jay Melody, Kusah, Young Lunya, Mbosso, Khaligraph Jones, Joel Lwaga, Khadija Kopa, Lady Jaydee n.k.
7. Katika nyimbo zote 19 kutoka katika albamu hiyo iliyosimamiwa na Diamond, Barnaba amefanya kolabo, kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita, kati albamu zaidi ya 40 nilizozishuhudia katika Bongo Fleva, hii ndiyo ya kwanza kufanya kitu kama hicho.
8. Barnaba ni jina ambalo alipewa na wazazi wake, hivyo hakubadili jina alipoingia katika muziki, jina kamili ni Barnabas Elias, wasanii wengine ambao hakubadili majina yao ni Joslin, Vanessa Mdee, Linah, n.k.
9. Baada ya Recho kujiunga pale THT akawa na uhusiano wa siri na Barnaba, penzi lao likawa na faida kwake kwani Barnaba ndiye aliyemwandikia wimbo uliomtoa kimuziki, Kizunguzungu (2011).
10. Miongoni mwa nyimbo kubwa za Barnaba kutengenezwa katika studio yake, High Table Sound, ni ‘Nakutunza’ aliomshirikisha Jose Chameleone wa Uganda, pia wimbo wa kwanza kuachiwa na Mimi Mars ‘Sugar’ ulirekodiwa hapo ila Prodyuza alikuwa ni Deey Classic.
Ikumbukwe wasanii wengine Bongo wenye studio zao ni pamoja na Diamond (Wasafi Records), Dully Sykes (Studio 4.12), Nahreel (The Industry), Nay wa Mitego (Free Nation), Rayvanny (Surprise Music/NLM), Quick Rocka (Switch Music) n.k.