
Dar es Salaam, Akiwa tayari ameleta mapinduzi makubwa katika muziki wa Bongofleva kutokana na uthubutu wake, bado Diamond Platnumz anaendelea kufanya vizuri ikiwa ni miaka 15 tangu ametoka rasmi kimuziki.
Tayari ametoa albamu tatu na EP moja, ameshinda tuzo kubwa kama TMA na MTV EMAs, ameanzisha WCB Wasafi, na ni msanii kinara Tanzania anayeuza zaidi katika majukwaa ya kidijitali. Mfahamu zaidi.
1. Dada yake Diamond, Esma Platnumz ameonekana katika video ya wimbo wa mwimbaji huyo, Kamwambie (2009) ingawa haikupangwa kuwa hivyo, katazame kwa makini mwishoni mwa video hiyo utamuona.
Hiyo ni baada ya Diamond kumkosa mrembo wa kucheza nafasi hiyo ndipo Esma akaamua kumsaidia. Ni video aliyoshuti kwa Director Adam Juma kufuatia kushauriwa hivyo na Dully Sykes.
2. Tangu kumsaini Zuchu ndani ya WCB Wasafi mwaka 2020, Diamond hajafanya kolabo na msanii yeyote wa kike Tanzania na wawili hao tayari wameshirikiana katika nyimbo nne ambazo ni Cheche (2020), Litawachoma (2020), Mtasubiri (2022) na Raha (2024).
3. Kuna wasanii wengi Bongo imekuwa ni mtihani kwao kutengeneza nyimbo nyingine kubwa kama zile walizomshirikisha Diamond ambazo zimekuwa zikipata namba kubwa hasa katika mtandao wa YouTube.
Wasanii hao ni Chege (Waache Waoane), Linex (Salima), Navy Kenzo (Katika), AY (Zigo Remix), Harmonize (Kwangwaru), Jux (Enjoy), Mbosso (Baikoko), Fid Q (Fresh Remix) n.k.
4. Muda mfupi baada ya Rayvanny kujiunga WCB Wasafi, alichangia melodi katika wimbo wa Diamond, Make Me Sing (2016) ambao alishirikiana na AKA wa Afrika Kusini pamoja na Zigo Remix (2016) wake AY ambao Diamond ameshirikishwa.
5. Wimbo wa Diamond, Mawazo (2012) aliutunga kwa ajili ya aliyewahi kuwa mpenzi wake, Jacqueline Wolper, hiyo ni baada ya wawili hao waliokuwa na uhusiano wa siri kugombana. Awali wimbo huo alipoundika alimpa mwimbaji kutokea Zanzibar, Baby J ambaye alikuwa rafiki wa Wolper kipindi hicho, lakini Baby J hakuvutiwa nao ndipo Diamond akaurekodi na ukajumuishwa katika albamu yake ya pili, Lala Salama (2012).
6. Hata hivyo, sio Wolper tu aliyetungiwa wimbo na Diamond, kuna Wema Sepetu, wakiwa ndani ya ndege ndipo Diamond aliandika wimbo, Lala Salama (2012), ni wakati ambao penzi lake na Wema, Miss Tanzania 2006 limepamba moto.
7. Kwa mara ya kwanza Diamond alikutana na Laizer nchini Burundi ambapo msanii huyo alienda katika show, wakiwa studio na staa mwingine wa huko, Loliloo ndipo akapenda uwezo wake na kumkaribisha Wasafi Records ambayo ndio ilikuwa inaanza.
Na wimbo wa Akothee kutoka Kenya, Sweet Love (2016) akimshirikisha Diamond, ndio kazi ya kwanza ya Laizer kuachia chini ya Wasafi Records, huku wimbo wa Rayvanny, Kwetu (2016) ukiwa wa kwanza kumtangaza zaidi.
8. Diamond ndiye msanii aliyeshinda tuzo nyingi za Muziki Tanzania (TMA) kwa muda wote zikiwa ni zaidi ya 22, kwa msimu huu alishinda nne akiwa ndiye msanii pekee aliyeondoka na idadi kubwa ya tuzo.
9. Diamond alimuomba Sallam SK awe Meneja wake rasmi baada ya kufanikisha kukamilika kwa kolabo yake na Davido, My Number Remix (2014) ambayo ndio ilimtangaza kimataifa kwa mara ya kwanza. Hapo awali, Sallam SK alikuwa meneja wa AY, sasa akapewa kazi ya kumleta Davido katika tamasha la Fiesta. Baada ya mkali huyo wa Nigeria kutua nchini ndipo Diamond akamuomba kumuunganisha naye.
10. Baada ya kurekodi, Diamond na Sallam SK walienda Nigeria kwa ajili ya kushuti video na remix hiyo ilipotoka ikafanya vizuri na kumuwezesha Diamond kuwania tuzo za MTV MAMAs kwa mara ya kwanza kama Msanii Bora wa Kiume na Wimbo Bora wa Kushirikiana 2014.