Usiyoyajua kambi ya Mdude Mbeya, zimetimia siku 16 bila kada huyo kupatikana

Mbeya. Kambi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) inayoshinikiza kupatikana kwa kada wake, Mdude Nyagali, inaendelea kujitokeza kwa sura mpya baada ya kuanza kupeana zamu za kulala katika kambi hiyo miongoni mwa wafuasi, huku wakieleza matarajio yao kuhusu hatima ya kiongozi huyo.

Kambi hiyo ilianza Mei 3,2025  siku moja baada ya Mdude kudaiwa kuvamiwa na kupigwa nyumbani kwake, mtaa wa Iwambi jijini Mbeya, na watu waliodai kuwa ni askari polisi, kisha kuondolewa na hajulikani alipo.

Baadhi ya makada wa Chadema walioweka kambi zilipo ofisi za chama hicho Kanda ya Nyasa jijini Mbeya wakiwa wamelala.

Tangu kupotea kwa mwanaharakati huyo, wafuasi na viongozi wa Chadema kutoka maeneo mbalimbali wamekuwa wakifanya msako sehemu tofauti wakimtafuta Mdude, lakini bila mafanikio. Hatimaye, waliazimia kuanzisha kambi katika ofisi za chama hicho Kanda ya Nyasa jijini Mbeya.

Pia, tayari zimeshachukuliwa hatua kadhaa na wafuasi hao, ikiwa ni pamoja na kufanya mazungumzo na mamlaka za Serikali, akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk Juma Homera ambaye alitoa ahadi ya kumpa zawadi ya Sh5 milioni mtu atakayefanikisha kupatikana kwa Mdude.

Ahadi ya zawadi ya fedha pia imetolewa na Chadema ambao wametoa Sh10 milioni kwa atakayefanikisha kupatikana kwa kada wao huyo. Jeshi la Polisi mkoani humo nao wametangaza kuendelea na uchunguzi huku wakiomba mwananchi mwenye taarifa kuhudu kada huyo kutoa ushirikiano.

Baadhi ya makada wa Chadema walioweka kambi zilipo ofisi za chama hicho Kanda ya Nyasa jijini Mbeya wakiendelea na shughuli za kuandaa chakula

Mwananchi imefika mara kadhaa ofisi za chama hicho na kushuhudia kundi la wafuasi wa chama hicho wakiwa wamevalia sare za chama wakiendelea na vikao tofauti, huku ajenda ikiwa ni kumpata Mdude.

Hata hivyo, katika hali isiyo ya kawaida, kambi hiyo imeonekana si ya kichovu kwa kuwa asubuhi huamka na ubize bila kujali jinsia, ambao kila mmoja hufanya shughuli za kuandaa kifungua kinywa (chai) huku vitafunwa vikibadilishwa kila siku.

Kama haitoshi gazeti hili limeshuhudia kila mara wafuasi wanaofika kambini hapo huja na vifurushi vya vyakula vikiwamo mchele, mahindi, viazi vitamu na mbatata na mabegi yenye nguo.

Kwa upande wa chakula, hali imeonekana si ya kitoto kwa kuwa mlo hubadilishwa kulingana na mapenzi yao, huku kitoweo kikiwa ni nyama na mazingira hayo yanaonekana kukubalika kwa kila mmoja.

Pia, suala la kulala limeonekana si tatizo kwani gazeti hili limeshuhudia baadhi ya makada wa jinsia ya kike wakiwa chumbani wamelala, huku wengine wakiwa wamejipumzisha sebuleni na kwenye varanda za ofisi hiyo.

Mazingira yanayozunguka jengo hilo yamesafishwa na nyasi zilizokuwapo awali zimelimwa na kila mmoja akifurahia maisha ya sehemu hiyo.

Ofisi hiyo ina zaidi ya vyumba vitatu vyenye nafasi kubwa ambayo kwa makadirio ukijumlisha na varanda wanaishi watu wasiopungua 300 ambao huingia na kutoka kulingana na zamu za kulala walizopeana. Nyumba hiyo pia ina vyoo vya ndani na nje vinavyotumiwa na makada hao.

Wenye familia na majukumu

Katibu wa Chama hicho Kanda ya Nyasa, Grace Shio anasema kwa sasa wameanzisha utaratibu mpya kwa kupeana zamu kwa ambao wanabanwa na majukumu huondoka asubuhi na kurudi jioni, kupokezana na wanaoshinda kambini hapo.

Anasema wapo wenye familia haswa watoto wanaoenda shule ambapo wameamua kuweka mazingira hayo, ili kila mmoja apate nafasi ya kushiriki kupigania haki ya Mdude kupatikana.

“Tunafahamu kuna wenye kazi zao serikalini, wafanyabiashara, wajasiriamali na wenye familia tumeamua kuweka zamu ili kutoa nafasi kila mmoja apate nafasi ya kushiriki azimio hili,” anasema Grace.

Watenga dau la Sh10 milioni

Katibu wa chama hicho mkoani humo, Hamad Mbeyale anasema kutokana na muda unavyozidi kwenda bila mafanikio, wameamua kuweka dau la Sh10 milioni kama bonasi kwa yeyote atakayefichua alipo kada wao.

Anasema baada ya msako katika maeneo mbalimbali bila mafanikio, kwa sasa wanaendelea na kambi isiyo na kikomo, lakini wakipambana kuzilazimisha mamlaka kuweka wazi alipo mwenzao ili aendelee na shughuli zake za kulijenga Taifa.

Kuhusu wanaodaiwa kuathirika na kinachodhaniwa kuwa ni sumu iliyomwagwa kambini hapo, Mbeyale anasema wenye tatizo wanashauriwa kufika hospitali, lakini kwa wasio na uwezo chama hicho kinawakaribisha ili kuchukua hatua za haraka na dharura.

“Kwa walioathirika na sumu waende hospitali, lakini kama hawana pesa sisi chama tutawapeleka sehemu yetu kwa matibabu, tumeongeza dau hadi la Sh10 milioni kwa atakayefanikisha kumpata mwenzetu” anadai Mbeyale.

Kuhusu hatima ya kambi

Katibu wa chama hicho Kanda ya Nyasa, Grace anasema pamoja na majaribu wanayopitia ikiwamo kuvamiwa na kumwagiwa dawa inayodhaniwa sumu kambini hapo, lakini hawatarajii kuivunja hadi watakapompata mpendwa wao.

Anasema haiwezekani wakavunja matanga kabla ya kupatikana kwa kada mwenzao, akiwa hai au amekufa kwani hata familia yake imegoma kusafisha nyumba kutokana na damu zilizomwagika wakisubiri hatima yake.

“Kambi hii ni endelevu, tutaondokaje Mdude hajapatikana? Hata nyumbani kwao familia inataabika na zile damu hazijasafishwa hadi apatikane, wanaojaribu kutudhoofisha hatuondoki hapa” anasema Grace.

Anadai kuwa wana matarajio kwamba Mdude yuko hai na waliomshikilia ni Jeshi la Polisi akieleza kuwa wanaendelea kushinikiza mamlaka kueleza alipo kada huyo ambaye ni mtetezi wa haki za binadamu.

Grace anadai kuwa baada ya kutokea sintofahamu ya kundi la watu wasiojulikana kuvamia kambi na kumwaga sumu, tayari wamejiimarisha kiulinzi na usalama katika eneo la ofisi hiyo.

Amebainisha kuwa hata hivyo pamoja na tukio hilo, vijana wao walikuwa makini kupambana na kundi hilo la kihalifu.

“Muda wote tunao vijana wanaolinda usalama, hata wakati wa tukio hilo usiku wa manane, ulinzi ulikuwapo ndio maana waliishia nje bila kuingia ndani na ulinzi wetu tumeendelea kuuimarisha kwa kuwa mamlaka husika hazina habari na sisi.

“Jeshi la Zimamoto na Uokoaji walifika wakatusaidia kupuliza maji kuondoa presha na harufu kali iliyokuwa imetanda, tunasubiri majibu ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwani watendaji wa ofisi yake walishuhudia dawa hizo” anadai katibu huyo.

Anabainisha kuwa hadi sasa wanafurahishwa na kasi ya wananchi na wafuasi, namna wanavyofika kambini hapo wakitoka sehemu tofauti ndani na nje ya Jiji la Mbeya, akieleza kuwa baadhi yao wanatoa taarifa za matumaini kupatikana kwa Mdude.

Grace anadai kuwa mbali na wananchi wasamaria wema, lakini pia wamo askari Polisi wanaowapenyezea za chini kuwa kada huyo yupo salama na wanaendelea kukusanya taarifa hizo kisha kufikisha kwa mamlaka husika kwa hatua zaidi.

Wafuasi wafunguka

Mmoja wa wanachama wa chama hicho, Magreth Mwanguku (80) anasema bado hofu ni kubwa kambini hapo akieleza kuwa hawaelewi hatima ya maisha ya Mdude, akibainisha kuwa hawapo eneo hilo kwa furaha bali kupigania uhai wa mwenzao.

“Tunaanza kuishi kwa hofu, kazi ya Polisi hatujui ni nini, hatma ya Mdude bado hatuelewi, watu tupo hapa si kwa ajili ya sherehe, tunaomba kujua hatima ya mwenzetu,”anasema Magreth mkazi wa Kata ya Ruanda jijini Mbeya.

Kauli ya Zimamoto na Polisi

Akizungumzia kwa njia ya simu Kamanda wa Zimamoto Mkoa wa Mbeya, Malumbo Ngata amethibitisha kuwapo tukio la umwagaji dawa eneo la kambi ya Chadema, akieleza kuwa baada ya kupata taarifa walifika eneo hilo na kutoa huduma.

Kuhusu kinachodaiwa kuwa sumu, Kamanda Ngata amesema hana uhakika kwa kuwa majibu hayo ni kwa Mkemia Mkuu wa Serikali, akifafanua kuwa wao walifika na kupuliza maji kuondoa presha ya harufu kali iliyokuwapo.

“Kujua kama ilikuwa au haikuwa sumu Mkemia Mkuu ndiye anaweza kuzungumza, lakini ilionekana kuwa na harufu kali na ya kukereketa wakaomba tupulize maji kuondoa presha ya harufu.

“Sisi tumefanya sehemu ya wajibu wetu kusafisha, lakini tumeacha ushauri iwapo watapata madhara yoyote wawasiliane na Mamlaka ofisi ya Mkemia Mkuu ambao walifika kuchukua sampuli kujua kama ni sumu au ni kitu gani” amesema Ngata.

Mei 10, Jeshi la Polisi mkoani Mbeya lilieleza kuwa linaendelea na uchunguzi wa tukio la kuvamiwa na kupigwa kwa Mdude Nyagali.

Aidha, Jeshi hilo lilitoa onyo kali kwa baadhi ya watu wanaotoa matamko ya kiholela na kuwataja askari Polisi kuhusika na tukio hilo bila kuwa na ushahidi wowote, likisisitiza kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wanaoeneza tuhuma zisizothibitishwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *