Kila mwaka ifikapo Februari 14, duniani kote huadhimishwa siku ya wapendanao ‘Valentine Day’.
Siku hii hugeuka kuwa shubiri kwa baadhi ya wapendanao kutokana na vimbwanga vinavyotokea, vikitajwa kusababishwa na ukosefu wa uaminifu katika mahusiano.
Ikiwa imebaki siku moja kusherehekea siku hiyo, ambayo wapendanao hupeana zawadi, hupata chakula cha pamoja na kwenda matembezi, wengine huangukia kwenye majonzi.
Mwanasaikolojia Modesta Kimonga amesema mihemko na matarajio ndiyo adui wa siku hiyo.

“Watu wanakuwa na matarajio makubwa ambayo yanatokea tofauti na wanavyotaka. Pia kujilinganisha—mtu anaona rafiki yake anavyofanyiwa maandalizi na mpenzi wake, naye anataka kujilinganisha, lakini anajikuta yupo tofauti na matamanio yake. Hiyo inafanya mahusiano mengi yavunjike.
“Wengine wanakuwa na mihemko, mtu anataka kufanya kitu kikubwa ambacho kipo nje ya uwezo wake. Ila kwa sababu ameona kwenye TV na mitandao ya kijamii kuna kampeni za Valentine, inampa matamanio. Mwisho wa siku, vile vitu vyote alivyokuwa anategemea, anakuta ni vya ndotoni tu,” amesema.
Amesema ni vyema kuchukulia kila kitu katika hali ya kawaida bila kupelekeshwa na matukio, kwani Valentine ni siku ya kawaida kama nyingine.
Hata hivyo, Mwananchi imefanya mahojiano na baadhi ya waathirika wa siku ya Valentine na kueleza mikasa waliokutana nayo katika siku hiyo.
“Mahusiano yangu yalivunjika kwa ajili ya Valentine. Nakumbuka mwaka jana, 2024, niliandaa keki nikiamini mpenzi wangu atakuja tukate na tusherehekee pamoja. Lakini pia nilitarajia na yeye ataniletea zawadi. Ajabu, kila nilipokuwa nikimpigia usiku ule, hakupokea. Nilikaa kusubiri hadi siku ilipinduka.

“Kesho yake nilijaribu kumtafuta, lakini hakupokea simu wala kujibu meseji. Niliumia sana. Kumbe siku hiyo ya Valentine, ambayo mimi nilimuandalia vitu, yeye alikuwa anamvalisha pete mwanamke mwingine,” amesema Mariam Mwita, mkazi wa Sinza.
Naye Jaden John, mkazi wa Tabata, amesema kila ifikapo siku hiyo hujikuta kwenye kumbukumbu mbaya, kwani siku kama hiyo ndiyo ilikuwa mwisho wa uhai wa penzi lake.
“Siku mbili kabla ya Valentine mwaka 2024, nilikuwa mimi, mshikaji wangu na mpenzi wangu. Nakumbuka nilimuahidi mwanamke wangu kuwa Valentine nitampelekea zawadi. Nilivyomwambia hivyo, yule mwanamke akamtania mshikaji wangu kwa kumuuliza na yeye atamnunulia nini? Jamaa akamjibu asijali, ataiona siku ikifika. Mimi nilidhani wanataniana.
“Siku ilipofika, mshikaji wangu alipeleka zawadi kwa yule mwanamke—yalikuwa maua, chocolate na perfume. Nakumbuka mimi nilimnunulia zawadi ya mdoli nikapeleka.
“Aisee, siwezi kusahau! Yule mwanamke alinitolea maneno machafu. Alisema hadhi yake siyo mdoli. Alionyesha kuifurahia zaidi zawadi ya jamaa yangu. Ilileta shida. Hauwezi kuamini ule mtafaruku ulipelekea mwanamke akaniacha mazima,” amesema Jaden John.
Mwananchi haikuishia hapo. Ikazungumza na Tabu Suleiman, mkazi wa Manzese, ambaye kwa upande wake amesema Valentine ya 2023 ndiyo ilikuwa mwisho wa furaha kati yake na baba wa mtoto wake.
“Niliachana na baba wa watoto wangu siku hiyo. Ni siku ambayo aliaga anasafiri kikazi kwenda Nachingwea, lakini haikuwa kweli. Alikuwa na binti wa chuo. Kama Mungu tu, nilimpigia simu usiku, akapokea yule binti na kusema mpenzi wake amelala.
“Nilisikia kuzimia, lakini sikuweza. Yule binti alijiamini, alinipa majibu mabaya na kuniambia yeye ni msomi wa chuo, mimi nisiye na elimu niendelee kukaa nyumbani kulea watoto,” amesema na kuongeza kuwa baada ya hapo hakuwa na imani tena na baba wa mtoto wake, ambaye wamezaa watoto wawili.
Licha ya kuwa siku hiyo inapewa umuhimu na baadhi ya watu, Erick Sebastian, mkazi wa Mwenge, amesema kabla ya kuingia kwenye mahusiano humpa masharti mwenza wake.
“Mimi nikiingia kwenye mahusiano huwa namwambia mtu ‘no Valentine, no birthday’, yaani sifanyi chochote kwa sababu sitaki kuzifanya hizo siku zionekane za muhimu sana.
“Naona siku hii inazalisha chuki. Kama hauna cha kumpa mwenzako, hakuelewi. Sasa, je, kuna ulazima gani wa kupeana zawadi? Pia naona kama imeegemea sehemu moja. Wanawake ndiyo wanataka kupewa,” amesema Erick.
Mbali na maswahibu yote hayo, wapo baadhi ya watu ambao huitumia siku hiyo kuimarisha mahusiano yao na wengine huiadhimisha kwa njia ya kuabudu.