DABI ya Kariakoo, mechi kati ya Yanga na Simba ni tukio lenye umaarufu mkubwa siyo tu kwa wapenzi wa soka, bali pia wajasiriamali na wafanyabiashara kutoka sehemu mbalimbali.
Jumamosi hii soka litasimama kama biashara inayotoa fursa katika maeneo mengi kuanzia uuzaji wa bidhaa hadi huduma zinazohusiana na tukio.
Mechi hiyo siyo tu ni kivumbi cha ushindani wa soka, bali ni jukwaa kwa wafanyabiashara kuonyesha ubunifu na kujipatia faida.
Hapa tutaangazia fursa za kibiashara zinazolika katika Dabi ya Kariakoo ambazo zimekuwa na mchango katika uchumi wa soka.

1. BIASHARA YA VITU VYA MASHABIKI (Merchandise)
Moja ya fursa kubwa zinazojitokeza wakati wa Dabi ya Kariakoo ni uuzaji wa bidhaa za timu kama vile jezi, kofia, bendera na vifaa vingine vya mashabiki. Bidhaa hizo ni muhimu kwa mashabiki wa timu husika, kwani wengi hupenda kuvaa na kubeba alama za timu zao ili kuonyesha upendo na mshikamano. Hii ni biashara inayokua kwa kasi wakati wa mechi kubwa kama hiyo ambapo mashabiki hujitokeza kwa wingi na kuhitaji vifaa vya ushabiki.
Wajasiriamali wanaweza kuweka vibanda karibu na uwanja wa mchezo – katika maeneo yenye mikusanyiko ya watu au katika miji mikubwa kama Dar es Salaam. Kuwa na bidhaa zinazohusiana na timu hizo ni fursa ya kibiashara inayoweza kuleta faida. Wafanyabiashara pia wanaweza kutangaza bidhaa kupitia mitandao ya kijamii ili kuwafikia mashabiki wengi zaidi wanaotafuta vifaa vya ushabiki mtandaoni.

2. CHAKULA NA VINYWAJI
Wakati wa Dabi ya Kariakoo idadi ya watu wanaokusanyika kwenye viwanja au maeneo ya mikusanyiko ni kubwa na inatoa fursa kwa wajasiriamali katika sekta ya huduma za chakula na vinywaji. Wafanyabiashara wanaweza kuuza vyakula vya mtaani kama vile viazi, maandazi, samaki, chipsi, na vinywaji baridi na vinywaji vya joto kama chai, kahawa, na vinywaji vya matunda. Hizi ni bidhaa zinazohitajika sana kwa mashabiki ambao hutumia muda mwingi uwanjani au kwenye maeneo ya mikusanyiko.
Wajasiriamali wanaweza kufungua vibanda vya chakula karibu na viwanja vya michezo au maeneo maarufu ya jiji, na hii itawapa fursa ya kuuza bidhaa zao kwa mashabiki na wapenzi wa soka. Pia, katika mechi ya dab hiyo mashabiki wengi hujitokeza, na hivyo, wafanyabiashara wa chakula na vinywaji wanaweza kupata wateja wengi. Ni muhimu kwa wafanyabiashara kuzingatia ubora wa bidhaa na kuhakikisha wanatoa huduma bora ili kujenga uaminifu na kurudiwa na wateja kwa matukio mengine ya soka.

3. HUDUMA ZA USAFIRI
Usafiri ni moja ya sekta zinazozalisha fursa kubwa wakati wa dabi. Idadi kubwa ya mashabiki hufika uwanjani kwa kutumia usafiri wa umma, magari ya teksi, bajaji, na mabasi. Hii inatoa fursa kwa wajasiriamali kuanzisha huduma za usafiri kwa mashabiki wanaoenda kwenye mechi au mikusanyiko ya matukio yanayohusiana na dabi ya Kariakoo.
Wafanyabiashara wanaweza kuanzisha huduma za teksi za pamoja, bajaji au mabasi ya kisasa, ambayo yatakuwa na safari maalumu kuelekea viwanja vya michezo au maeneo ya matukio. Hizo ni huduma zinazohitajika kwa mashabiki wanaotaka kufika kwa urahisi kwenye mechi au mikusanyiko ya soka.

4. HUDUMA ZA USALAMA NA ULINZI
Katika Kariakoo Dabi, ambapo idadi ya mashabiki ni kubwa, huduma za usalama na ulinzi ni muhimu sana. Wafanyabiashara wanaweza kuanzisha biashara zinazohusiana na huduma za usalama, kama vile huduma za walinzi, vifaa vya usalama kama kamera za CCTV, na huduma za ulinzi binafsi.
Mashabiki, wachezaji, na waandaaji wa mechi wanahitaji kuhakikisha kuwa usalama wa matukio haya unazingatiwa vyema. Wafanyabiashara wanaoingia katika sekta hii wanahitaji kutoa huduma za ubora wa juu ili kuwapa wateja wao amani ya akili. Biashara za usalama na ulinzi zinaweza kuwa na faida kubwa kutokana na hitaji la huduma hizi wakati wa matukio kama haya yanayohusisha mikusanyiko ya watu wengi.

5. HOTELI NA MALAZI
Dabi ya Kariakoo hutoa fursa nzuri kwa wajasiriamali wa hoteli na malazi, kwani mashabiki wengi kutoka mikoa mingine wanahitaji maeneo ya kula na malazi. Hoteli na nyumba za wageni zinazozunguka maeneo ya viwanja vya michezo au maeneo maarufu ya jiji, kama Kariakoo huwa na wateja wengi wanaokuja kushuhudia mechi ya kihistoria.
Wajasiriamali wanaweza kujenga au kuboresha hoteli zao ili kutoa huduma bora za malazi kwa mashabiki wa soka na wageni wanaokuja kwa ajili ya Kariakoo Dabi. Huduma bora za malazi, chakula, na vinywaji ni muhimu ili kuwavutia wateja na kuwa na sifa nzuri kwa matukio yajayo.
WASIKIE WENYEWE
Mfanyabiashara wa jezi Kariakoo, Dar es ws Salaam, Abdul Mfaume anasema: “Kila siku ya mechi kubwa kama hii biashara ya jezi inashamiri. Mashabiki wanakuja kununua jezi mpya ili kuonyesha mapenzi kwa timu zao. Wengine wananunua kwa ajili ya watoto na kuna wale wanaonunua kwa ajili ya zawadi. Tangu Jumatatu mauzo yangu yameongezeka mara tatu kuliko siku za kawaida. Kariakoo Dabi ni sherehe kubwa, na sisi wafanyabiashara tunafaidika sana.”
Kwa upande wake, Mama Janeth ambaye ni muuzaji wa vyakula mtaani, anasema: “Mashabiki wa mpira wanapenda kula. Napika chipsi mayai, mishikaki, na vyakula vingine vya haraka. Siku ya mechi nina uhakika wa kuuza mara mbili hadi tatu ya kawaida. Muda mwingine hata kabla ya mechi kuanza, chakula changu kinakuwa kimekwisha. Mechi ya Simba na Yanga inanisaidia sana kuongeza kipato.”
Naye Joseph Mrope ambaye ni dereva wa Bodaboda anasema: “Mechi ya watani wa jadi ni siku yangu ya mavuno. Mashabiki wanatoka maeneo tofauti na wanahitaji usafiri wa haraka kwenda uwanjani au kurudi makwao au sehemu walizofikia baada ya mechi.”