Usiku wa Ulaya kuondoka na wanne leo

Leo moto utawaka kwenye viwanja vinne tofauti katika hatua ya mtoano wa Ligi ya Mabingwa Ulaya huku timu nne kati ya nane zitakazocheza zitayaaga mashindano hayo wakati nyingine nne zitabaki.

Michuano hii mikubwa Barani Ulaya inayofuatiliwa zaidi kwa sasa na msimu huu imekuja kivingine baada ya kubadilisha mfumo kutoka kupangwa timu kwenye makundi na sasa timu zinacheza kwa mfumo wa Ligi.

Katika mfumo huu mpya kila timu ilicheza mechi nane, nne nyumbani na nne ugenini huku zile zilizomaliza nafasi ya kwanza hadi ya nane zilifuzu moja kwa mojahatua ya 16 bora.

Timu zilizomaliza nafasi ya tisa mpaka 24 zitacheza hatua ya mtoano ili kutafuta timu nane zitakazoungana na zile nyingine zilizomaliza nafasi nane za juu katika kucheza hatua ya 16 bora.

AC Milan vs Feyenoord

AC Milan iliyomaliza nafasi ya 13 leo itakuwa kwenye Uwanja wa San Siro kukabiliana na Feyenoord katika mchezo wa pili wa mtoano huku AC Milan ikiingia kwenye mchezo huu ikiwa nyuma kwa bao moja ililofungwa ugenini kwenye Uwanja wa Feijenoord, Rotterdam, Uholanzi.

Bayern Munich vs Celtic

Bayern iliyotoka kupata ushindi wa mabao 2-1 ugenini, leo itaivaa Celtic katika mechi ya marudiano itakayochezwa kwenye Uwanja wa Alianz Arena huku Celtic ikiwa na nafasi ya kupindua meza kwani Bayern imekuwa na safu duni ya ulinzi ambayo imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara 13.

Mbali na kuruhusu mabao 13 katika michuano ya UEFA, vijana wa Vincent Kompany siyo wanyonge katika kufumania nyavu kwani mpaka sasa wamefunga mabao 22 tu.

Kwa upande wa Celtic, yenyewe imefunga mabao 13 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 14 ikiwa imeruhusu idadi kubwa ya mabao ya kufungwa kuliko iliyofunga jambo linaloipa faida safu ya ushambuliaji ya Bayern ikiongozwa na Harry Kane.

Atalanta vs Club Brugge

Atalanta yenye nyota kama Ademora Lookman, Mateo Retegui na Charles De Ketelaere ilijikuta ikikubali kipigo cha mabao 2-1 ugenini huku bao la ushindi la Club Brugge likifungwa katika dakika za mwisho na Gustaf Nilsson kwa mkwaju wa penati baada ya kuchezewa vibaya na beki wa Atalanta, Stefan Posch.

Mechi ya leo itakuwa ya aina yake pale kwenye Uwanja wa Gewiss ambapo Atalanta itakuwa inapambana kupindua meza ili kufuzu katika hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Benfica vs Monaco

Monaco wataingia kama watumwa kwenye Uwanja wa Sport Lisboa Benfica baada ya kupoteza bao 1-0 kwenye mchezo wa kwanza ilipokuwa nyumbani.

Benfica iliyomaliza nafasi ya 16 mbele ya Monaco iliyomaliza nafasi ya 17 imefunga jumla ya mabao 17 na kuruhusu 12, wakati Monaco imefunga mabao 13 na kuruhusu 13.

Leo timu nne zitafuzu kwenda kuungana na zile zilizomalizia nafasi nane za juu huku timu nyingine nane zikisubiliwa kucheza hapo kesho ambapo nne nyingine zitafuzu ili kukamilisha idadi ya timu 16 zitakazochuana katka hatua nyingine ya mtoano.

Timu nane zilizofuzu hatua ya 16 bora ni Liverpool, Barcelona, Arsenal, Inter Milan, Atletico Madrid, Bayern Leverkusen, Lille na Aston Villa.

Michezo ya kesho UEFA

Real Madrid vs Manchester City

Borussia Dortmund vs Sporting CP

PSV Eindhoven vs Juventus

Paris Saint-Germain vs Brest.