Dar es Salaam. Aman Nzala ndilo jina lake ingawa wengi wanamfahamu kama Anko Nzala. Mwonekano wake unaweza kusema ni kati ya vitu vilivyompa umaarufu huku wengi wakijiuliza umri wake.

Akizungumza na Mwananchi Nzala anasema shauku yake ya kufanya vichekesho aliipata kutoka kwa wachekeshaji kama marehemu Mzee Majuto na Senga.
“Mimi nina miaka 22, lakini mwaka huu Novemba nitatimiza 23. Ukweli ni kwamba sanaa ya vichekesho imenipatia mafanikio makubwa sana nakumbuka nilikuja Dar sina kitu lakini kwa sasa kuna vitu nimevipata hata kujulikana. Namshukuru Mungu kwa hilo amenibariki,” anasema shabiki huyo kindakindaki wa Simba.
Anasema licha ya kuwa na mwonekano kama mtoto lakini hiyo si changamoto kwake katika kazi anazofanya.
“Changamoto kutokana na mwonekano wangu hakuna kwa sababu watu wamenizoea. Nafurahi nacheka na watu, makosa ambayo yapo ni makosa ya kawaida ya kibinadamu yanayomtokea kila mtu,” anasema.

Kutokana na maswali ya wengi kwenye mitandao ya kijamii kuhusiana na uhusiano wake, baada ya kusambaa kwa video akiwa na D Voice ikimuonesha akikimbia wanawake hadi kupelekea wengi kudai mchekeshaji huyo anaogopa wanawake, Nzala anasema bado hajaoa lakini mpenzi anaye.
“Siogopi wanawake lakini ile clip ambayo nakimbia msichana nilikuwa kwenye ‘mood’ ambayo walikuwa kama wamenisusia. Sikupata ujasiri wa kuweza kuimudu nilishindwa kuvumilia. D Voice alinitafuta akaomba tufanye kazi tukalezana mambo ya bajeti tukafanya kazi,” anasema
Utakumbuka Nzala ameonekana kwenye video ya wimbo wa D Voice ‘Tisheti Yangu’, uliotoka miezi mitatu iliyopita huku kwenye mtandao wa YouTube ukiwa umetazamwa zaidi ya mara laki nne.
Hata hivyo, licha ya mchekeshaji huyo kutumia picha mbalimbali za Mohammed Dewji kama sehemu ya maudhui yake na kupelekea baadhi ya watu kudhani wawili hao wana ukaribu. Nzala anafunguka kuwa hajawahi kuonana na tajiri huyo ana kwa ana.

“Sijawahi kukutana na Mo lakini ni mtu ambaye hana mambo mengi amenyooka, na amewekeza kwenye timu yetu tunafurahi,”anasema.
Ikumbukwe Mo aliwahi kuchapisha video ya Nzala kwenye ukurasa wake wa Instagram na hapo ndipo mchekeshaji huyo alianza kutumia kama maudhui kwake.
Licha ya hayo anasema kabla hajafahamika kwa ukubwa, alikumbana na changamoto zilitokata kumkatisha tamaa.
“Kabla sijatoka nilikuwa nafanya clip zangu haziendi na komenti za watu zilikuwa mbaya. Zilikuwa zinanikatisha tamaa lakini kwa sasa Mungu anasaidia nawashukuru mashabiki wananisapoti nawapenda sana,

“Kitu ambacho natamani mashabiki wafahamu ni kwamba nawapenda na ninawakubali bila wao mimi si kitu nisipoposti wananipigia simu, napenda kuwafurahisha watu ili kuondoa mawazo,”anasema.
Sababu ya kujiita Anko Nzala
Linapotajwa jina Anko wengi hupata tafsiri ya mtu mzima (mkubwa kiumri), lakini hii ni tofauti kwa Nzala ambaye licha ya mwonekano wake kuwa mdogo lakini ameamua kujiitua Anko Nzala.
“Anko ni heshima jina nilikubali kujiita hivyo. Nilipenda kujiita hivyo tangu nikiwa shuleni ni jina ambalo nilikuwa nalikubali kwamba siku yoyote nitakapofungua mitandao ya kijamii nitajiita hivyo na hadi sasa najiita,”anasema.