
Dar es Salaam. Wengi tunajua kuwa kitunguu saumu ni mojawapo ya viungo ambavyo mara nyingi hutumika kuongeza ladha na harufu nzuri katika chakula, lakini hatujui kwa undani faida zilizopo katika kitunguu hicho.
Kama ulikuwa hujui, jifunze sasa. Kitunguu saumu husaidia kuzuia maambukizi yatokanayo na bakteria, baadhi ya virusi na fangasi, hasa katika utumbo, mapafu na sehemu za ukeni.
Mtaalamu wa masuala ya lishe kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC), Elizabeth Lyimo anasema vipo vitunguu saumu vya rangi nyeupe, zambarau na pinki na kwamba vitunguu hivyo vyote vina ubora sawa.
Lyimo anasema mbali na faida hizo, kitunguu saumu pia husaidia katika uyeyushwaji wa chakula na kuzuia kuharisha.
Pia huzuia maambukizi yatokanayo na fangasi kwenye kinywa kutokana na viambata vinavyopatikana kwenye vitunguu saumu ambavyo ni; Allicin, Vitamini C, Vitamin B6 na Manganese.
Unaweza kuandaa kitunguu saumu kwa ajili ya kusaidia kutuliza vidonda vya kooni kwa watu wenye maambukizi ya Ukimwi.
Chukua punje nne za kitunguu saumu, maji kikombe kimoja, na sukari au asali.
Menya na katakata kitunguu, tia kwenye maji yanayochemka, acha kichemke kwa dakika 10. Epua, funika na acha ipoe, kisha ongeza asali au sukari kwa ajili ya ladha.
Kunywa kikombe kimoja kutwa mara tatu.