Ushiriki wa wanawake ndani ya vyama vya siasa gumzo

Dar es Salaam. Baadhi ya wadau wa siasa wametofautiana kuhusu demokrasia, ikiwamo ushirikishi wa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika chaguzi Tanzania.

Wamesema vigezo vinapaswa kuzingatiwa, huku wengine wakivitaka vyama vya siasa viache mfumo dume.

Wametoa maoni hayo leo Ijumaa Septemba 20, 2024 wakati wa mkutano wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Demokrasia inayoadhimishwa kila Septemba 15. Maadhimisho hayo yameambatana na majadiliano kuhusu tathmini ya hali ya demokrasia nchini.

Mkutano huo uliongia siku ya pili leo umeandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) na kuhudhuriwa na viongozi waandamizi wa siasa, wadau, wanafunzi wa vyuo vikuu na asasi za kiraia.

Akichangia mjadala, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Afrika (Wildaf), Anna Kulaya amesema bado kuna shida katika mifumo ambayo mingi inaongozwa na wanaume, akiwataka kuacha ubinafsi.

Kulaya amesema kwa mujibu wa ripoti ya TCD kuhusu ushiriki wa wanawake katika demokrasia na uchaguzi inaonyesha kundi hilo lipo chini katika kuwania ubunge wa majimbo na udiwani wa kata tofauti na wanaume.

“Mara nyingi huwa tunaangalia sababu za nje, mara wanawake hawana usalama au ujasiri lakini ndani ya vyama hawa wanaume ujasiri wanaoutoa wapi? Utashi ndani ya vyama vya siasa unahitajika.

“Tunapoelekea katika uchaguzi tuna fursa, tunaomba tuone utashi ndani ya vyama vya siasa, kama vikiamua kuwatoa wanawake vijana na watu wenye ulemavu kwenye siasa inawezeka na takwimu hizi za TCD zitasogea,” amesema.

Kulaya amesema ukizungumza na wanawake ndani ya vyama vya siasa utabaini tatizo lililopo siyo nje, akisema wananchi hawana shida hata wakipelekewa mgombea wa jinsia hiyo wanamchagua.

“Wanawake wanaopelekwa asilimia 90 wanashinda shida siyo jamii, bali vyama vya siasa ambako kuna changamoto ya ubaguzi, mifumo na unyanyasaji wa kimfumo.

“Wanawake wamekuwa wakilalamika wakichukua fomu, wanaanza kufuatwa kwamba wao ‘si mna viti vyenu maalumu’ tuachieni sisi huku (jimbo), ndiyo maana tunasema kuna ubinafsi ndani ya vyama,” amesema Kulaya.

Naibu Katibu Mkuu wa Chadema -Zanzibar, Salum Mwalimu amekuwa na maoni tofauti aliyeanza kuwaomba radhi wanawake na kuwaambia tatizo kubwa lipo kwao akidai baadhi yao wapo kwa ajili ya kusaka fursa.

“Tatizo ninaloliona bado hamjabadili fikra, dada zetu siku hizi mnapambania fursa, ndiyo maana mmekuwa wakulalamika tu… ndiyo maana mnaona haya mapambano kwa ajili ya fursa au kupata huruma.

“Sasa utapataje huruma kirahisi katika uchaguzi? Unaangalia takwimu za wanawake waliojitokeza kuwania ubunge wa jimbo unakuta 670 haya tuambieni waliojaza viti maalumu kama hawajafika 8,000,” amesema Mwalimu.

Mwalimu amesema huwezi ukamwambia mfano Salima Mwalimu akagombee sehemu fulani wakati kuna mtu (mwanaume) ambaye akiwania nafasi hiyo atapata kura nyingi.

Amewataka wanawake kuacha kupambana kung’oa wanaume badala yake waende sambamba katika michakato hiyo.

Mbunge wa zamani wa Mtwara Vijijini (CCM), Hawa Ghasia amesema wanawake wana uwezo sawa na wanaume lakini bado kuna changamoto ya mfumo dume.

“Lakini nisikitike amesimama Salum Mwalimu (Naibu Katibu Mkuu), kama lugha anazozungumza ndiyo hizo hivi kweli huyu atasimama kumtia moyo mwanamke agombee kama lugha zake ndiyo hizi za mfumo dume?

“CCM na ACT – Wazalendo wanafanya vizuri wana kiongozi wao mwanamke (Dorothy Semu) vyama vya siasa vikiamua wanawake wenye uwezo wapo,” amesema Ghasia aliyewahi kuwa Waziri wa Tamisemi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Bob Wangwe amesema, “tutafakari tunahitaji hawa wawepo tu au? Ninachoamini kinachohitajika katika nafasi za uongozi ni watu wenye uwezo wa kutatua changamoto za wananchi.

“Siamini upewe nafasi kwa sababu unavaa sketi au umri wako mdogo (kijana), ukiwa Jaji Warioba (Joseph) na kijana wa miaka 24 au 30  katika uongozi mimi namchagua Jaji Warioba hata kama ana miaka 100, namna nzuri ni kuwajengea uwezo wanawake na vijana ili kupata nafasi,” amesema Wangwe.

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amesema siyo kwa sababu vyama vya siasa havipeleki wagombea bali mfumo wenyewe uliopo haupo katika mazingira rafiki.

“Tuna wabunge watatu ndani ya Bunge wawili wanawake, kuna wabunge wanane wa vyama vingine vya upinzani kati yao wanawake watatu na wanaume watano, siyo kwa sababu hatukuweka wagombea lakini kura ndizo zilizoamua.

“Mazungumzo yenu yote yanalenga CCM… tukiyazungumzia haya, tuwashauri pia chama tawala wanachopaswa kufanya,” amesema Profesa Lipumba.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Watu Wasiojiweza Tanzania (Mowodita), Nuru Awadh ametaka kuwepo ukomo siyo kila siku viongozi wanakuwa wale wale, badala yake watu wengine wapewe nafasi.

Mratibu wa Taasisi ya Wanawake ya Ulingo, Dk Ave-Maria Semakafu ameshauri kuwepo kwa misingi ya demokrasia na misingi ya kisheria ndani ya vyama vya siasa ili kuondoa ukandamizaji wa kiumfumo dhidi ya wanawake katika vyama hivyo.

Hata hivyo, Katika Sheria ya Vyama vya Siasa vyama vinalazimika kwa mujibu wa sheria kuwa na sera itakayojali masuala ya jinsia ikiwamo kuanzisha dawati la jinsia. Chama cha ACT-Wazalendo kwa nyakati tofauri kimeeleza kuwa tayari kina sera hiyo.

Tangu kuanza kwa mfumo wa siasa za vyama vingi ni chini ya asilimia 10 ya wanawake walioshinda ubunge kwa kuchaguliwa.

Katika Bunge la sasa kati ya wabunge 264 kutoka majimboni 26 pekee ndiyo wanawake, sawa na asilimia 9.4.

Kwa miaka kadhaa kumekuwa na harakati za kuhakikisha unafikiwa usawa wa kijinsia wa asilimia 50 kwa 50.