Ushindi wa Janabi, mwanga mpya afya ya Afrika

Ushindi wa Janabi, mwanga mpya afya ya Afrika

Ushindi wa Profesa Mohamed Janabi kuwa Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika ni hatua ya kihistoria na fahari kubwa kwa Tanzania na Bara la Afrika kwa ujumla.

Ni ushindi wa kitaifa na wa Kiafrika, ambao unawakilisha matumaini mapya ya kupambana na changamoto sugu za kiafya zinazoikabili Afrika.

Profesa Janabi, si tu kwamba anawakilisha ubora wa taaluma ya tiba kutoka Tanzania, bali pia anakuwa alama ya uongozi thabiti na wenye dira katika kipindi ambacho bara linahitaji zaidi ya mabadiliko ya kimfumo, linahitaji msukumo wa kiuongozi wenye maono.

Katika historia ya changamoto za kiafya, Afrika imeendelea kupambana na matatizo kama vile uhaba mkubwa wa watumishi wa afya, miundombinu isiyo thabiti ya hospitali, na milipuko ya magonjwa ya mara kwa mara kama Ebola, kipindupindu na malaria.

Pia Magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama kisukari, shinikizo la damu, magonjwa ya moyo, na saratani yanazidi kuongezeka kwa kasi kubwa, ikisababisha mzigo mkubwa kwa mifumo ya afya.

Hali hii inahatarisha maendeleo yaliyopatikana na kuleta hatari ya kuendelea kuathiri maisha ya watu wengi, hasa wale wa kipato cha chini. Kwa hiyo, juhudi za kuhimiza uelewa wa magonjwa haya ni muhimu, ikiwa ni pamoja na kuhamasisha mabadiliko ya mtindo wa maisha na kutoa elimu kuhusu umuhimu wa kujikinga.

Pamoja na hayo, ukosefu wa chanjo ni tatizo sugu linalohitaji mkazo wa kipekee. Chanjo ni njia bora ya kuzuia magonjwa hatari kama surua, pepopunda na rubella, lakini bado kuna maeneo mengi upatikanaji wake haujafikiwa kikamilifu.

Takwimu za WHO zinaonyesha kuwa ni asilimia 46 tu ya Waafrika wanaopata huduma bora za afya, hali ambayo iko mbali na lengo la kimataifa la kufikia asilimia 68 ifikapo mwaka 2030. Hii ni changamoto halisi inayohitaji uongozi wa dhati na maamuzi ya kimkakati, majukumu ambayo sasa yanamkabili Profesa Janabi.

Katika hotuba yake ya awali, Profesa Janabi alionyesha wazi kuwa anafahamu ukubwa wa jukumu alilopewa. Alitaja vipaumbele saba ambavyo vitatoa mwelekeo mpya kwa sekta ya afya barani Afrika, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wote, kuongeza rasilimali fedha kwa ajili ya sekta ya afya, na kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa afya ya umma.

Kwa Tanzania, ni ushindi wa juhudi za kidiplomasia na uthibitisho wa heshima ya kitaifa katika majukwaa ya kimataifa. Kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan, akimpongeza Profesa Janabi, inadhihirisha kuwa taifa limewekeza imani kubwa katika uwezo wake.

Tunaamini kuwa kupitia nafasi hii, kuna matarajio ya kuimarika kwa ushirikiano wa kanda ya Afrika Mashariki na WHO, ikiwemo mikakati ya pamoja ya kukabiliana na milipuko ya magonjwa, mafunzo ya wataalamu wa afya na uboreshaji wa miundombinu ya sekta ya afya.

Tunaamini kuwa kwa ushirikiano wa kweli wa Kiafrika, mchango wake utaacha alama ya kudumu katika historia ya afya ya umma barani Afrika.

Kwa dhati, tunampongeza Profesa Janabi kwa ushindi huu mkubwa. Hongera kwa kuchaguliwa kuwa nahodha wa afya wa Afrika. Sasa ni wakati wa kulifanya bara letu kuwa mahali salama zaidi kiafya kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *