Ushambuliaji, ulinzi tatizo Fountain Gate

BAADA ya mapumziko ya takribani siku tano, kikosi cha Fountain Gate kimerejea kambini kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Singida Black Stars, Aprili 2, huku kocha wa kikosi hicho, Mkenya, Roberto Matano akikomalia mambo mawili yanayoonekana kuwa tatizo sugu kwao.

Timu hiyo katika michezo 23 ya Ligi Kuu Bara msimu huu, imefunga mabao 28 ikiwa na wastani wa kufunga bao 1.2 kila mechi, huku ikiruhusu 40 kwa wastani wa 1.7 kila mechi. Fountain Gate ni kati ya timu mbili zilizoruhusu mabao mengi zaidi msimu huu sambamba na KenGold.

Akizungumza na Mwanaspoti, Matano alisema mambo anayokabiliana nayo ni katika eneo la ulizi na ushambuliaji kwani bado hajaridhishwa nayo, jambo linalomfanya kufanya mabadiliko ya mara kwa mara kutokana na changamoto hiyo.

“Ni changamoto ambayo haiwezi kuisha kwa siku moja ndio maana tunarudi kwenye uwanja wa mazoezi ili kuhakikisha kama sio kuimaliza basi tuipunguze, najaribu kuingiza pia mifumo yangu taratibu kutokana na aina ya wachezaji waliopo,” alisema.

Matano alisema licha ya hayo, moja ya mambo yanayompa matumaini makubwa ni safu ya kiungo ambayo hadi sasa imekuwa na muunganiko mzuri wa kutengeneza nafasi kwa washambuliaji, hivyo hiyo ni ishara bora kwake kwa michezo iliyombele.

Kocha huyo tangu ateuliwe Januari 10, 2025 akitokea Sofapaka ya kwao Kenya, amekiongoza kikosi hicho katika jumla ya michezo yake saba ya Ligi Kuu Bara, ambapo kati ya hiyo ameshinda miwili na kutoka sare miwili na vipigo vitatu.

Matano aliyechukua nafasi ya Mohamed Muya aliyeondoshwa Desemba 29, 2024 baada ya kikosi hicho kuchapwa mabao 5-0 dhidi ya Yanga, katika michezo yake saba timu yake imefunga mabao manne na kuruhusu manane.

Hadi Muya anaondoka aliiongoza katika michezo 16 ya Ligi Kuu ambapo kati hiyo alishinda sita, sare miwili na kupoteza minane, ingawa kiujumla imecheza 23, ikishinda minane, sare minne na kupoteza 11, ikiwa nafasi ya saba na pointi 28.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *