Unguja. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imetangaza kuwa iko katika hatua za mwisho za kuandaa viwango maalumu vya nauli kwa waendesha bodaboda, ili kuondoa changamoto ya kila mmoja kuweka bei anayoitaka, hivyo kuwaumiza wananchi wanaotegemea usafiri huo.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Nadir Abdulatif Yussuf, leo Alhamisi, Mei 15, 2025, wakati akijibu maswali ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi katika kipindi cha maswali na majibu.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Nadir Abdulatif Yussuf akizungumza barazani.
Katika swali la nyongeza, Mwakilishi wa Nungwi, Abdalla Abasi Wadi, ameeleza kuwa tatizo la waendesha bodaboda kujipangia bei kiholela limekuwa likiwaumiza wananchi wengi.
Ametaka kufahamu mpango wa Serikali kuhusu utoaji wa bei elekezi kwa huduma hiyo, kama inavyofanyika kwenye vyombo vingine vya usafiri.
Naye Mwakilishi wa Ziwani (CCM), Suleiman Ali Makame, amesema kuwa Serikali inawaonea wananchi, kwani hoja ya kurasimishwa kwa bodaboda ililetwa barazani mwaka 2018 na Dk Mohamed Said Dimwa (Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar), wakati huo akiwa mjumbe wa Baraza.
Amesisitiza kuwa, kama mpaka Serikali haijachukua hatua ya kuweka bei elekezi kwa huduma ya bodaboda, wananchi wamekuwa wakiteseka kutokana na waendesha bodaboda kujipangia bei kubwa kupita kiasi.
Akijibu hoja hiyo, Naibu Waziri amesema kuwa kwa sasa bei elekezi ipo kwa usafiri wa ndege, bandarini, na daladala, lakini Serikali iko kwenye utaratibu wa kuweka bei elekezi kwa bodaboda.
“Tupo kwenye utaratibu wa kuhakikisha kuwa bodaboda nazo zitakuwa na bei maalumu badala ya kila mmoja kujipangia bei yake mwenyewe, ili wananchi wafaidi usafiri huu kwa bei inayofaa,” amesema Naibu Waziri.
Katika swali la msingi, Mwakilishi Wadi amehoji kuhusu hatua zinazochukuliwa dhidi ya waendesha bodaboda wanaokiuka sheria barabarani, kwani wanatengeneza kero kubwa katika jamii, na jinsi utoaji wa leseni unavyofanywa katika maeneo ya wilaya.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri Nadir amesema kuwa hatua zinazochukuliwa ni pamoja na ushirikiano kati ya mamlaka husika na Jeshi la Polisi, ambapo hufanya operesheni za mara kwa mara kuwakamata waendesha bodaboda wanaokiuka sheria za usalama barabarani.
Nadir amesema waendesha bodaboda hao hutozwa faini na pia wanatakiwa kuhudhuria mafunzo kabla ya kuendelea kutoa huduma hiyo.
“Hadi kufikia Machi 2025, jumla ya bodaboda 517 zimekamatwa kwa makosa mbalimbali ya uvunjifu wa sheria za usalama barabarani,” amesema Nadir.
Amesema mamlaka inaendelea kukamilisha utaratibu wa majaribio kwa madereva, ambapo baada ya kufanyiwa majaribio, hupatiwa cheti cha umahiri.
Nadir amesema cheti hicho kinawawezesha madereva kupata leseni katika ofisi za Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) zilizopo katika mikoa yote ya Unguja na Pemba.
Amesema Serikali ilirasimisha biashara ya bodaboda kwa kuweka utaratibu kwa wale watakaofanya biashara hiyo kwa kufuata utaratibu wa kupata mafunzo ya udereva, kuwa na leseni ya udereva na vigezo vingine.
“Tunaiomba jamii kufuata sheria zilizowekwa bila ya shuruti, ikiwemo waendesha bodaboda kuacha vitendo vyote vinavyokwenda kinyume na sheria zetu, ambavyo ni kero kwa jamii.
“Hata hivyo, mamlaka za kusimamia sheria nazo zinatakiwa kuchukua hatua ipasavyo kwa wale wote ambao wataendesha bodaboda kinyume cha utaratibu uliowekwa,” amesema Nadir.