Hujuma hizo zinafanyika wakati Jumuiya ya Kimataifa ikifanya juhudi za kujaribu kutafuta namna ya kupatikana amani.
Ujerumani ni mojawapo ya mataifa ya jumuiya ya kimataifa ambayo ni mshirika mkubwa wa Ukraine na inajaribu kutafuta njia za kusadia kupatikana amani kwenye mzozo huo.Urusi yaishambulia Kharkiv kwa droni na kusababisha vifo vya watu 2
Waziri wa ulinzi wa nchi hiyo Boris Pistrorius amewasili Kiev masaa machache yaliyopita ambako anataka kujadili kwa kina suala la kuipatia Ukraine msaada zaidi wa silaha katika wakati ambapo juhudi za kumaliza vita hivyo vya miaka mitatu na Urusi zikionesha kukabiliwa na changamoto na Moscow imekuwa ikiimarisha mashambulizi yake dhidi ya Ukraine.
Waziri huyo wa Ujerumani Boris Pistorius amesema mojawapo ya malengo ya ziara yake ni kuonesha mshikamano na Ukraine.
“Ziara hii haina malengo maalum, lakini kimsingi inadhamiria kuonesha kwamba kwa hivi sasa Ujerumani ina bunge na serikali mpya na inaendelea kusimama pamoja na Ukraine katika kile ambacho kinaonekana kuwa bado ni hali ngumu.”
Urusi na Ukraine ziliwahi kukutana kwa mazungumzo mjini Istanbul nchini Uturuki mwanzoni mwa mwezi huu kwa lengo la kutafuta amani lakini zilishindwa kukubaliana kuhusu suala la Urusi kuyaachia maeneo ya Ukraine iliyoyanyakuwa na suala la Ukraine kukubaliwa kuwa mwanachama wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO.
Na vita vimekuwa vikiendelea kushika kasi. Urusi imeongeza mashambulizi ya kutumia Droni. Siku ya Jumatano watu sita waliuwawa kwenye mashambulio yaliyofanywa na nchi hiyo yakiulenga mkoa wa Kharkiv unaokaribiana kabisa na Urusi.
Usiku wa Kuamkia leo mashambulizi mengine ya Droni yamewajeruhi watu 15 wakiwemo watoto wanne mashariki wa mji wa Kharkiv.Msemaji wa huduma za dharura kwenye mkoa huo Yevhen Vasylenko amezungumzia mashambulizi hayo.
”Usiku wa kuamkia leo adui alifanya mashambulio makubwa sana dhidi ya mji wa Kharkiv, yakilenga hasa maeneo ya makaazi ya watu katika sehemu mbali mbali za mji.”
Gavana wa mkoa wa Kharkiv Oleh Syniehubov amesema mkoa wote umeshuhudia mashambulio ya Urusi,yaliyoharibu miundo mbinu inayotumiwa na raia,ikiwemo majumba 11 ya raia,magari na shule mbili.Urusi yaifunika Ukraine kwa usiku mwengine wa droni
China nayo imesema kwamba imembadilisha mjumbe wake anayehusika na masuala ya Kidiplomasia katika mgogoro huo wa Ukraine.
Hivi sasa Sun Linjiang aliyekuwa balozi wake nchini Poland ameteuliwa mjumbe maalum kuhusu masuala ya mahusiano kati ya Ulaya na Asia akichukuwa nafasi ya Li Hui aliyekuwa akiiwakilisha China kuendesha shughuli za kidiplomasia barani Ulaya na kwengineko kwa lengo la kutafuta suluhu ya kisiasa katika vita vya Ukraine.
China imekuwa ikijinadi kama mshirika asiyeegemea upande kwenye vita hivyo, japo serikali za mataifa ya Magharibi zinasema Beijing imekuwa ikiisadia Moscow Kiuchumi na kidiplomasia kutokana na ushirika wao wa karibu.