
Mazungumzo ya simu kati ya Vladimir Putin na Donald Trump, ambayo yamelenga juu ya pendekezo la kusitisha vita nchini Ukraine, yamefanyika Jumanne, Machi 18. Mwishoni mwa mkutano huo, Kremlin imesema kuwa imekubali kusitisha mashambulizi kwenye miundombinu ya nishati nchini Ukraine kwa siku 30. Urusi imefahamisha Marekani kuhusu masharti yake ya kusitisha mapigano, ikiwa ni pamoja na kusitisha msaada wa nchi za Magharibi kwa Kyiv.
Imechapishwa:
Dakika 3
Matangazo ya kibiashara
Vladimir Putin na Donald Trump wamekubaliana siku ya Jumanne, Machi 18, kuhusu usitishwaji mapigano kwenye miundombinu ya nishati, lakini mazungumzo yao ya simu yaliyokuwa yakitarajiwa yamemalizika bila mafanikio yoyote makubwa kuelekea makubaliano ya kweli ya kusitisha mapigano kati ya Urusi na Ukraine.
Usitishaji wa mapigano kwa sehemu
Urusi inasema Rais wa Urusi Vladimir Putin amekubali kusitisha kwa siku 30 kwa pande zote mashambulizi kwenye miundombinu ya nishati ya Ukraine, pendekezo lililopendekezwa na Donald Trump wakati wa mazungumzo ya simu. Rais wa Urusi “ameitikia vyema” mpango huo wa rais wa Marekani na “mara moja akatoa amri kwa wanajeshi wa Urusi,” Kremlin imesema katika taarifa yake ikitoa muhtasari wa wito huo na rais wa Marekani. Zaidi ya hayo, taarifa hiyo inahakikisha kwamba wafungwa 175 wa vita kutoka kila upande watakabidhiwa mamlaka ya kila upande siku ya Jumatano, Machi 19: “Vladimir Putin ametangaza kwamba Machi 19, Urusi na Ukraine zitabadilishana wafungwa – watu 175 kwa 175.”
Volodymyr Zelensky amezungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari mtandaoni, akisema anaunga mkono kimsingi usitishwaji mapigano wa siku 30 na Urusi katika mashambulizi yake kwenye miundombinu ya nishati, lakini amesisitiza juu ya hitaji la kupata “maelezo” kutoka Washington. “Tutaunga mkono mapendekezo kama haya, lakini inafurahisha sana kujua maelezo na ni nini hasa kinapendekezwa,” rais wa Ukraine amesisitiza.
Urusi inakumbuka masharti yake ya amani
Vladimir Putin pia ametoa wito kwa mwenzake wa Marekani “kusitisha kabisa” msaada wa kijeshi wa Magharibi na kugawana taarifa za kijasusi zinazotolewa kwa Ukraine: “Imesisitizwa kwamba sharti muhimu la kuzuia kuongezeka kwa mzozo na kufanyia kazi utatuzi wake kwa njia za kisiasa na kidiplomasia lazima iwe kukomesha kabisa msaada wa kijeshi wa kigeni na utoaji wa habari kwa Kyiv. “
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema kuwa masharti yaliyowekwa na mwenzake wa Urusi Vladimir Putin kwa ajili ya usitishwaji mapigano na Kyiv yanalenga “kuidhoofisha” Ukraine na kuonyesha kwamba hayuko tayari “kumaliza” vita. “Mchezo wake wote ni kutudhoofisha iwezekanavyo,” Zelensky amesema.
Kufuatia matamshi hayo, Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron wameihakikishia Ukraine kuendelea kwa misaada ya kijeshi kwa nchi hiyo dhidi ya Urusi. “Sote wawili tunakubali kwamba Ukraine inaweza kututegemea, kwamba Ukraine inaweza kutegemea Ulaya, na kwamba hatutaiangusha,” Olaf Scholz amesema mjini Berlin pamoja na Emmanuel Macron, ambaye amehakikisha: “Tutaendelea kuunga mkono jeshi la Ukraine katika vita vyake vya upinzani dhidi ya uvamizi wa Urusi.”
Mazungumzo kufanyika haraka
Mazungumzo juu ya mzozo yanapaswa kuanza “mara moja.” Mazungumzo haya yatafanyika Mashariki ya Kati, Ikulu ya White House imetangaza katika taarifa, ambayo imependekeza “faida kubwa” ya uhusiano “bora” kati ya Marekani na Urusi. Kwa hivyo imetaja “mazungumzo ya kiufundi juu ya kuanzishwa kwa usitishaji mapigano wa baharini katika Bahari Nyeusi, juu ya usitishaji kamili wa mapigano na amani ya kudumu.”
“Rais wa Urusi amesema yuko tayari kufanya kazi na mshirika wake Marekani katika uchunguzi wa kina wa njia zinazowezekana za kufikia suluhu, ambayo inapaswa kuwa ya kina, thabiti na ya kudumu,” taarifa ya Kremlin imesema. Jeshi la Ukraine linaendelea kupigana katika eneo la Kursk, Rais Volodymyr Zelensky amesema baada ya vikwazo vya hivi karibuni vilivyosababishwa na askari wake huko: “Jeshi la Ukraine lipo. Na watakaa huko mradi tu tunahitaji operesheni hii.”
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alisema mjini Berlin siku ya Jumanne kwamba makubaliano hayo lazima “yathibitishwe” nchini Ukraine na kwamba Waukraine lazima wahusishwe katika majadiliano. “Lengo lazima libaki lile lile: kuwa na usitishaji mapigano unaopimika na unaoweza kuthibitishwa, kuheshimiwa kikamilifu (…) amani thabiti na ya kudumu na dhamana inayoambatana nayo,” amesema pamoja na Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz. “Ni wazi, hili haliwezekani bila Waukraine kuwa kwenye meza ya maungumzo,” amesema.