Urusi: Putin asema nchi za Ulaya ‘zinaweza kushiriki’ katika utatuzi wa mgogoro wa Ukraine

Rais wa Urusi Vladimir Putin amesema siku ya Jumatatu, Februari 24, kwamba nchi za Ulaya zinaweza “kushiriki” katika mchakato wa kusuluhisha mzozo wa Ukraine, wakati EU inahofia kutengwa tangu kuanza kwa mazungumzo ya moja kwa moja kati ya Moscow na Washington.

Imechapishwa:

Dakika 2

Matangazo ya kibiashara

“Nchi za Ulaya, lakini pia nchi zingine, wana haki na fursa ya kushiriki. Na tunaheshimu hilo,” Vladimir Putin amesema katika mahojiano ya televisheni.

Amesisitiza kuwa ni nchi za Ulaya zilizojitenga na Urusi baada ya kuanza kuishambulia Ukraine miaka mitatu iliyopita. “Wao wenyewe walikataa kuwasiliana nasi, na kila aina ya mawazo ya kujipa moyo ya kuishinda Urusi kwenye uwanja wa vita,” amesema. “Ushiriki wao katika mchakato wa mazungumzo ni muhimu. “Hatukukataa kamwe,” ameongeza.

Vladimir Putin amesisitiza kwamba mazungumzo ya Urusi na Marekani yaliyofanyika wiki iliyopita nchini Saudi Arabia, ya kwanza katika ngazi hii tangu kuanza kwa mzozo na ambayo Kyiv na nchi za Ulaya zilitengwa, yalilenga “kuimarisha imani” kati ya Moscow na Washington.

“Hakuna swali linaloweza kutatuliwa bila hili. Ikiwa ni pamoja na suala tata na kali kama mgogoro wa Ukraine, “amesema. Mawaziri wa mambo ya nje wa Urusi na Marekani Sergei Lavrov na Marco Rubio walijadili nchini Saudi Arabia “masuala yanayohusiana na mzozo wa Ukraine, lakini sio mgogoro wa Ukraine wenyewe,” kulingana na Vladimir Putin.

Volodymyr Zelensky, “kiongozi mbaya” kulingana na Vladimir Putin

Kiongozi wa Urusi, hata hivyo, alimwita mwenzake wa Ukraine Volodymyr Zelensky “kiongozi mbaya,” akirudia baadhi ya ukosoaji mkali uliotolewa wiki iliyopita na Donald Trump dhidi ya rais wa Ukraine. Vladimir Putin amemshutumu Volodymyr Zelensky kwa “kutoa amri za kejeli” kwa askari wake, na kusababisha “hasara isiyo ya haki, hata ya juu sana au ya janga kwa jeshi la Ukraine”, na kuwa “sababu katika mtengano wa jeshi, jamii na serikali”.

Amemshutumu kwa “kukwepa mazungumzo” kwa kusema kwamba Volodymyr Zelensky alipiga marufuku kwa amri mnamo Oktoba 2022 mazungumzo yoyote na Vladimir Putin, na alizingatia kwamba nafasi yake ya kushinda uchaguzi ujao wa urais nchini Ukraine ni “hafifu kabisa”.

Shutuma hizi zinafanana na zile za Donald Trump, ambaye alimwita Volodymyr Zelensky “dikteta” na kufikia hatua ya kumlaumu kwa mzozo huo.