
Serba. Katika hali isiyo ya kawaida, wabunge wa upinzani nchini Serbia wamerusha mabomu ya machozi ndani ya bunge ili kupinga uamuzi wa Serikali kumkingia kifua Rais, Aleksandar Vucic anayepingwa nchini humo kwa uzembe na madai ya rushwa.
CNN imeripoti leo Jumanne Machi 4,2025, kuwa kundi la wabunge hao wa upinzani wamechukua uamuzi huo ikiwa ni kuunga mkono maandamano ya wanafunzi waliokuwa wakiandamana kupinga utawala wa Rais Vucic.
Kufuatia kitendo hicho wabunge baadhi wamepata mshtuko ikiwemo kupata majeraha huku mmoja akipata kiharusi wakati wa vurugu hizo.
Maandamano yanayoongozwa na wanafunzi kwa miezi minne, yalianzishwa na wanafunzi na walimu wa shule za sekondari na vyuo nchini humo na baadaye kuungwa mkono na wakulima na makundi mengine huku yakitajwa kuwa tishio zaidi kwa utawala wa Rais Aleksandar Vucic ambao umedumu kwa muongo mmoja.
Katika kikao cha bunge, baada ya muungano wa chama tawala unaoongozwa na Chama cha Maendeleo cha Serbia (SNS) kupitisha ajenda ya mkutano, baadhi ya wanasiasa wa upinzani walitoka kwenye viti vyao na kuelekea kwa spika wa bunge kisha kuzuka mtafaruku kati yao na maofisa usalama wanaolinda bunge hilo.
Wengine walirusha mabomu ya machozi ndani ya bunge hilo huku televisheni ya taifa ikirusha tukio hilo mubashara (moja kwa moja) ikionyesha moshi mweusi na ndani ya bunge ambalo kwa miongo kadhaa limewahi kushuhudia mapigano na hata kurushiana maji tangu kuanzishwa kwa demokrasia ya vyama vingi mwaka 1990.
Spika wa Bunge, Ana Brnabic amesema wabunge wawili wamejeruhiwa, mmoja wao akiwa Jasmina Obradovic wa chama cha SNS, aliyepata kiharusi na hali yake imebadilika na kuwa mbaya.
“Bunge litaendelea kufanya kazi na kulinda Serbia,” amesema Brnabic wakati wa kikao.
Baada ya sintofahamu hiyo, kikao cha bunge kiliendelea, wanasiasa wa muungano tawala walijadili huku wabunge wa upinzani wakipiga filimbi na kupuliza matarumbeta ili kuhakikusha kikao hicho hakiendelei.
Wabunge wa upinzani pia walibeba mabango yaliyoandikwa: “Mgomo wa jumla” na “Haki kwa waliouawa”, huku nje ya jengo waandamanaji wakisimama kimya kuwaenzi watu 15 waliouawa baada ya paa la kituo cha reli kuporomoka tukio lililochochea kuanza kwa maandamano hayo kuwa vifo vya watu hao vilisababishwa na uzembe wa Serikali.
Viongozi wa maandamano walitoa wito wa kufanyika kwa maandamano makubwa katika mji mkuu wa Belgrade Machi 15, mwaka huu.
Chama tawala nchini humo, kimedai kuwa mashirika ya kijasusi ya Magharibi yanajaribu kuleta machafuko nchini Serbia na kuuangusha utawala wa Serikali iliyoko madarakani kwa kuunga mkono maandamano hayo.
Bunge lilitarajiwa Jumanne kupitisha sheria ya kuongeza fedha kwa vyuo vikuu moja ya madai makuu ya wanafunzi waliokuwa wakizuia shughuli za vyuo tangu Desemba, 2024.
Bunge pia lilipaswa kuthibitisha kujiuzulu kwa Waziri Mkuu, Milos Vucevic, lakini mambo mengine yaliyoingizwa kwenye ajenda na muungano tawala yaliwakasirisha wabunge wa upinzani na kufikia uamuzi huo.