
Unguja. Wakati Serikali ikihamasisha wananchi kujikita kwenye ufugaji wa kaa na majongoo baharini ili kujikwamua kiuchumi, wafugaji hao wameeleza changamoto ya upepo kuwarejesha nyuma katika jitihada hizo.
Wafugaji wa kaa na samaki kutoka Chwaka, wamesema upepo unawaathiri na kuharibu miundombinu yao.
Wametoa kauli hiyo leo Jumatatu, Machi 3, 2025, wakati mkuu wa kitengo cha ufugaji wa mazao ya baharini, Sharifa Moh’d Miraji alipofanya ziara ya kikazi katika maeneo ya wafugaji wa Chwaka na Bambi Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja.
“Changamoto mbalimbali zinajitokeza wakati wa upepo mkali na kupelekea kuharibika kwa mabwawa ya kufugia,” amesema mfugaji wa kaa, Khamis Ali, mkazi wa Chwaka.
Hata hivyo, amesema changamoto hiyo isiwe sababu ya kuwafanya wasiendelee na shughuli za ufugaji huo, badala yake waendelee huku wakizitafutia ufumbuzi changamoto hizo.
Mfugaji mwingine, Ayoub Makame, amesema jamii inapaswa kutilia uzito shughuli za ufugaji wa mazao ya baharini, kwani kazi hiyo ina tija kwa jamii na maslahi makubwa kwa wafugaji na Taifa kwa ujumla.
Naye mkuu wa kitengo cha ufugaji wa mazao ya baharini, Sharifa Moh’d Miraji, amesema lengo la ziara hiyo ni kujua changamoto zinazowakabili wafugaji hao na kuzitafutia ufumbuzi, pamoja na kujenga uhusiano wa karibu kati ya wataalamu na wakulima hapa nchini.
Sambamba na hayo, ametoa wito kwa wafugaji kuachana na kufuga kimazoea na kufuga kwa njia za kisasa, ambazo ni za kibiashara zaidi ili zilete tija kwa maslahi ya jamii na Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake, mwakilishi kutoka Kampuni ya South South Partnership Ltd, Mariam Hamis Kombo, ameitaka jamii ya Zanzibar kutumia samaki wa maji baridi aina ya sato, kwani wana virutubisho vingi kwa afya ya binadamu, sawa na samaki wa baharini.