Waziri wa Katiba na Sheria Dkt Damas Ndumbaro amesema upendo wa Rais wa Jamhuri wa Muungano Dkt Samia Suluhu Hassan kwa wananchi wake haujaishia katika kuleta maendeleo kupitia miradi mbalimbali bali umeenda hadi katika kuhakikisha wanapata haki zao.
Dkt Ndumbaro ameeleza hayo katika nyakati mbalimbali akiwa ziarani Mkoani Kagera akikagua miradi ya maendeleo kama mlezi wa mkoa huo ili kujiridhisha endapo fedha zinazo tolewa na serikali zinatumika kwa ufanisi.
Amesema,” hakuna asiyeona kazi kubwa aliyoifanya Rais wetu Dkt Samia Suluhu Hassan katika sekta mbalimbali, amejitahidi kugusa kila eneo iwe barabara,elimu, afya, ajira na sasa Rais Samia anahakikisha wananchi wake wanapata haki na kujua haki zao kupitia Kampeni ya Msaada wa kisheria inayo tekelezwa nchini kote”.
Amesisitiza kuwa Ibara ya 13 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeeleza bayana kuwa binadamu wote ni sawa mbele ya haki hivyo Rais Samia ameona awasaidie wananchi ambao wanauhitaji wa kupata haki lakini hawamudu gharama.
“Huduma za Msaada wa Kisheria zinatolewa bure kwa wananchi wote bila kujali chama chako cha siasa kabila umri ili mradi wewe ni mtanzania Rais wetu mwenye upendo atahakikisha unahudumiwa na wanasheria wabobezi ili upate haki yako”, amesisitiza Dkt Ndumbaro
Aidha ameongeza kuwa kuna baadhi ya wanasiasa wanatoa kauli za kupotosha kwa wananchi na kuwahamasisha kuwa haki ya mwananchi ni maandamano na kususia uchaguzi badala ya kuwaelimisha mambo ambayo serikali imeyafanyia kazi kubwa katika sekta zote ili kuhakikisha nchi inapata maendeleo makubwa.
Dkt Ndumbaro amekagua na kujiridhisha ubora katika miradi mbalimbali ikiwa ni pamoja na mradi wa shule ya msingi Igayaza Wilayani Misenyi, mradi wa ujenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Karagwe, ujenzi wa mradi wa maji Nyabiyonza wilayani Karagwe, ujenzi wa shule ya sekondari ya amali Katerero, zahanati ya Mulahya na mradi wa maji Kemondo wilayani Bukoba.
Miradi mingine aliyokagua Dkt Ndumbaro ni ujenzi wa sekondari ya kasheno na mradi wa maji Kamachumu-Bushagara wilayani Muleba pamoja na mradi ujenzi wa sekondari ya Mahindi na mradi wa maji Nyamigogo -songambele ya Wilayani Biharamulo.
Kwa upande wao viongozi mbalimbali mkoani Kagera wamempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za kufanikisha ujenzi wa miradi mbalimbali.
Mkuu wa Wilaya ya Biharamulo SACP Advera Bulimba amesema katika halmashauri ya Wilaya hiyo wamepokea shilingi bilioni 98 kutoka serikali kuu kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Karagwe Julius Laizer amempongeza Rais Samia kwa kampeni ya Msaada wa Kisheria kwani inapunguza migogoro mingi ambayo imeshindikana kutokana na wananchi kukosa pesa za kugharamia wanasheria na mawakili.
The post UPENDO WA RAIS SAMIA KWA WANANCHI HAUJAISHIA KWENYE MAENDELEO, UMEENDELEA HADI KWENYE HAKI appeared first on Mzalendo.