
Suala la waendesha vyombo vya moto kutumia barabara za mwendokasi kinyume cha sheria limekuwa likijadiliwa mara kwa mara, lakini bado hali hiyo inaendelea.
Bila kibali, barabara hizi hutumiwa na watu mbalimbali, wakiwemo wale wenye nyadhifa serikalini na madereva binafsi wanaoamini kuwa hawawezi kuchukuliwa hatua zozote.
Kila mara Serikali imekuwa ikitangaza hatua mbalimbali kuhakikisha sheria husika inatekelezwa ipasavyo, kwamba barabara hizo zinatumika kwa mabasi ya mwendokasi pekee na pale inapobidi, kwa magari ya dharura kama vile ya wagonjwa na zimamoto.
Hata hivyo, utekelezaji wa sheria umekuwa na changamoto, kwani madereva wa magari ya Serikali wameendelea kuzitumia barabara hizo bila kibali, hali inayosababisha mkanganyiko na kudhoofisha mamlaka ya usimamizi wa sheria.
Kwa ujumla kinachoonekana ni kuwa utekelezaji wa sheria umekuwa na upendeleo, ambapo baadhi ya magari ya viongozi wa serikali yamekuwa yakipita bila kuzuiwa, huku baadhi ya madereva wa magari binafsi wakikabiliwa na hatua kali. Ni utekelezaji wa sheria wenye matabaka.
Mkuu wa Jeshi la Polisi, Camillius Wambura, alinukuliwa Septemba 16, 2022, akieleza kuwa si sahihi kwa magari ya Serikali kupita kwenye barabara hizo isipokuwa kwa yale ya dharura.
Hata hivyo, hali halisi barabarani inaonyesha kuwa madereva wa serikali na binafsi wanaendelea kuvunja sheria, huku hatua zinazochukuliwa zikiwa na mwanya wa upendeleo.
Mathalan, kwa hatua za hivi karibuni ni kuwa dereva binafsi waliokamatwa kwa kutumia barabara hizo wamesema wanapitia hatua kali kama vile kuwekwa mahabusu, kulipa faini na kufikishwa mahakamani.
Hata Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema kuwa dereva anayekamatwa huhojiwa mara mbili, kwa saa nne kila moja, ili kubaini uelewa wake kuhusu matumizi ya barabara za mwendokasi.
Lakini kwa upande mwingine, baadhi ya madereva wa Serikali wamekuwa wakiachiliwa bila hatua zozote madhubuti, hali inayozua hisia za upendeleo na kuleta mgawanyiko wa matabaka barabarani.
Changamoto hii inahitaji suluhisho la haraka kutoka kwa mamlaka husika ili kuhakikisha usawa na haki katika utoaji wa adhabu kwa wote wanaotumia barabara za mwendokasi kinyume cha taratibu.
Sheria mpya inayotarajiwa kutoka Dart, ambayo itabainisha viwango vipya vya adhabu, inatarajiwa kusaidia katika kudhibiti tabia ya uvunjaji wa sheria na kuhakikisha kuwa barabara hizo zinatumika ipasavyo.
Ingawa hatua hii inalenga kuimarisha usimamizi wa sheria, bado kuna haja ya kutoa elimu zaidi kwa umma kuhusu utaratibu wa kupita kwenye barabara hizo wakati wa dharura ili kuepusha malalamiko na migogoro kati ya madereva na askari wa barabarani.
Ili kuondoa tatizo hili, ni muhimu kwa Serikali kuhakikisha kuwa utekelezaji wa sheria unakuwa wa haki kwa wote bila kujali hadhi ya mtu.
Hatua kali zinapaswa kuchukuliwa kwa yeyote anayevunja sheria ili kudhibiti matumizi holela ya barabara za mwendokasi. Upendeleo wa aina yoyote unapaswa kuepukwa, na sheria iheshimiwe kwa usawa na uwajibikaji wa kweli.