Upelelezi kesi ya ‘bwana harusi’ wakamilika

Dar es Salaam. Kesi ya jinai inayomkabili mfanyabiashara Vicent Masawe (36), ‘bwana harusi’, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Dar es Salaam, Kisutu, upelelezi wake kukamilika.

Taarifa za kukamilika kwa upelelezi wa kesi hiyo zimetolewa mahakamani hapo leo, Jumatano, Machi 12, 2025 na mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali, Adolf Velandumi, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kuangalia hali ya upelelezi.

“Mheshimiwa, shauri hili limepangwa leo kwa ajili ya kutajwa. Upelelezi wa shauri hili umeshakamilika, hivyo Tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya usikilizwaji wa awali,” amesema Wakili Velandumi.

Kutokana na kukamilika kwa upelelezi huo, Hakimu Mkazi Mkuu Beda Nyaki, anayesikiliza kesi hiyo amekubaliana na maombi hayo ya upande wa mashtaka na akapanga usikilizwaji wa awali wa kesi hiyo ufanyike Machi 24, 2025.

Hivyo, ameahirisha kesi hiyo mpaka tarehe hiyo kwa ajili ya hatua hiyo ya usikilizwaji wa awali.

Katika hatua hiyo, mshtakiwa atasomewa hoja au maelezo ya awali ya kesi kisha atatakiwa kubainisha mambo anayokubaliana nayo na asiyokubaliana nayo, ambayo upande wa mashtaka utawajibika kuwasilisha ushahidi kuyathibitisha.

Katika kesi hiyo ya jinai namba 35738/2024, Massawe anakabiliwa na mashtaka mawili.

Mshtakiwa huyo ambaye yuko nje kwa dhamana alipandishwa kizimbani mahakamani hapo kwa mara ya kwanza na kusomewa mashtaka Desemba 24, 2024.

Anadaiwa kutenda makosa hayo Novemba 15, 2025 kinyume na vifungu namba 258 na 273(b) vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Katika shtaka la kwanza la wizi wa kuaminika, Masawe anadaiwa akiwa wakala, Novemba 15, 2024 katika Jiji la Dar es Salaam, aliiba gari lenye namba za usajili T 642 EGU aina ya Toyota Ractis.

Gari hilo lenye thamani ya Sh15 milioni, kwa mujibu wa upande wa mashtaka ni mali ya Silvester Masawe.

Anadaiwa kuwa, aliazimwa gari hilo na Silvester kwa lengo la kulitumia katika harusi yake lakini baada ya hapo, hakurudisha gari kama walivyokubaliana.

Katika shtaka la pili ni kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, anadaiwa Novemba 15, 2024 katika Jiji la Dar es Salaam, kwa lengo la kuiba na kutapeli, alijipatia fedha taslimu Sh3 milioni kutoka kwa Silvester.

Anadaiwa kuwa, alijipatia fedha hizo kwa kuahidi kuwa, atamrudishia fedha hizo baadaye, wakati akijua ni uongo na hakuweza kurudisha fedha hizo hadi alipokamatwa.

Kabla ya kukamatwa kisha kufikishwa mahakamani na kusomewa mashtaka hayo, Massawe mkazi wa Ungindoni, Kigamboni jijini Dar es salaam alidaiwa kupotea.

Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi, Novemba 18, 2024 Massawe aliyekuwa fungate baada ya kufunga ndoa, alitoa taarifa kwa marafiki zake kuwa alikuwa Mbezi anafuatiliwa na gari ambalo halijui.

Tangu siku hakuonekana wala kupatikana kwenye simu zake.

Hata hivyo, Desemba 17, 2024 Kamanda wa Polisi Kanda ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro alitoa taarifa za kukamatwa kwake.

Kamanda Muliro alisema Massawe alikamatwa Desemba 15, 2024, akiwa kwa mganga wa kienyeji, Pemba na alikuwa na tuhuma za wizi.

Alieleza kuwa, kutokana na tuhuma hizo, ndio maana alitengeneza mazingira ya uwongo kwamba amepotea kisha akaenda kujificha kwa mganga huyo wa kienyeji.

Hata hivyo, alipopandishwa kizimbani na kusomewa mashtaka hayo, Massawe alikana kutenda makosa hayo na aliachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti aliyopewa.