
Dar es Salaam. Kwa mara nyingine Serikali imeieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Dar es Salaam, Kisutu kuwa upelelezi wa kesi ya wizi wa gari na fedha inayomkabili mfanyabiashara Vicent Masawe (36), maarufu “Bwana harusi,” haujakamilika.
Masawe anakabiliwa na mashtaka mawili ambayo ni wizi wa gari aina ya Toyota Ractis lenye thamani ya Sh15 milioni ambalo aliazimwa kwa ajili ya kulitumia katika sherehe ya harusi yake na pia kujipatia fedha taslimu Sh3 milioni kwa njia ya udanganyifu.
Kesi hiyo namba 35738/2024 inayosikilizwa na Hakimu Mkazi Mkuu Beda Nyaki, imetajwa leo Jumatano, Februari 12, 2025 kwa mara ya pili kwa ajili ya kuangalia kama upelelezi umeshakamilika.
Hata hivy,o wakati kesi hiyo ilipoitwa mbele ya Hakimu Mkazi, Ana Magutu kwa niaba ya Hakimu Nyaki ambaye yuko likizo, mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Cathbert Mbilingi, amesema bado upelelezi haujakamilika na akaiomba Mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Hivyo, Hakimu Magutu ametoa siku 30 nyingine kwa upande wa mashtaka kukamilisha upelelezi na ameahirisha kesi hiyo mpaka Machi 12, 2025, kesi hiyo.
Wakati kesi hiyo ikifunguliwa kabla ya upelelezi kukamilika, kifungu cha 131A (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) kama ilivyorekebishwa mwaka 2022, kinazuia mashauri ya jinai kupelekwa mahakamani kabla ya upelelezi kukamilika.
Hata hivyo, kwa mujibu wa kifungu kidogo cha (4) cha kifungu hicho, kuna makosa ambayo kesi inaweza kufunguliwa hata bila upelelezi kukamilika, yaliyotajwa ni makosa makubwa hasa yake yasiyo na dhamana. Mashtaka yanayomkabili Massawe si miongoni mwa hayo.
Mshtakiwa huyo ambaye yuko nje kwa dhamana, alipandishwa kizimbani mahakamani hapo kwa mara ya kwanza na kusomewa mashtaka hayo Desemba 24, 2024.
Katika shtaka la kwanza la wizi wa kuaminika, Masawe anadaiwa kuwa akiwa wakala, Novemba 15, 2024 katika Jiji la Dar es Salaam, aliiba gari lenye namba za usajili T 642 EGU aina ya Toyota Ractis.
Gari hilo lenye thamani ya Sh15 milioni, kwa mujibu wa upande wa mashtaka ni mali ya Silvester Masawe.
Anadaiwa kuwa aliazimwa gari hilo na Silvester kwa lengo la kulitumia katika sherehe ya harusi yake, lakini baada ya hapo, hakurudisha gari kama ambavyo walikubaliana.
Katika shtaka la pili la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, anadaiwa kuwa tarehe hiyohiyo katika Jiji la Dar es Salaam, kwa lengo la kuiba na kutapeli, alijipatia fedha taslimu Sh 3 milioni kutoka kwa Silvester.
Anadaiwa kuwa alijipatia fedha hizo kwa kuahidi kuwa atamrudisha baadaye, wakati akijua kuwa ni uongo na hakurudisha fedha hizo.
Kabla ya kukamatwa na kisha kufikishwa mahakamani na kusomewa mashtaka hayo, Massawe mkazi wa Ungindoni, Kigamboni jijini Dar es Salaam alidaiwa kupotea.
Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi, Novemba 18, 2024 Massawe ambaye alikuwa fungate baada ya harusi alitoa taarifa kwa marafiki zake, kuwa alikuwa Mbezi na kwamba alikuwa anafuatiliwa na gari ambalo halijui.
Tangu siku hiyo hakuonekana wala kupatikana kwenye simu zake.
Hata hivyo, Desemba 17, 2024 Kamanda wa Polisi Kanda ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro alitoa taarifa za kukamatwa kwake.
Kamanda Muliro alisema Massawe alikamatwa Desemba 15, 2024, akiwa kwa mganga wa kienyeji, Pemba.
Hata hivyo alipopandishwa kizimbani na kusomewa mashtaka hayo, Massawe alikana kutenda makosa hayo, na aliachiwa kwa dhamana.