
Dar es Salaam. Serikali imeieleza Mahakama bado inaendelea na uchunguzi katika kesi ya kusambaza taarifa za uongo inayomkabili Meya wa zamani wa Kinondoni na Ubungo, Boniface Jacob, maarufu Boni Yai.
Mshtakiwa huyo anakabiliwa na mashitaka mawili ya kuchapisha taarifa za uongo kwenye mtandao wake wa X (zamani Twitter).
Kesi hiyo iliitwa leo Jumanne, Machi 11, 2025 kwa ajili ya kutajwa na Wakili wa Serikali, Frank Rimoy amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Franco Kiswaga, kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado unaendelea.
Wakili Rimoy amedai pia wanasubiri uamuzi Mahakama ya Rufani baada ya mshtakiwa huyo kufungua shauri la maombi ya mapitio huko, kupinga uamuzi uliotolewa na Mahakama Kuu kuhusiana na kesi hiyo.
Hakimu Kiswaga baada ya kusikiliza maelezo hayo, ameahirisha kesi hiyo hadi Aprili 10, 2025 kwa ajili ya kutajwa na mshtakiwa yupo nje kwa dhamana.
Kiini cha shauri la Mahakama ya Rufani
Kiini cha shauri hilo lililopo Mahakama ya Rufani, kinatokana na Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni (RCO), Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP), David Msangi kuwasilisha maombi akiiomba Mahakama ya Kisutu imuamuru mshtakiwa Boni Yai kutoa nywila (password) za simu zake mbili za mkononi kwa ajili ya uchunguzi wa tuhuma hizo.
Maombi hayo yaliamuriwa upande mmoja, ambapo Mahakama hiyo ilimuamuru Boni Yai kufika ofisi ya RCO na kutoa nywila kufungua simu zake mbili za mkononi aina ya Samsung Galaxy S20 Ultra SG na Samsung Galaxy S23 Ultra.
Boni Yai kupitia Wakili wake Hekima Mwasipu alifungua shauri la maombi ya mapitio Mahakama Kuu, chini ya hati ya dharura, akiiomba Mahakama hiyo iitishe kumbukumbu za mwenendo wa Mahakama ya Kisutu, ijiridhishe na usahihi na uhalali wake, hatimaye itengue amri hiyo, akidai kuwa ilitolewa bila kumpa haki ya kusikilizwa.
Hata hivyo Serikali iliibua pingamizi la awali likipinga shauri hilo lisisikilizwe kwa kuwa ni batili kisheria huku ikitoa sababu mbili.
Mahakama Kuu katika uamuzi wake uliotolewa na Jaji Anold Kirekiano Novemba 28, 2024, ilitupilia mbali maombi ya Jacob, baada ya kukubaliana na pingamizi lililoibuliwa na Serikali kuwa shauri hilo ni batili na limekiuka kifungu cha 43(2) cha Sheria ya Mahakama za Mahakimu (MCA), sura ya 11 marejeo ya mwaka 2019.
Hata hivyo, Jacob hakukubaliana na uamuzi huo wa Mahakama Kuu, hivyo alifungua shauri la maombi ya mapitio Mahakama ya Rufani kupinga uamuzi huo wa Mahakama Kuu, na sasa wanasubiri kupangiwa tarehe ya usikilizwaji.
Katika kesi ya msingi, Boni Yai anakabiliwa na mashitaka mawili, ya kuchapisha taarifa za uongo katika mfumo wa kompyuta katika akaunti ya X yenye jina la Boniface Jacob @Ex MayorUbungo kwa nia ya kupotosha umma kinyume na kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Kimtandano namba 14 ya mwaka 2015.
Katika shitaka la kwanza, Boni anadaiwa Septemba 12 2024 jijini Dar alichapisha taarifa za uongo zikimuhusisha Mkuu wa Upelelezi wa Kanda (ZCO) ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP).
Taarifa hizo zinasomeka kuwa:
“Mafwele anatuhumiwa na familia nyingi kama mtu ambaye ameshiriki mauaji katika kuwapoteza ndugu wa baadhi ya familia zao, kupotea kwa mfanyabiashara Mussa Mziba, kupotea kwa Deo Mugasa, kupotea kwa Adinani Hussein Mbezi, kupotea kwa vijana watano wa Aggrey,” amesema.
Katika shitaka la pili, mshtakiwa anadaiwa Septemba 14, 2024 jijini Dar es Salaam alichapisha taarifa za uongo kuwa zinazowahusisha wakuu wa upelelezi wa mikoa na utekaji, mauaji ya watu na kutupa miili yao.
Ujumbe huo inasomeka kuwa:
“Mkawasifia Ma-RCO (Wakuu wa Upelelezi Mikoa) wanaozuia uhalifu kwa kutenda uhalifu …, bali Ma-RCO waliokuwa wakiteka, kukamata, kupiga watuhumiwa risasi, kuwafunga tape, kuwafunga mifuko ya nailoni usoni na kisha kutupa miili ya watuhumiwa ndio wanaijua kazi ya upolisi.”
Kwa mara ya kwanza, mshtakiwa huyo alifikishwa mahakamani hapo Septemba 19, 2024 kujibu mashitaka yanayomkabili.