Upatu unavyozidi kuwa janga

Dar es Salaam. Ni janga, hivi ndivyo ilivyoelezwa na wataalamu wa masuala ya fedha na uchumi walipozungumzia utamaduni wa watu wengi kuchagua michezo ya kupeana kama njia ya kutunza fedha zao.

Hili limekuja kukiwa na matukio ya watunza fedha katika michezo hii wanaojulikana kama vijumbe kukimbia na fedha hizo au kushindwa kukamilisha mzunguko wa mchezo husika hali inayosababisha baadhi ya wachezaji kupoteza fedha zao.

Tukio la hivi karibuni ni lile linalomhusu mwigizaji Joyce Mbaga maarufu Nicole Berry kushikiliwa na Jeshi la Polisi Kanda maalumu ya Dar es Salaam kwa tuhuma za kujipatia kiasi cha Sh100 milioni kwa njia ya udanganyifu.

Mwigizaji huyo anadaiwa kutengeneza makundi ya upatu na kukusanya fedha za watu kwa lengo la kuchezesha michezo ya kupeana.

Mwananchi imebaini kuwa watu wengi wanapoteza fedha kupitia michezo hiyo kutokana na vijumbe au wachezaji kukosa uaminifu.

Akizungumza leo Alhamisi Machi 6, 2025 na Gazeti la Mwananchi, mkazi wa Tandika Mabatini, Katija Ismail amesema  ni miongoni mwa waliowahi kukutana na utapeli kwenye mchezo,  kijumbe wao alihama ghafla kwenye nyumba aliyokuwa anaishi kabla ya kukamilika kwa mzunguko wa fedha.

“Kinachotuponza ni uaminifu, huku uswahilini tunaaminiana sana halafu hiyo michezo ndiyo inatusaidia kuendesha maisha. Si kwamba hatukutani na majanga wakati mwingine tunapoteza fedha.

“Imewahi kutokea kuna kijumbe wetu aliondoka na hajarudi hadi leo, mchezo ulikuwa mdogo tu wa Sh3,000 alikusanya hela kwa watu wote  halafu akapotea, inawezekana alipata shida lakini haibadili maana kwamba ameondoka na fedha zetu,” amesema Katija.

Hata hivyo, Katija amesema tukio hilo halijamfanya kuikwepa michezo kwa kile alichoeleza kuwa, ina msaada mkubwa hasa kwa watu wa hali ya chini.

“Wakati mwingine tunaingia kwenye michezo kwa sababu ya hatuwezi kutunza fedha wenyewe, kupitia mchezo wa Sh100,000 kwa mwezi naweza kukusanya ada na kodi, lakini nikisema niweke hiyo fedha nina uhakika sitoboi, nitaitumia tu.

“Hata hivyo, siingii kwenye mchezo bila kuwa na uhakika na makazi na shughuli anayofanya huyo kijumbe au watu ninaocheza nao, kama mtu hana shughuli inayoeleweka ni rahisi kutapeli,”amesema Katija.

Mwanasaikojia, John Ambrose amesema watu kupenda upatu ni matokeo ya kukosa nidhamu ya fedha, hivyo kulazimika kutafuta njia ya kuweka kidogo kidogo.

“Kuna wale ambao wana tabia ya kukosa nidhamu ya fedha, sasa hii ikikomaa ndiyo anashindwa kabisa kujiamini kutunza fedha yake, hivyo atahitaji usaidizi kwenye hilo ndipo anapotafuta mchezo.

“Siwezi kusema kwamba ina ubaya moja kwa moja, lakini kuna watu inawasaidia kwa sababu akijua kuna pahala anatakiwa kupeleka fedha kila siku, wiki au mwezi hivyo atalazimika kuongeza juhudi kwenye kutafuta,” amesema Ambrose.

Nini kinasababisha haya

Kukosekana kwa elimu ya fedha, milolongo ya taasisi rasmi za kuhifadhi fedha ni miongoni mwa sababu zinazotajwa kuchangia kushamiri kwa michezo ya upatu.

Mhadhiri wa Uchumi, Dk Abel Kinyondo amesema kukosekana kwa elimu ya fedha kunawafanya watu kutafuta njia rahisi za kuweka na kupata fedha bila kujali hatari iliyo mbele.

Amesema watu wanakimbilia kwenye michezo ya upatu kwa sababu ni jukwaa rahisi la kuweka fedha lisilo na vigezo wala masharti magumu zaidi ya kujuana.

“Huku dhamana ni kujuana, mtu anaona ni heri aweke fedha zake kwa mtu anayemjua kuliko kupeleka benki au kwenye mitandao ya simu kwa sababu ya kukwepa hatua za kufuata. Wakati mwingine mtu anaona shida hata kuwasilisha viambatanisho kumuwezesha kufungua akaunti benki,”amesema Dk Kinyondo.

Pia, amesema hatari ya michezo hiyo ni pale mtu anapoingia kwenye umaskini baada ya kupoteza fedha zake alizowekeza.

Amesema kukabiliana na hilo ni vyema Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ikawekeza kwenye utaoji wa elimu ya fedha kwa umma.

“Hili ni jukumu la BoT, itoe elimu ya fedha, watu wajue sehemu zipi wanaweza kuweka fedha zao zikawa salama na wakapata faida inaweza kuwa benki au kwenye mifuko ya uwekezaji,”amesema Dk Kinyondo.

Hoja hiyo  imeelezwa pia na mtoa elimu ya fedha aliyethibitishwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Dk Amani Makirita.

Dk Makirita amesema kinachowafanya watu wengi kuikimbilia michezo ni matokeo ya kukosa elimu ya fedha na kujikuta wakitaka fedha za haraka.

Amesema tofauti na inavyoonekana na wengi kwamba michezo ni watu wenye kipato cha chini, hata watu wenye vipato vikubwa wanaingia kwenye michezo hiyo kwa sababu ya tamaa na kufuata mkumbo.

“Watu wana matamanio ya kupata fedha nyingi kwa pamoja anaona bora aende kwenye upatu, huyu mtu hana elimu ya fedha kwa sababu angekuwa nayo angepeleka kwenye njia nyingine za uwekezaji.

“Hapa Tanzania sasa hivi kuna njia nyingi za kuwekeza fedha, kuna mifuko kama UTT unaweka fedha zako kidogo kidogo na unapata faida lakini haya hayawezi kuwa rahisi kueleweka kama watu hawana elimu ya fedha,”amesema Dk Makirita.

Mwanasaikolojia wa uchumi Gaston Mtweve amesema taasisi za kifedha zinapaswa kutengeneza mazingira rafiki kwa watu wa makundi yote ili kuvutiwa na huduma za kifedha.

“Mtu anaona hawezi kuweka fedha na hawezi kufuata michakato ya benki, wakati mwingine anakwepa gharama kwa sababu benki ukitaka kutoa hela yako unakutana na makato.

“Mtu anaona ni heri aweke fedha yake kwa kijumbe, halafu ilivyo kwa kiasi kikubwa hawa vijumbe ni watu wenye ushawishi hivyo ni rahisi kwao kuaiminika sasa, akiwa sio mwaminifu ndipo majanga yanaweza kutokea,” amesema  Mtweve.

“Athari ya hili ni watu kuingia kwenye umaskini, inawezekana ikasababisha hata migogoro kwenye familia maana wapo ambao wanabana matumizi ya familia ili apeleke hela kwenye mchezo halafu mwisho wa siku anashindwa kuipata hela yenyewe.”

Hata hivyo, Mtweve amesema michezo inaweza kuwa na tija endapo itawekewa utaratibu mzuri kwa kuondoa mianya yote inayoweza kusababisha mtu kukimbia na fedha.

“Serikali inapiga marufuku hii michezo kwa kuwalinda wananchi wake dhidi ya matukio ya utapeli lakini ukweli ni kwamba hii michezo ipo. Kwa sababu hiyo ni vyema ikaiwekea mifumo ya udhibiti na wananchi wawe tayari kuchangia gharama za uendeshaji itakapoonekana kuna haja ya kufanya hivyo,”amesema Mtweve.