
Dar es Salaam. Baada ya mkwamo wa takribani miaka 10 wa upatikanaji wa Katiba mpya, sasa mchakato huo utaamuriwa na Mahakama kutokana na shauri la kikatiba lililofunguliwa ili kukwamua na kuhitimisha mchakato huo.
Shauri hilo limefunguliwa Mahakama Kuu Masjala Ndogo, Tabora na Mwa-nasheria, Alexander Barunguza dhidi ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC, zamani Tume ya Taifa ya Uchaguzi – Nec) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Shauri hilo la maombi mchanganyiko namba 3965/2025 limepangwa kuanza kusikilizwa Machi 19, 2025 na Jaji Zain-abu Mango katika hatua ya awali ya uchunguzi wa ustahilifu wake.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mahakama hiyo Februari 21, 2025, kwenda kwa wadaawa kuwajulisha tarehe ya usikilizwaji wa shauri hilo, shauri hilo limepangwa kuanza kusik-ilizwa tarehe hiyo kuanzia saa 5:00 asubuhi.
“Unatakiwa kufika katika mahakama hii bila kukosa na unatakiwa kuwasilisha siku hiyo nyaraka zote unazokusudia kuzitumia katika kuunga mkono kesi yako,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo ya wito kwa wadaawa, ambayo Mwananchi limeiona nakala yake.
Katika shauri hilo, Barunguza pamoja na mambo mengine anaiomba Mahakama hiyo iamuru wadaiwa wafanye mareke-bisho ya Sheria ya Kura ya Maoni na pia iamuru upigaji wa kura ya maoni ufan-yike wakati wowote kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Yaliyojiri mchakato wa Katiba Mpya
Mchakato wa Katiba mpya ulianza rasmi mwaka 2011 zilipotungwa sheria za ku-ratibu na kuwezesha upatikanaji Katiba Mpya.
Hizi ni Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Namba 83/2011 iliyoelekeza kuundwa vyombo vya kuratibu utekelezaji mcha-kato huo, yaani Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Mabaraza ya Katiba na Bunge Maalum la Katiba (BMK) na Sheria ya Kura ya Maoni Namba 11/2013.
Sheria hizo ziliainisha namna ya ushiriki wa wananchi katika hatua zote za mchakato wa utungwaji Katiba Pen-dekezwa na hatua na utaratibu wa upi-gaji kura ya maoni Katiba Pendekezwa.
Tume ya Mabadiliko ya Katiba ili-yoongozwa na Waziri Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Warioba iliratibu mchakato wa kukusanya maoni ya wananchi na kuandaa Rasimu ya Kwanza ya Katiba iliyohaririwa na Mabaraza ya Katiba na kupata Rasimu ya Pili ya Katiba.
Rasimu ya Pili ya Katiba iliwasilishwa kwenye Bunge Maalumu la Katiba am-balo licha ya mvutano wa kiitikadi wa wajumbe uliosababisha baadhi ya wajumbe wa kususia majadiliano na kuunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), lilijadili na Oktoba 2, 2014 lil-ipitisha Katiba Pendekezwa.
Oktoba 8, 2014, aliyekuwa mwenyekiti wa Bunge hilo la Katiba, Samwel Sitta aliikabidhi Katiba Pendekezwa kwa Rais wa wakati huo, Jakaya Kikwete, am-bayo ilizinduliwa rasmi siku hiyo kwa ajili ya kuendelea na hatua nyingine.
Mkwamo wa mchakato
Kwa mujibu wa Sheria ya Kura ya Maoni, kama alivyoirejea Barunguza, ndani ya siku 14 baada ya kupokea Kati-ba Pendekezwa, Rais alipaswa kuchap-isha katika Gazeti la Serikali, amri kuiele-keza Nec kuanzisha mchakato wa kura ya maoni.
Mchakato huo ni pamoja na kuchapish-wa kwa Katiba Pendekezwa, kuainisha muda wa kuanza kampeni za kura ya maoni, tarehe ya kupiga kura, kuandaa na kuchapisha wa swali la kura ya maoni ndani ya siku saba baada ya Katiba Pen-dekezwa kuchapishwa.
Mambo mengine ni ndani ya siku 14 baada ya kuchapishwa swali la kura ya maoni, kutoa taarifa kuainisha muda wa uhamasishaji na kutoa ufahamu kwa umma kuhusu kura ya maoni.
Hata hivyo, mchakato wa kura ya maoni ulikuwa unagongana na shughuli ya kuboresha Daftati la Kudumu la Usajili wa Wapigakura kwa mufumo wa Biometric Voters Registration (BVR), kupelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2015.
Hivyo waziri mwenye dhamana ya uchaguzi, Waziri Mkuu akitumia kifungu cha 51 cha sheria hiyo kupitia GN namba 383 la Oktoba 17, 2014 alifanya ma-rekebisho ya sheria hiyo, yaliyompa Rais mamlaka huria kutangaza tarehe ya kampeni na ya kupiga kura ya maoni.
Kupitia GN hiyo, amri ya Rais iliandali-wa na Rais alitangaza kampeni za kura ya maoni zingeanza Machi 30 mpaka Aprili 29, 2015, (siku 31) na tarehe ya kupiga kura ya maoni Aprili 30, 2015.
Tarehe hiyohiyo, Oktoba 17, 2014, Nec kupitia GN namba 414A ilichapisha swali la kura ya maoni lililouliza; “Unaikubali Katiba Inayopendekezwa?”
Hata hivyo, Aprili 2, 2015 Tume, ili-tangaza kuahirisha kura ya maoni ya Katiba Pendekezwa kutoka Aprili 30, 2014 hadi itakapotangazwa tena. Mpaka leo haijatangazwa.
Sababu Barunguza kwenda mahaka-mani
Barunguza anadai alishiriki kikamilifu katika mchakato wa mabadiliko ya Kati-ba kuanzia ukusanyaji wa maoni mpaka utungwaji wa Katiba Pendekezwa na kwamba kilichobakia ni hatua ya upigaji kura ya maoni.
Anadai kuwa, Nec haikutekeleza wajibu wake wa kikatiba kutekeleza masharti ya Sheria ya Kura ya Maoni ndani ya muda uliolezwa kwa takribani miaka 10 sasa.
Anadai wadaiwa wamezuia utekelezaji wa mchakato huo bila kuueleza umma sababu au kwa sababu zisizo wazi na halali, bila kushauriana na kuhusisha ushiriki wa wananchi, wala bila kujali muda, fedha na raslimali zilizotumika katika mchakato wote.
Barunguza anadai huo ni ukiukwaji wa Ibara ya 18(d) ya Katiba, inayotoa haki ya kupewa taarifa muda wote kuhusiana na matukio muhimu ya maisha na shughuli za watu na masuala yenye umuhimu kwa jamii.
Hivyo, anadai kuwa kusitishwa mcha-kato huo kumemnyima fursa ya kikatiba kunufaika na haki zake za kikatiba ku-shiriki katika mambo ya nchi na haki yake ya kufahamishwa sababu za kusit-ishwa kwa zaidi ya miaka tisa sasa ime-kiukwa.
Pia, anadai kuwa amenyimwa haki yake ya kuwa na nchi ya kidemokrasia ina-yozingatia utawala wa sheria na mgawanyo wa madaraka, kwa kuwa Katiba ya mwaka 1977 haikutokana na mchakato shirikishi.
Vilevile anadai kuwa si yeye tu pekee aliyeathirika na mkwamo huo, bali hata Watanzania wengi walitoa maoni yao kwa upana yaliyowezesha Katiba Pendekezwa.
Nafuu anazoziomba
Kutokana na mkwamo huo wa kura ya maoni, Barunguza anaiomba Mahakama itoe tamko na amri:
Kwamba Nec/Inec ilikuwa na wajibu kikatiba kutekeleza masharti ya Sheria ya Kura ya Maoni ndani ya muda uli-oelezwa na kutokutekeleza masharti hayo ilikiuka Katiba Ibara ya 26(1), ina-yotoa wajibu kila mtu kufuata na kutii Katiba na Sheria.
Wadaiwa kuzuia mchakato wa Katiba kwa zaidi ya miaka tisa ni kinyume na ibara ya 21(1) na (2) ya Katiba ya Nchi, kuhusu haki ya raia wote kushiriki katika masuala ya umma na Mkataba wa Kima-taifa kuhusu Haki za Kiraia na Kisiasa (ICCPR).
Pia, kati ya sasa na Aprili 2025 wadaiwa wafanye marekebisho yote muhimu ya Sheria ya Kura ya Maoni kuwezesha upi-gaji kura ya maoni, muda wowote kabla ya Julai 30, 2025 au kabla ya kuanza kwa uchaguzi mkuu Oktoba/Novemba 2025.