WASHINGTON. Baada ya uchaguzi wa Marekani kukamilika jana na Donal Trump kuongoza katika matokeo ya jumla, rasmi atakuwa Rais wa 47 wa nchi hiyo ikiwa ni muhula wake wapili kuchaguliwa.
Trump ambaye amejizolea umaarufu zaidi kupitia siasa, ni miongoni mwa marais wa Marekani ambao wamekuwa na ushiriki mkubwa katika michezo.
Leo tumekuletea upande wake wa pili mbali ya siasa na amekuwa akishiriki michezo mbalimbali na kumekuwa na maswali nini Marekani itafanya chini yake wakati inaandaa mashindano ya Kombe la Dunia mwaka 2026.
ANAVYOSHIRIKI
Trump ni muumini na shabiki mkubwa wa mchezo wa Gofu, hivi karibuni wakati wa kampeni zake za uchaguzi, alinusurika kuuawa akiwa kwenye kiwanja cha mchezo huo.
Kutokana na mahaba yake na mchezo huu, Trump ameanzisha hadi klabu yake ya gofu inayomiliki eneo kubwa lenye viwanja na huwa inaandaa michuano mbalimbali. Viwanja na ofisi za klabu hii vipo huko New York, Marekani.

Mbali ya Golf, Trump pia ni mdau mkubwa wa mchezo wa mieleka na katika miaka 2000 alidiriki hadi kuwekeza.
Mara kadhaa ameonekana ulingoni akishiriki shughuli mbalimbali za mchezo huo na katika mechi ya WrestleMania 23 mwaka 2007, aliwekeana dau na Mwenyekiti wa WWE, Vince McMahon waitishe pambano na kila mmoja awe na wapiganaji wake na atakayeshinda aidha Vince au Trump mmoja wao atanyolewa nywele.
NI KOMBE LA DUNIA LA TRUMP
Mashindano hayo yanayotarajiwa kuanza Juni 19 hadi Julai 19 yatapigwa katika mataifa matatu na mbali ya Marekani, yatachezwa Canada na Mexico lakini Marekani ndio ina viwanja vingi zaidi (10), vya kuchezea mashindano hayo.
Moja kati ya maswali ni namna ambavyo nchi hiyo itawekeza katika kuandaa mashindano na watu wengi wakitarajia kuona vitu vya kipekee kama ilivyokuwa katika mashindano yaliyopita yaliyofanyika Qatar ambako makontena yakitumika kama hoteli.
Ingawa hiyo itakuwa ngumu kwa nchi kama Marekani ambayo imeshajitengenezea miundombinu imara kwa muda mrefu lakini nchi yoyote inayoandaa michuano huyo huwa na kitu cha kuvutia ambacho huandaliwa ili kuvutia zaidi wageni wanaokwenda kutazama mashindano hayo.

Timu ya taifa ya Marekani pia inasubiriwa kwa hamu kuonyesha itafanya nini kwani katika historia ya michuano hii, hatua ya juu zaidi iliyowahi kufika ilikuwa ni kumaliza nafasi ya tatu mwaka 1930.
Katika mashindano haya yatakayofanyika katika ardhi ya nyumbani kwao mashabiki watataka kuona timu hiyo yenye mastaa kama Christian Pulisic na Weston McKennie.