Upande huu Joh Makini ana dunia yake!

Dar es Salaam. Popote duniani muziki wa Hip Hop na RnB unapokutana inazaliwa ladha moja ya kipekee masikioni mwa msikilizaji na umekuwa ni utamaduni wa miaka mingi kwa wasanii wanaofanya aina hizo za muziki kushirikishana katika nyimbo zao.

Ndani ya Bongofleva hilo limekuwa likifanyika pia, sauti ya Joh Makini kutoka kundi la Weusi imekuwa kipenzi cha wasanii wengi wa RnB kitu kilichofanya kushirikishwa na wakali karibia wote wa muziki huo nchini.

Joh Makini aliyeanza rap na kundi la River Camp huko Arusha, alitoka rasmi kimuziki na wimbo wake, Chochote Popote (2006) ambao ulijumuishwa katika albamu yake ya kwanza, Zamu Yangu (2007).

Alishinda Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) kama Msanii Bora wa Hip Hop 2012, hivyo wasanii wa RnB wanapompa nafasi katika nyimbo zao sio kwa bahati mbaya, bali anajua na ni wazi upande huu ana dunia yake kama ifuatavyo.

JO 01

Ben Pol – Wanichora

Zaidi ya kuwa na uwezo mkubwa upande wa uimbaji wa RnB, pia Ben Pol ni mwandishi mzuri wa nyimbo, mathalani amewahi kushinda tuzo ya TMA kama Mtunzi Bora wa Mashairi ya Bongofleva 2013.

Aliamua kumshirikisha Joh Makini katika wimbo wake, Unanichora (2014) uliotayarishwa na Fundi Samweli kutokea Sweden, huku video yake ikisimamiwa na Director Nisher, mshindi wa Tuzo za Watu kama Muongozaji wa Video Anayependwa 2014.

Utakumbuka Ben Pol alitoka kimuziki na wimbo wake, Nikikupata (2010) uliotayarishwa na Duke Tachez, hiyo ni baada ya kusainiwa na lebo ya M Lab ambayo imetoa wasanii wengi wa Hip Hop kama Nikki Mbishi, Stereo, Songa, One The Incredible n.k.

JO 02

Jux – Looking For You

Tangu akiwa na kundi la Wakacha, Jux alijipambanua kama msanii mkali wa RnB, wimbo wake, Sisikii (2014) uliotayarishwa na Bob Manecky kutokea AM Records ulishinda TMA kama Wimbo Bora wa RnB 2015.

Huyu naye alitambua kuwa michano ya Joh Makini inahitajika katika muziki wake ndipo akamshirikisha katika nyimbo zake mbili, Looking For You (2015) uliotayarishwa na Nahreel, pia na kuna Tell Me (2018) kutoka katika mikono ya S2kizzy.

Na hadi sasa Jux ametoa albamu mbili, The Love Album (2019) na King of Hearts (2022), huku wimbo wake, Enjoy (2023) ukiwa ndio wenye mafanikio makubwa YouTube ukitazamwa zaidi ya mara milioni 100 ukiwa ni wimbo wa nane Bongo kufanya hivyo.

JO 03

Rama Dee – Sina Muda

Kwa miaka 20 sasa Rama anatambulika kama msanii mkali wa RnB, wimbo wake, Kuwa na Subira (2012) uliotayarishwa na Nahreel kutoka The Industry huku akilishirikisha kundi la Mapacha (Maujanja Saplayaz) ulishinda TMA kama Wimbo Bora wa RnB 2013.

Ukiachana na Mapacha, Joh Makini ni msanii mwingine wa Hip Hop aliyesikika sana katika nyimbo za Rama Dee, tayari wawili hao wameshirikiana katika nyimbo tatu, Tomorrow (2008), Sina Muda (2008) na Furaha Yetu (2018).

Ikumbukwe kuwa sauti ya Rama Dee ndio inasikika mwanzoni mwa wimbo wa Professor Jay, J.O.S.E.P.H (2006), na yeye na wenzake ndio waliimba kiitikio cha wimbo huo uliobeba jina la albamu ya tatu ya rapa huyo aliyetoka na kundi la Hard Blasterz Crew (HBC).

JO 04

TID – Confidence

Baada ya kushirikiana na wakali wengi wa Hip Hop Bongo akiwamo Professor Jay, King Crazy GK, Fid Q, AY, Jay Moe, Ngwea na wengineo, TID akaona sauti ya Joh Makini bado inaweza kuwa na nafasi kwenye muziki wake.

Basi wakaingia studio na kurekodi wimbo, Confidence (2016) huku sauti ya Dully Sykes ikisikika mwishoni ingawa hakutokea kwenye video ya wimbo huo kwa kile kinachodaiwa alikuwa hakubaliani na aina ya muziki wanaofanya Weusi.

Utakumbuka albamu yake ya kwanza, Sauti ya Dhahabu (2002) ilipoingia sokoni ilimpatia TID kitita cha Sh30 milioni, fedha hiyo ikagharamikia video chache alizofanya, pamoja na kumlipa P-Funk Majani, hivyo akabakiwa na Sh22 milioni.

JO 05

Belle 9 – Vitamin Music

Amekuwapo kwenye muziki kwa kipindi cha miaka zaidi ya 10, baadhi ya mashabiki wanamuita Mfalme wa RnB Bongo ingawa majina ya wasanii wengine kama Jux, Ben Pol na Rama Dee yamekuwa yakipewa heshima hiyo pia.

Belle 9 alimshirikisha Joh Makini kwenye wimbo wake, Vitamin Music (2014), na kutokana na kufanya vizuri kwa wimbo huu ndipo akaamua kufungua kampuni ya kusimamia muziki wake aliyoipa jina la Vitamin Music Group (VMG).

Kabla ya Belle 9 kuanza kusikika akiimba muziki mzuri wa RnB, mwanzo kabisa alikuwa akichana lakini baadaye akabadilika ndipo akatoka wimbo wake, Sumu ya Penzi (2009), kisha kusikika katika viitikio vya nyimbo nyingi za Hip Hop Bongo. 

Ukiachana na hao, wasanii wengine wa RnB waliomshirikisha Joh Makini katika nyimbo zao ni pamoja na Q Jay (Sitorudi), TK Nendeze (Away), Damian Sol (Ni Penzi), Otuck William (Push It), Barakah The Prince (Permanent Love) n.k.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *