Uongozi bora katika urutubishaji wa chakula, uboreshaji wa afya ya uzazi wampa Rais Samia tuzo

Hivi karibuni Rais Samia Suluhu Hassan alitunukiwa tuzo ya Gates Foundation Goalkeepers kutokana na kazi kubwa anayofanya katika kupunguza utapiamlo, kuimarisha afya ya wananchi na kuendeleza afya na lishe ya mama, watoto wachanga na vijana. Tuzo hii inaonyesha maendeleo ya Tanzania katika kukabiliana na utapiamlo na kuboresha afya chini ya uongozi wake.

Akizungumza katika hafla ya tuzo hizo Rais Samia Suluhu Hassan alisisitiza dhamira yake ya kuimarisha programu za afya na lishe, akisisitiza urutubishaji wa chakula kama mkakati muhimu.

Urutubishaji wa chakula, mchakato wa kuongeza vitamini na madini muhimu kwa vyakula vinavyotumiwa kwa kawaida, unahakikisha kwamba Watanzania wanapata virutubisho muhimu kupitia vyakula vikuu kama vile mahindi na unga wa ngano.

Kwa kutambua umuhimu wa urutubishaji, hivi karibuni Serikali ilipitisha Sheria ya Urutubishaji, ili kuweka hitaji la kisheria kwa wazalishaji wote wa kibiashara wanaofungasha na kuuza unga wa mahindi na ngano, bila kujali ukubwa wa kiwanda na kuwezesha upatikanaji wa virutubisho ili kuanza kurutubisha bidhaa zao. Sheria hii, inayoungwa mkono na Rais, inasisitiza hitaji la kufuata utaratibu wa urutubishaji miongoni mwa wzalishaji nchini.

Katika kipindi cha miaka sita iliyopita Tanzania imepiga hatua kubwa katika viashiria muhimu vya afya. Kwa mujibu wa Utafiti wa Demografia na Afya Tanzania (TDHS 2022), vifo vya uzazi vimepungua kutoka 556 hadi 104 kwa kila vizazi hai 100,000, huku vifo vya watoto chini ya miaka mitano vimepungua kutoka 67 hadi 43 kwa kila vizazi hai 1,000. Vifo vya watoto wachanga pia vimepungua kutoka 43 hadi 33 kwa kila watoto 1,000 wanaozaliwa hai. Hata hivyo, vifo vya watoto wachanga bado vinatia wasiwasi na kupungua kidogo tu kutoka 25 hadi 24 kwa kila watoto 1,000 wanaozaliwa hai.

Wakati viashiria hivi vikionyesha hatua kubwa katika kupambana na hali hii bado utapiamlo unaendelea kuathiri Watanzania hususani watoto. Udumavu kwa watoto chini ya miaka mitano umepungua kutoka asilimia 34 hadi 30, huku udumavu uliokithiri ukipungua kutoka asilimia 4 hadi 3. Uwepo wa watoto wenye uzito mdogo pia yamepungua kutoka asilimia 14 hadi 12.

Takwimu hizi zinaonyesha kuwa afua za lishe, pamoja na urutubishaji wa chakula, vina faida kubwa kwa Taifa. Hata hivyo, asilimia kubwa ya watoto bado wanaathiriwa na utapiamlo, jambo ambalo linaweza kuwa na matokeo mabaya katika ukuaji wao wa kiakili, kupata elimu na tija ya kiuchumi katika maisha yao ya baadaye.

Ili kuendeleza juhudi hizi, kuna haja ya uwekezaji endelevu katika programu za lishe, hasa zile zinazohakikisha upatikanaji sawa wa vyakula vilivyorutubishwa.

Urutubishaji wa chakula ni kama mojawapo ya mikakati madhubuti ya kushughulikia upungufu wa virutubishi vidogo kwa kiwango kikubwa. Serikali imetekeleza sera zinazotaka vyakula vinavyotumiwa katika maisha ya kila siku kama vile unga na mafuta ya kupikia viongezewe vitamini na madini muhimu. Pamoja na sera hizo, changamoto zinaendelea katika kufikia lengo hili na kuhakikisha kuwa Watanzania wote wananufaika na vyakula vilivyorutubishwa.

Hivi sasa, wazalishaji wengi wa unga, hasa kampuni ndogo na za kati (SMEs), wanakabiliwa na changamoto za urutubishaji kutokana na kutumia malighafi duni zinazopatikana sokoni ambazo hutoa faida kidogo za kiafya huku wengine wakishindwa kupata virutubisho hivyo kwa sababu ni gharama.

Sanku, shirika lenye makao yake makuu Afrika Mashariki ambalo limedhamiria kukabiliana na changamoto hii kwa kuhakikisha viwanda vidogo na vya kati vinakuwa na zana zinazohitajika ili kuimarisha urutubishaji katika bidhaa wanazozalisha kwa gharama nafuu.

Katika kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha lishe, hivi karibuni Sanku ilizindua kiwanda jijini Dar es Salaam, Tanzania, ambacho ni cha kwanza kabisa cha uchanganyaji wa viinilishe Afrika Mashariki na Kati.

Kiwanda hiki kina uwezo wa kuzalisha takriban 150MT za mchanganyiko wa virutubisho kwa mwezi na kinakidhi mahitaji ya wazalishaji wa unga Tanzania, Kenya, Ethiopia, Uganda na kwingineko. Kwa kuwezesha upatikanaji rahisi wa virutubisho vyenye ubora na kwa bei nafuu, kiwanda hiki pia kinawasaidia wazalishaji kufuata sheria za urutubishaji wa chakula huku wakiboresha ubora wa lishe wa bidhaa zao.

Hii ni hatua muhimu katika kuhakikisha kwamba hata wazalishaji wadogo wanashiriki katika juhudi za urutubishaji jambo linalowafanya kuwa sehemu ya uboreshaji wa lishe nchini.

Zaidi ya usambazaji wa virutubisho hivyo, Sanku inatoa teknolojia ya Dosifier bila gharama kwa wazalishaji, kuhakikisha nyongeza sahihi ya virutubishi kwenye unga ambao ni chakula kikubwa cha mamilioni ya Watanzania. Teknolojia ya Dosifier inahakikisha kwamba kiasi sahihi cha vitamini na madini kinaongezwa kwenye unga, kudumisha uthabiti na kufuata viwango vya urutubishaji.

Ufanisi wa mbinu hii ulithibitihswa mkoani Morogoro, ambapo utafiti wa mwaka 2015 ulibaini kuwa ni asilimia 2.5 tu ya kaya zinazotumia unga uliorutubishwa. Baada ya Sanku kufunga mashine 70 za Dosifier mkoani humo, utafiti wa mwisho wa mwaka 2017 uliofanywa na Helen Keller International ulionyesha kuwa asilimia 90 ya kaya katika Wilaya ya Manispaa ya Morogoro zilikuwa zinatumia unga uliorutubishwa. Tangu wakati huo, utaratibu huu umeenea zaidi na juhudi za Sanku sasa zinawafikia watu milioni 10 Afrika Mashariki kila siku.

Hata hivyo, kudumisha urutubishaji wa chakula kunahitaji ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi na washirika wa maendeleo. Ingawa mipango mikubwa ya urutubishaji imetekelezwa, changamoto kama vile kuathiriwa kwa mnyororo wa usambazaji, udhibiti wa kimamlaka na uwezo wa kumudu bei wa bidhaa zilizorutubishwa.

Ili wazalishaji wadogo na wa kati wapate mafanikio katika urutibishaji wa chakula, wanahitaji usaidizi endelevu wa kiufundi, upatikanaji rahisi na bei nafuu wa virutubisho vyenye ubora na mazingira mazuri ya kisera ambayo huchochea juhudi za urutubishaji.

Urutubishaji wa chakula unaendelea kuwa mojawapo ya afua za gharama nafuu katika kuboresha lishe kwani hauhitaji mabadiliko ya tabia kwa watumiaji. Vyakula vilivyorutubishwa hutumiwa kama sehemu ya mlo wa kila siku, vikihakikisha kwamba watu wanapata virutubisho muhimu bila kubadilisha tabia zao za kula.

Wakati Tanzania ikiongeza juhudi zake katika urutubishaji, kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za Serikali, wazalishaji na mashirika kama Sanku ni muhimu. Kwa kuendeleza uwekezaji na ushirikiano, urutubishaji utakuwa sehemu muhimu katika kuboresha matokeo ya afya, hasa kwa jamii zilizo katika mazingira magumu na kuhakikisha kwamba Watanzania wote wanapata chakula chenye lishe.