
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepiga kura siku ya Ijumaa kulitaka jeshi la Rwanda kuacha kuunga mkono kundi la waasi la M23 mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kuwaondoa mara moja wanajeshi wake wote katika ardhi ya Kongo “bila masharti.”
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 2
Matangazo ya kibiashara
M23 imeteka miji miwili mikubwa mashariki mwa Kongo na kuzua hofu ya kutokea kwa vita vikubwa zaidi. Rwanda inakanusha madai ya Kongo na Umoja wa Mataifa kwamba inaunga mkono M23 kwa kuipelekea silaha na wanajeshi. Rwada inadai kujilinda dhidi ya wanamgambo wa Kihutu ambao inawashutumu kwa kusaidia jeshi la Kongo, FARDC.
Azimio la Umoja wa Mataifa lililoandaliwa na Ufaransa “linalaani vikali mashambulizi na kusonga mbele kwa M23 katika mikoa ya Kivu Kaskazini na Kusini kwa msaada wa Jeshi la Ulinzi la Rwanda (RDF)” na kutaka M23 wakomeshe mara moja uhasama na kujiondoa katika maeneo ambayo wamedhibiti.
Azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lazima lipokee angalau kura tisa za kuunga mkono na hakuna kura ya turufu kutoka Marekani, Urusi, China, Uingereza au Ufaransa itakayopitishwa. Wanadiplomasia kadhaa wamesema azimio hilo linapaswa kupitishwa.
Congo inasema Rwanda ilitumia waasi wa M23 kama washirika kupora madini yake kama vile dhahabu na coltan, yanayotumika katika simu za kisasa na kompyuta. Marekani imemuwekea vikwazo waziri wa Rwanda na afisa mkuu wa waasi kwa madai ya kuhusika katika mzozo huo.
Nakala hiyo pia inalaani uungwaji mkono wa wanajeshi wa Kongo “kwa makundi maalum yenye silaha, hususan FDLR [Vikosi vya Kidemokrasia vya Ukombozi wa Rwanda], na inataka kusitishwa kwa uungaji mkono huu na utekelezaji wa haraka wa ahadi zinazolenga kuliangamiza kundi hilo.”
Rwanda inaishutumu Kongo kwa kulishirikisha kundi la FDLR katika mapigano yake. Jeshi la Kongo limeahidi kuwakamata wanajeshi wanaoshirikiana na FDLR, lakini serikali imeendelea kuwatumia wapiganaji wa FDLR kama washirika, walisema wataalamu wa Umoja wa Mataifa mwezi Disemba.
Kundi la M23 limejitolea kutetea maslahi ya Watutsi, hasa dhidi ya wanamgambo wa kabila la Kihutu kama vile FDLR. Kundi la FDLR lilianzishwa na Wahutu waliokimbia Rwanda baada ya kushiriki katika mauaji ya halaiki ya mwaka 1994 yaliyoua karibu Watutsi milioni moja na Wahutu wenye msimamo wa wastani.
Rasimu ya azimio la Umoja wa Mataifa inazitaka DRC na Rwanda kuanza tena mazungumzo ya kidiplomasia ili kufikia azimio la kudumu la amani.
Kuongezeka kwa uasi uliodumu kwa muongo mmoja kumesababisha vifo vya walinda amani kadhaa wa kikosi cha Umoja wa Mataifa nchini Kongo kinachojulikana kwa jina la MONUSCO.
Rasimu ya azimio la Umoja wa Mataifa inaonya kwamba “mashambulizi dhidi ya walinda amani yanaweza kujumuisha uhalifu wa kivita na kwamba kupanga, kuelekeza, kufadhili au kushiriki katika mashambulizi dhidi ya walinda amani wa MONUSCO ni msingi wa vikwazo.”