
Manchester England. Manchester United itakuwa uwanjani tena leo usiku ikijiuliza wakati itakapovaana na Fulham kwenye mchezo wa Ligi Kuu England, Premier.
United imekuwa haina matokeo mazuri kwenye ligi msimu huu, lakini inakwenda kwenye mechi hii ikitoka kupata ushindi muhimu dhidi ya Rangers kwenye mechi ya Kombe la Europa na kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kufuzu hatua ya 16 Bora.
Kocha wa United Rúben Amorim, anasubiriwa kwa hamu kubwa kama leo ataendelea kufanya mabadiliko kwenye kikosi chake kama ambavyo amekuwa akifanya kwenye michezo kadhaa iliyopita, huku mshambuliaji wake Marcus Rashford akisubiri hatma yake klabuni hapo.
Hii ni mechi muhimu kwa United kupata ushindi ikiwa katika nafasi ya 13 na pointi 26 baada ya kucheza michezo 22, kama ikipoteza mchezo huu inaweza kuporomoka zaidi kwenye msimamo wa ligi lakini itakuwa mechi ya pili mfululizo kupoteza baada ya wikiendi iliyopita kulala kwa mabao 3-1 dhidi ya Brighton.
Hata hivyo, inavaana na Fulham ambayo ipo nafasi ya kumi kwenye ligi ikiwa imekusanya pointi 33 katika michezo 22, lakini imekuwa ikionyesha kiwango cha juu sana inapocheza kwenye Uwanja wake wa nyumbani wa Craven Cottage.
Takwimu zinaonyesha kuwa Fulham ndiyo timu ambayo imepiga pasi nyingi zilizofika kwa walengwa kuliko timu nyingine kwenye ligi, lakini ikiwa pia ni kati ya timu iliyopewa penalti nyingi baada ya hadi sasa kuwa nazo nne, jambo ambalo United wanatakiwa kuwa nalo makini.
Fulham imepoteza michezo miwili tu kati ya 11 iliyocheza kwenye Uwanja wake wa nyumbani,jambo ambalo United wanatakiwa nalo makini.
Fulham inatarajiwa kuwakosa beki wake wa kulia Kenny Tete pamoja na winga Reiss Nelson.
Kwa upande wa United yenyewe inatarajiwa kumkosa Luke Shaw, Mason Mount, Victor Lindelof na Jonny Evans.
Matokeo ya mechi za jana EPL
Bournemouth 5-0 Nott’m Forest
Brighton 0-1 Everton
Liverpool 4-1 Ipswich
Southampton 1-3 Newcastle
Wolverhampton 0-1 Arsenal
Manchester City 3-1 Chelsea