United, Chelsea na Tottenham zatinga robo fainali 

Manchester United imefanikiwa kutinga hatua ya robo fainali ya Kombe la Europa baada ya kupata ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Real Sociedad kwenye Uwanja wa Old Trafford.

United imefuzu robo fainali kwa ushindi wa jumla wa mabao 5-2 kwani katika mchezo wa kwanza kule Hispania ilipata sare ya bao 1-1.

Mabao ya United yalifungwa na Bruno Fernandez ambaye alifunga matatu (Hat trick) huku bao lingine likifungwa na Diogo Dalot wakati bao la kufutia machozi la Sociedad lilifungwa na Mikel Oyarzabal.

Baada ya kufunga mikwaju miwili ya penalti, Bruno Fernandez anaongoza kwa kufunga penalti nyingi zaidi ya mchezaji mwingine kwenye mashindano hayo akiwa amefunga tisa.

Pia, nahodha huyu wa United amehusika kwenye mabao 41 akiwa amefunga 24 na kutoa pasi za mwisho 17 ambapo ndiye mchezaji pekee anayeshikilia rekodi hii katika mashindano ya Europa.

United itakutana na Lyon ya Ufaransa katika hatua ya robo fainali itakayofanyika Aprili 10, 2025 ambapo United itaanzia ugenini na kumalizia nyumbani kwenye Dimba la Old Trafford Aprili 17, 2025. 

Tottenham nayo imefuzu robo fainali baada ya kuifunga AZ Alkmaar kwa jumla ya mabao 3-2. Katika hatua ya robo fainali Tottenham itacheza dhidi ya Eintracht Frankfurt.

Timu zitakazo kutana robo fainali ya Europa League

Bodø/Glimt vs Lazio 

Tottenham vs Eintracht Frankfurt

Rangers vs Athletic Club

Lyon vs Manchester United.

Katika mashindano ya Conference League, Chelsea imefuzu hatua ya robo fainali baada ya kuifunga Copenhagen jumla ya mabao 3-1, kwani mechi ya kwanza Chelsea ilishinda mabao 2-1 kabla ya kushinda tena jana bao 1-0.

Chelsea itacheza hatua ya robo fainali na Legia Warszawa ya Poland ambapo itaanzia ugenini Aprili 10, 2025 na kumalizia nyumbani, Stanford Bridge Aprili 17, 2025. 

Ratiba ya robo fainali ya Conference League

Legia Warszawa vs Chelsea

Real Betis vs Jagiellonia

Celje vs Fiorentina

Djurgården vs SK Rapid.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *