
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) jana Ijumaa lilionya kuwa zaidi ya watu milioni tatu wako katika hatari ya kuugua ugonjwa wa kipindupindu nchini Sudan.
UNICEF imesema hayo katika mtandao wa kijamii wa X na kuongezwa kuwa: “Watu milioni 3.1, ikiwa ni pamoja na watoto 500,000 wenye umri wa chini ya miaka 5, wako katika hatari ya kukumbwa na ugonjwa wa kipindupindu Sudan.”
Kwa mujibu wa UNICEF, utoaji wa chanjo nchini Sudan umeshuka hadi asilimia 50 kutoka asilimia 85 ya kabla ya kuzuka vita vya uchu wa madaraka baina ya majenerali wa kijeshi wanaoongoza makundi mawili ya SAF na RSF mwezi Aprili 2023.
Shirika hilo pia limesema: “Zaidi ya asilimia 70 ya hospitali katika maeneo yaliyoathiriwa na vita hazifanyi kazi huku wafanyikazi wa huduma za afya walioko mstari wa mbele wakiwa hawajalipwa mishahara yao kwa miezi kadhaa sasa.”
Tangu vilipozuka vita baina ya majenerali wa kijeshi nchini Sudan hadi hivi sasa, magonjwa ya mripuko kama vile kipindupindu, malaria, surua na homa ya dengue yameenea sana na kusababisha mamia ya vifo.
Mwezi Agosti mwaka huu, Wizara ya Afya ya Sudan ilitangaza mripuko wa kipindupindu nchini humo baada ya kusambaratika mfumo wa mazingira safi kutokana na vita na watu kulazimika kutumia maji machafu.