Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) amesema kuwa watoto wa Ukanda wa Gaza huko Palestina wanahitaji uangalizi wa dharura wa kitiba.
Catherine Russell amesema watoto elfu mbili na mia tano wa Kipalestina katika Ukanda wa Gaza wanahitaji huduma za dharura za kitiba na kusisitiza kuwa, baadhi ya watoto hao wanasumbuliwa na ugonjwa wa saratani.
Awali mashirika ya Umoja wa Mataifa yalisema kuwa, watoto Wapalestina katika Ukanda wa Ghaza wanakufa kwa uchungu kwa kukosa matibabu ya dharura kutokana na utawala wa Kizayuni wa Israel kuwazuia kwenda kupatiwa matibabu nje ya eneo hilo lililowekewa mzingiro baada ya kufungwa kivuko cha Rafah.
Akizungumzia hali hiyo, Msemaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF, James Elder amesema, hapo kabla karibu watoto 300 walikuwa wakisafirishwa kila mwezi kaa ajili ya matibabu, lakini saa idadi hiyo imepungua hadi kiwango cha chini ya mtoto mmoja kwa siku.

Idara ya Habari ya Serikali ya Palestina katika Ukanda wa Ghaza imetangaza katika ripoti yake kuwa, tangu kuanza mashambulizi ya utawala wa Kizayuni wa Israel tarehe 7 Oktoba 2023, karibu raia 43,000 wa Palestina wameuawa shahidi.
Kulingana na ripoti ya idara hiyo, zaidi ya watoto 17,000 na karibu wanawake 12,000 wa Gaza wameuawa shahidi katika mauaji ya kimbari yanayoendelea kufanywa na Israel katika eneo hilo la Palestina.