UNICEF: Kutumiwa watoto kama askari kwenye magenge yenye silaha Haiti kumeongezeka kwa 70%

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF limetangaza kuwa, idadi ya watoto wanaoandikishwa katika makundi yenye silaha nchini Haiti imeongezeka kwa asilimia 70 katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Ongezeko hilo ambalo kwa mujibu wa Unicef halijawahi kushuhudiwa, linaonyesha pia ulinzi kwa watoto umezorota kwa kiwango cha kutisha huku kukiwapo na ongezeko la machafuko katika taifa hilo la Karibea.

Makadirio ya hivi karibuni ya shirika hilo la UN la kuhudumia watoto yanaonyesha kuwa watoto hivi sasa wanajumuisha hadi nusu ya wanachama wote wa megenge yenye silaha, na kuajiriwa watoto hao katika magenge hayo kunachochewa na umaskini uliokita mizizi, ukosefu wa elimu na kuporomoka kwa huduma muhimu nchini Haiti.

Catherine Russell

Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Catherine Russell, amesema: “watoto nchini Haiti wamenaswa katika mzunguko mbaya na wameandikishwa katika magenge yenye silaha ambayo yanazidisha hali yao ya kukata tamaa, na idadi inaendelea kuongezeka. Machafuko na vitisho vimekuwa sehemu ya maisha ya kila siku”.

Taarifa ya UNICEF imeendelea kueleza kuwa, hali katika mji mkuu wa Haiti, Port-au-Prince, inatisha sana, huku watoto milioni 1.2 wakiishi huku wakikabiliwa na tishio la mara kwa mara la kufanyiwa unyanyasaji wa kutumia silaha.

Inakadiriwa kuwa asilimia 25 ya wakimbizi wote wa ndani 703,000 ni watoto, wanaoishi katika hali mbaya na kukabiliwa na vitisho vingi.

Aidha, UNICEF imeonya kwamba ukatili wa kijinsia na ubakaji umekithiri, huku ripoti za Ofisi ya Mwakilishi Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Watoto na Migogoro ya Kivita zikionyesha kuwa, katika mwaka huu pekee kumekuwepo na ongezeko la mara kumi  zaidi la  watoto wanaokabiliwa na ukatili wa kijinsia…/