Msemaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) amekosoa kimya cha Jamii ya Kimataifa kinachoyafanya mauaji ya watoto katika Ukanda wa Ghaza na Lebanon yaonekane jambo la kawaida.
Akizungumza mbele ya waandishi wa habari mjini Geneva, Msemaji wa UNICEF James Elder ameashiria ripoti inayoeleza kwamba sehemu kubwa ya watu karibu 44,000 waliouawa shahidi katika vita vya miezi 13 huko Ghaza ni watoto na akatoa indhari kwa kusema: “kuna hali za kutisha za kufanana kati ya vita vya Lebanon na vita vya Ghaza; na kwa hali hiyo, mauaji ya watoto huko Lebanon nayo pia yanageuzwa kimyakimya kuwa jambo linalokubalika”.

Msemaji wa UNICEF ameashiria kuuawa shahidi zaidi ya watoto 200 nchini Lebanon katika kipindi cha chini ya miezi miwili na akasema: “kuhusiana na hali hii, kimewekwa kigezo cha kutia wasiwasi kiitwacho “jambo la kawaida”.
Kwa mujibu wa maafisa wa afya na tiba wa Palestina katika Ukanda wa Ghaza, tangu vilipoanzishwa vita vya kinyama na mauaji ya kimbari Ukanda wa Ghaza na jeshi la utawala haramu wa Kizayuni wa Israel Oktoba 7, 2023, maelfu ya watoto wa Kipalestina wameuawa shahidi na kuna idadi ya wengine wengi miongoni mwao ambao wamepatwa na majeraha ya milele ya kimwili na kiakili…/